Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Mkasa wa kusisimua wa Dk. Lamwai usioujua
Makala & Uchambuzi

Mkasa wa kusisimua wa Dk. Lamwai usioujua

Dk. Masumbuko Roman Lamwai
Spread the love

KIFO cha Dk. Masumbuko Roman Lamwai, kilichokea usiku wa Jumatatu tarehe 4 Mei 2020, kimewatoa machozi Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Anaandika Regina Mkonde, Da es Salaam … (endelea).

Dk. Rugemeleza Nshala, Rais wa TLS kwa niaba ya chama hicho katika salam zake leo tarehe 8 Mei 2020, amesema kifo cha gwiji huo wa sheria nchini kimeacha pengo si kwa TLS, bali kwa taifa.

“Kuondokewa na Wakili Dk. Masumbuko Roman Mahunga Lamwai, kutaleta pengo kubwa siyo tu katika chama chetu bali kwa watu wote waliotegemea sana mchango wake wa kitaaluma.

“Kifo chake kinaongeza huzuni kwa wanachama wetu hasa ukitilia maanani, kuwa bado tulikuwa tunahitaji msaada wake katika taaluma ya uwakili,” amesema na kuongeza “kuna jambo moja ambalo wengi hawalijui kutoka kwa Dk. Lamwai ambalo leo ni vema niliseme.”

“Alinisimulia miaka miwili iliyopita na baadaye mwaka jana, nilimtaka alirudie nikiwa na Wakili na Mwandishi wa Habari Nguli Nyaronyo Mwita Kicheere.

“Ni tukio la baba yake mzazi kuwekwa kizuizini na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro miaka ya kati ya 60. Baba yake alikuwa ni Diwani wa Tanu kutoka Rombo,” ameeleza.

Dk. Nshala ameeleza, baba yake Dk. Lwamwai alitofautiana na Mkuu wa Mkoa ambaye aliamuru awekwe kizuizini. Hali hii ilimfanya Dk. Lamwai akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, kufanya kazi katika mashamba na sehemu mbalimbali kupata fedha ili apate wakili wa kumtetea baba yake.

“Alifanikiwa kupata shilingi 2,000/- na kwenda kwa wakili wa kwanza Mwafrika pale Moshi. Alipoingia na kueleza kuwa anataka kumuajiri wakili, aliulizwa unadhani unaweza kuniajiri mimi una pesa za kulipa, akatoa pesa alizokuwa nazo.

Anasema, wakili huyo alipiga simu polisi kwenda kumkamata Dk. Lamwai ambapo walimchukua na kwenda naye polisi kwani alidhaniwa ameiba.

“Alifanikiwa kujieleza na kuachiwa. Aliporudi bibi yake akamwambia, wapande treni kwenda Dar es Salaam. Bibi yake alikuwa hajui Kiswahili hivyo mkalimani wake akawa ni mjukuu wake Lamwai.

“Walipofika na kuulizia Ikulu, walielekezwa na walipofika getini walinzi wakawauliuza wanashida gani, wakasema wanataka kumuona Rais yaani Mwalimu Nyerere. Wakawakatalia. Kwa kuwa hawakuwa na mwenyeji Dar es Salaam, walibakia nje ya geti,” anaeleza Dk. Nshala.

Anaeleza, Mwalimu Julius Nyerere alipita siku ya kwanza, siku ya pili na hatimaye siku ya tatu. Akauliza kuwa mbona kila siku anawaona pale wana shida gani? Ndipo bibi yake alipoeleza kupitia kwa Mkalimani Lamwai kuwa, amekwenda kudai kuachiwa kwa mwanawe kutokana na kuwekwa kizuizini na Mkuu wa Mkoa.

“Mwalimu Nyerere alimpigia simu hapo hapo Mkuu wa Mkoa, na baada ya kumuuliza kuhusu kuwekwa Ndani kwa Diwani Lamwai, alimuamuru amuachie mara moja. Dk. Lamwai na bibi yake walipewa waranti ya serikali na kurudi Moshi,” amesema Dk. Nshala.

Hata hivyo, Dk. Nshala amesema, alimsihi Dk. Lamwai aandike simulizi hiyo, lakini bahati mbaya amefariki dunia kabla ya kuiandika.

Akieleza moja ya kazi za Dk. Lamwai iliyosisimua taifa, kwamba ni ile aliyomtetea Maalim Seif Shariff Hamad, alipokuwa amewekwa ndani baada ya kuvuliwa uanachama wa CCM Mwaka 1989.

“Mawakili wengi wa nje na ndani walikuja kumtetea Maalim Seif, lakini baada ya hao kushindwa ni Dk, Lamwai aliyefanikiwa kumtetea na kumtoa kizuizini Maalim Seif,” amesema.

Dk. Nshala ameeleza, mbobezi huyo wa sheria nchini alipata uwakili tarehe 14 Disemba 1986, na kupata namba ya uwakili 445 katika orodha ya Mawakili Tanzania Bara.

Amesema, katika kipindi cha miaka 33 alichofanya kazi kama wakili wa kujitegemea na mwanachama hai wa Tanganyika Law Society, amekuwa mwanachama mwaminifu na mfano wa kuigwa.

“Nilimfahamu Mwalimu Lamwai kama ambavyo nilivyozoea kumuita, tokea mwaka 1989 nilipojiunga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Yeye alikuwa akifundisha somo la Civil Procedure (Taratibu za Sheria za Madai) kwa wanafunzi wa Mwaka wa tatu. Kufahamika kwake ni kutokana na ufundishaji wake kwa sauti kubwa na yenye kudai usikivu kwa yoyote anayeisikia,” amesema Dk. Nshala.

Amesema, Dk. Lamwai alipokuwa akifundisha UDSM, alikuwa akivaa kawaida sana na ilibidi mtu akuambie kuwa yule ni mwalimu wa hapo chuoni, kwani ungedhani ni mgeni kaja tu kutembea pale chuoni.

Amesema, Dk. Lamwai amefundisha sehemu kubwa ya wanasheria hapa nchini na hata majaji na mahakimu na kwamba, licha ya kuwa mwalimu wao, alikuwa mnyenyekevu kukubali kuendesha kesi mbele ya wanafunzi wake na hata kuambiwa ameshindwa nao.

“Alijua maana halisi ya taaluma hii kuwa hakimu au jaji ndiye muamuzi na kuwa uamuzi anaoutoa lazima uheshimiwe na wote,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!