January 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mo Dewji akubali yaishe kwa Dk. Kigwangalla

Spread the love

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya timu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ amemwomba radhi Mbunge wa Nzega Vijijini (CCM), Dk. Hamis Kigwangalla kwa yaliyotokea baina yao. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Mo Dewji amechukua uamuzi huo leo Jumatano tarehe 25 Novemba 2020 ikiwa zimepita siku nne tangu Dk. Kigwangalla naye kumwomba radhi mwekezaji huyo wa Simba.

Kama ilivyokuwa kwa Dk. Kigwangalla aliyetumia akaunti zake za kijamii kuandika maelezo marefu ya kumwomba radhi mwenyekiti huyo na jinsi walivyokutana, naye Mo Dewji ametumia njia hiyo hiyo na picha ileile kuomba wasameheane na waendelee kuijenga Simba.

“Nia njema ni tabibu, nia njema ni ibada. Sote tuna mapenzi ya dhati na Simba, hata tulipokwazana ilikua katika nia njema kwenye maendeleo ya timu yetu. Naomba radhi nilipokosea na mimi uliponikosea nishasamehe. Tuijenge Simba pamoja sasa,” ameandika Mo Dewji.

        Soma zaidi:-

Sintofahamu kati ya Dk. Kigwangalla na Mo Dewji ilikuja mara baada ya Kigwangalla ambaye pia ni mwanachama wa klabu hiyo kutilia shaka uteuzi wa mtendaji mkuu wa sasa wa Simba, Barbara Gonzalenz Septemba 2020 kupitia ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter na kuandika kuwa kilichofanyika kwenye uteuzi huo ni ujanja ujanja.

Aidha Kigwangallah aliendelea kwa kuandika kuwa mabadiliko yaliyompa Mo Dewji kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ndani ya Simba hayajakamilika kwa kuwa hajalipa Sh. 20 bilioni na yeye kushangaa kwa nini anafanya uteuzi huo.

Mara baada ya kuandika hivyo, muda mfupi uliofuata Mo Dewji aliandika kwa kumjibu juu ya mjadala huo kwa kusema kuwa si kitu kizuri kuomba mtu yoyote apigwe mawe na kueleza swala la uwekezaji wake ameshalizungumza kwenye vyombo vya habari na alifika mbali na kueleza angeweza kumpigia simu kwa kuwa namba yake anayo.

“Mhe.Kigwangalla, sio utu kumuombea mtu yoyote apigwe mawe. Suala la uwekezaji Simba nililielezea kwenye interview na Wasafi FM. Wengi wameelewa. Itafute. Kama bado hutaelewa, namba yangu unayo nipigie nitakufafanulia. Pia nisamehe kwamba mkopo wa pikipiki ulioniomba haikuwezekana,” aliandika mfanyabiashara huyo.

Mara baada ya maneno hayo, mjadala huo ulihama na kuanza kujadiliwa swala la Dk. Kigwangalla kunyimwa mkopo wa pikipiki na kuhisi pengine swala hilo ndio lililopelekea kumvaa mwekezaji huyo wa Simba.

error: Content is protected !!