Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Miradi mikubwa: Serikali ya JPM yatamba bungeni
Habari za Siasa

Miradi mikubwa: Serikali ya JPM yatamba bungeni

Rais John Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kiwango cha rami katika mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma
Spread the love

SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imejigamba kutekeleza miradi mikubwa tangu iliopanza kuwatumikia wananchi mwaka 2015. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, serikali hiyo imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya kiuchumi (Ujenzi, Uchukuzi na nishati) na ugharamiaji wa huduma za jamii (Afya Elimu, Maji).

Akieleza mafanikio ya serikali hiyo leo tarehe 11 Juni 2020, wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 bungeni jijini Dodoma, Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Uchumi amesema, serikali hiyo imefanya ‘makubwa’ ikiwa ni pamoja na kulipa madeni makubwa.

Amesema, serikali imelipa madai mbalimbali yenye jumla ya Sh. 3.2 trilioni pamoja na madeni ya kimshahara ya watumishi wa umma Sh. 114.5 bilioni.

Katika huduma za kijamii, Dk. Mpango amesema, serikali imefanikiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, kwa kujenga zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za Halmashauri za Wilaya 71, hospitali za rufaa za Mikoa 10 na hospitali za rufaa za kanda tatu.

“Kuongezeka kwa bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi bilioni 269 mwaka 2019; na kuimarika kwa upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kufikia asilimia 94.4 mwaka 2019/20 kutoka asilimia 36 mwaka 2014/15,” amesema Dk. Mpango.

Dk. Mpango amesema Serikali ya Rais Magufuli imefanikiwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji safi na salama maeneo ya vijijini kutoka asilimia 70.1 hadi asilimia 84.

Dk. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na MIpango Tanzania

“Serikali imejenga na kukarabati miundombinu ya maji 1,423 ambapo miradi 1,268 ni ya vijijini na 155 ni ya mijini. Utekelezaji wa miradi ya maji 19 imegharimu jumla ya shilingi trilioni 1.55 kati ya mwaka 2015/16 hadi Aprili 2020,” ameeleza Dk. Mpango.

Katika sekta ya elimu, Dk. Mpango amesema, serikali imefanikiwa kugharamia elimu ya msingi bila ada ambapo jumla ya Sh. trilioni 1.03 zilitumika kati ya mwaka 2015/16 hadi 2019/20, kugharamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo madarasa, maabara, maktaba na mabweni.

“Serikali imefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa kutoa ruzuku kwa vyuo vya elimu ya juu na mikopo kwa wanafunzi. Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu iliongezeka kutoka shilingi bilioni 348.7 mwaka 2014/15 hadi shilingi bilioni 450 mwaka 2019/20. Jumla ya shilingi trilioni 2.20 zimetumika kugharamia mikopo katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020,” amesema Dk. Mpango.

Kuhusu sekta ya miundombinu ya ujenzi, uchukuzi na nishati, Dk. Mpango amesema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi Aprili 2020, serikali imejenga barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa km 2,624.27.

Amesema, serikali imefanikiwa kujenga madaraja matatu (daraja la juu la Mfugale (Dar es Salaam), daraja la Furahisha (Mwanza) na daraja la Magufuli (Mto Kilombero) ambayo ujenzi wake umekamilika.

Dk. Mpango amesema, miradi ya ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko imegharimu jumla ya shilingi trilioni 7.63 kati ya mwaka 2015/16 hadi Aprili 2020. Ambapo kati ya kiasi hicho, ujenzi wa barabara umegharimu shilingi trilioni 6.4 fedha za ndani na shilingi trilioni 1.02 fedha za nje, ujenzi wa madaraja shilingi bilioni 205.0 na ujenzi wa vivuko shilingi bilioni 20.1.

Kwenye uchukuzi, Dk. Mpango amesema, serikali imeanza ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro (km 300), na kipande cha Morogoro hadi Makutupora (km 422) ambapo jumla ya shilingi bilioni 170 na Dola za Marekani bilioni 1.5 zimetumika hadi sasa.

Amesema, utekelezaji wa mradi huu umewezesha kupatikana 24 kwa ajira 13,177 kwa wananchi na ushiriki wa wakandarasi wa ndani 640.

Waziri huyo wa Fedha amesema, utekelezwazi wa miradi hiyo, imesababisha pato la taifa kukua kutoka wastani wa asilimia 6.2 hadi 6.9 asilimia.

Pamoja na mapato ya ndani yameongezeka hadi kufikia Sh. 18.5 trilioni mwaka 2018/2019, kutoka Sh. 11.0 trilioni 2014/2015, ambalo ni sawa na asilimia 69.1.

“Wastani wa mapato ya kodi kwa mwezi umeongezeka kutoka shilingi bilioni 825 mwaka 2014/15 hadi wastani wa shilingi trilioni 1.3 mwaka 2018/19 na kuongezeka zaidi hadi wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020,” amesema Dk. Mpango na kuongeza:

“ Aidha, mapato ya kodi yameongezeka kutoka shilingi trilioni 9.9 mwaka 2014/15 hadi shilingi trilioni 15.5 mwaka 2018/19, sawa na ongezeko la asilimia 56.5.).”

Dk. Mpango amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezwaji  Sera za Mapato na Matumizi za Serikali ya Awamu ya Tano, za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia matumizi ya fedha za umma.

Dk. Mpango amesema Serikali ya Rais Magufuli imefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei ambapo umeen delea kubaki katika wigo wa tarakimu moja.

“Mfumuko wa bei uliendelea kuwa tulivu na kubakia katika wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia 4.4 kwa kipindi chote cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ambapo mwaka 2019, mfumuko wa bei ulifikia asilimia 3.4.

“Kiwango hiki ni cha chini kabisa kuwahi kutokea kwa kipindi cha nusu karne tangu mwaka 1970 tulipokuwa na mfumuko wa bei wa asilimia 2.4,” amesema Dk. Mpango.

Vile vile amesema, mapato yasiyo ya kodi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 688.7 mwaka 2014/15 hadi shilingi trilioni 2.4 mwaka 2018/19 na shilingi trilioni 2.25 katika kipindi cha miezi 10 ya kwanza ya mwaka 2019/20.

Dk. Mpango amesema, mafanikio hayo yametokana na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuimarika kwa bei za mafuta pamoja na upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani na nchi jirani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Chadema yamtaka Rais Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

error: Content is protected !!