Mkutano Mkuu CCM warekebisha katiba

Spread the love

MKUTANO Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umepitisha marekebisho ya katiba ya chama hicho, ili iendane na Sheria mpya ya vyama vya siasa, pamoja na kuendana na mageuzi ya uongozi. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Azimio hilo limefanyika leo Jumamosi tarehe 11 Julai 2020, jijini Dodoma, baada ya Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM, kuwasilisha ajenda ya marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017, kwa wajumbe wa mkutano huo.

Akizungumza kabla ya marekebisho hayo kupitishwa, Dk. Bashiru amesema Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wametoa mapendekezo kadhaa kwa ajili ya kufanya marekebisho ya vifungu vinavyokinzana na Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 2019.

“Mapendekezo yametoka kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kufuatia kuanza kutumika kwa sheria hii. Msajili wa vyama vya siasa alitaka vyama virekebishe katiba zao kwenye maeneo ambayo ibara za katiba zao zinakinzana na vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa Sura 258 Ya Mwaka 2019,” amesema Dk. Bashiru.

Dk. Bashiru amesema, marekebisho hayo yanalenga kutekeleza agizo la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa vyama hivyo kurekebisha vifungu vya katiba zao, vinavyokinzana na sheria hiyo.

“CCM kwenye katiba yake toleo la 2017 ina ibara kadhaa zinakidhi matakwa ya Sheria ya Vyama vya Siasa, hata hivyo zipo ibara chache zinahitaji kurekebishwa ambazo tunapendekeza hapa,” amesema Dk. Bashiru.

Aidha, Dk. Bashiru amesema ili CCM kiendane na kazi ya mageuzi ya kisiasa na utendaji, NEC imependekeza mambo kadhaa, kwa ajili ya kuingizwa katika katiba ya chama hicho.

Katibu huyo wa CCM amesema, mapendekezo hayo yatawezesha wenyeviti wa mashina kushiriki katika vikao vya kuchagua wagombea wa udiwani na wadi.

“Kwa upande wa masuala yanayohusu uendeshaji wa chama na demokrasia ndani ya chama, NEC inapendekeza maeneo makubwa mawili, eneo la kwanza ni kuwajumuisha wenyeviti wa mashina maarufu kama mabalozi kushiriki mikutano mikuu ya kata na wadi,” amesema Dk. Bashiru na kuongeza:

“Iili kupiga kura ya wagombea udiwani, lengo ni kuwawezesha hawa viongozi wetu wanaoshiriki kututafutia kura waweze kushiriki katika kupiga kura za maoni kwa viongozi ngazi ya vitongoji, mitaa, vijiji, kata na Wadi Zanzibar.”

Baada ya Dk. Bashiru kuwasilisha ajenda hiyo, Dk. John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM aliwauliza wajumbe wa mkutano huo kama wanakubaliana na ajenda hiyo, ambapo walijibu ndio, ishara kwamba wanakubaliana na marekebisho hayo.

MKUTANO Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umepitisha marekebisho ya katiba ya chama hicho, ili iendane na Sheria mpya ya vyama vya siasa, pamoja na kuendana na mageuzi ya uongozi. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea). Azimio hilo limefanyika leo Jumamosi tarehe 11 Julai 2020, jijini Dodoma, baada ya Dk. Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM, kuwasilisha ajenda ya marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017, kwa wajumbe wa mkutano huo. Akizungumza kabla ya marekebisho hayo kupitishwa, Dk. Bashiru amesema Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wametoa mapendekezo kadhaa kwa ajili ya kufanya marekebisho ya vifungu…

Review Overview

User Rating: Be the first one !

About Regina Mkonde

One comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!