Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Miradi inayofadhiliwa na China, yayumba Pakistan 
Habari za Siasa

Miradi inayofadhiliwa na China, yayumba Pakistan 

Rais wa China Xi Jinping
Spread the love

VURUGU za kisiasa, kukua kwa deni la nje na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19, vimesababisha kupunguza uwekezaji wa China nchini Pakistan, ambapo Beijing imezuia jumla ya Dola za Marekani bilioni 62 miongonimwao ikiwa ni Dola za Marekani bilioni 6.8 za mpango wa ukarabati wa reli. Anaandika Mwandishi Wetu…(endelea).

Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan kwa sasa analalamikiwa kwa kuendesha kijeshi serikali yake na ufujaji wa fursa za kiuchumi, matumizi makubwa ya fedha yasiyojali vipaumbele kwa kuharakisha uwekezaji mkubwa wa miundombinu inayofadhiliwa na China.

Mara baada ya Waziri Mkuu Khan kuingia madarakani mwaka 2018, alisitisha miradi kadhaa iliyokuwa ikiratibiwa chini ya mradi wa Uchumi wa Kikanda kati ya China na Pakistan kutokana na hofu ya ubadhirifu uliokuwa ukifanyika katika serikali iliyokuwepo na kutaka kuanza upya majadiliano.

…pia kurekebisha kasoro za mpango wa mradi huo ambao unadhamiria kuiunganisha China na Pakistan kupitia Bahari ya Hindi.

Miaka miwili baadaye, wajumbe wa Baraza la Mawaziri wanatajwa katika tuhuma za ubadhirifu zinazohusisha sekta ya umeme nchini Pakistan.

Theluthi moja ya kampuni za umeme zinahusika katika miradi ya Wachina chini ya mwamvuli wa mradi wa Uchumi wa Kikanda kati ya nchi hiyo na China.

Katika ripoti yenye kurasa 278, iliyotolewa na Tume ya Usalama ya Pakistani na kuwasilishwa kwa Khan, ilibaini kuwapo kwa ukiukwaji wa madai yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.8 katika ruzuku iliyotolewa kwa kampuni binafsi 16 za uzalishaji umeme zikiwamo kampuni zinazomilikiwa na washauri wa Waziri Mkuu Khani.

Kampuni hizo binafsi za uzalishaji umeme, ziliwekeza kiasi cha Rupia 60 bilioni sawa na dola 37.5 bilioni za Marekani ili kujenga mitambo ya kuzalisha umeme ambapo zilijipatia zaidi ya Rupia 400 bilioni sawa na dola 2.5bilioni za Marekani ndani ya kipindi cha miaka miwili hadi minne.

Pia ripoti hiyo ilibainisha namna kampuni za kufua umeme za Kichina zilivyotengeneza faida kwa muda mfupi.

Tume ya Usalama ya Pakistan ilibainisha kuwa, Kampuni ya Huang Shandong Ruyi Pakistan Ltd (HSR) na Port Qasim Electric Power Co Ltd (PQEPCL) kwa pamoja, zililipwa zaidi ya Rupia 483.6bilioni sawa na dola 3 bilioni za Marekani ikiwa ni pamoja na ongezeko la gharama zisizo sahihi za viwango vya malipo ya ndani vilivyoruhusiwa na Mamlaka ya Taifa ya Udhibiti wa Umeme na Wakala wa Ununuzi wa Umeme.

Kuanzia Oktoba mwaka 2020, Chama cha Demokrasia cha Pakistan ambacho ni muunganiko wa vyama vya siasa 11 vya upinzani, kiliwaongoza raia katika kampeni dhidi ya serikali huku kikitaka kuharakishwa kwa miradi inayofadhiliwa na China, hususan barabara na mpango wa reli ya kisasa ambayo imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu.

Aidha, Chama Cha Demokrasia cha Pakistan kinataka kuondolewa kwa mamlaka ya Mwenyekiti wa mradi wa Ukanda wa Kiuchumi kati ya China na Pakistan, Luteni Jenerali Mstaafu Asim Saleem Bajwa hadi hapo atokapoweka hadharani thamani ya mali anazomiliki na zile zinazomilikiwa na familiya yake zilizopo Marekani.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Asia Time, Bajwa anamiliki zaidi ya kampuni 100 katika nchi mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Kanada ambapo mke na watoto wake wanahusishwa pia.

Kabla ya kutembelea nchini China Oktoba 2019, Waziri Mkuu Khan alitoa agizo la kuanzishwa Mamlaka ya Mradi wa Ukanda wa Kiuchumi kati ya China na Pakistan na kumteua Luteni Jenerali mstaafu, Bajwa kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo kutoka Wizara ya Mipango na Maendeleo iliyokuwa ikisimamia mradi huo.

Mamlaka hiyo imehalalishwa kisheria baada ya sheria inayoipa nguvu kukamilika mwezi Juni 2020 ambapo Mradi wa Ukanda wa Kiuchumi kati ya China na Pakistan ulikuwa ukiendelea bila ya kuwepo uhalali wa kisheria.

Vyanzo vya habari vya Wizara ya Mipango viliiambia Asia Times kuwa, mradi huo ulilazimishwa na serikali ya China ambayo ilitaka jeshi la Pakistan kuhusika moja kwa moja katika utekelezaji wa mradi huo baada ya China kukasirishwa na kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo.

Kutokana na taarifa ya hivi karibuni zilizochapishwa na Asia Time za kushikiliwa kwa mali za Bajwa, zimezishitua mamlaka za China zilizohitaji kufanya kazi na jeshi ili kuepuka ufisadi.

Madai hayo yamepelekea kuahirishwa kwa ziara ya Rais wa China Xi Jinping kuitembelea Pakistan Septemba 2020, hata hivyo mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ulitajwa kuwa sababu rasmi ya kuahirishwa  kwa ziara hiyo.

Kwa mshangao, sheria inayoipa nguvu Mamlaka ya mradi huo, inatoa kinga kwa mwenyekiti na wafanyakazi juu ya kesi zote za kisheria zinazowakabili kwa kuwa sheria inawalinda dhidi ya hatua zozote zinazoweza kuchukuliwa na Ofisi ya Uwajibikaji ya Taifa na Shirikisho la Wakala wa Upelelezi pamoja na Polisi.

Kiongozi wa Jumuiya ya Waislamu ya Pakistan Senata Mushahid Hussain Sayed na Mwenyekiti wa Jopo la Wanazuoni waliiambia Asia Times kuwa Chama cha Demokrasia cha Pakistan kina wasiwasi sana pamoja na mambo mengine juu ya kifungu cha sheria kinachowapa kinga Mwenyekiti na viongozi wengine wa Mamlaka inayosimamia mradi huo.

“Suala la uhalali wa mradi wa Ukanda wa Kiuchumi kati ya China na Pakistan, kinga ya Mwenyekiti dhidi ya kesi za kisheria na utata unaotokana na biashara zote za kifamilia zinazosimamiwa na mke wa Mwenyekiti huyo nje ya nchi vinatoa taaswira mbaya na hivyo lazima zitatuliwe ili kuongeza ufanisi wa mradi huo,” anasema Mushahid wakati akitoa maoni juu ya wasiwasi wa Chama cha Demokrasia cha Pakistan

Senata Mushahid ambaye alihusisha ucheleweshaji wa mradi huo na mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19, hata hivyo alibainisha kuwa angalau miradi mitatu mipya, miradi miwili katika sekta ya umeme na mmoja kwenye ukarabati wa reli ilianzishwa tena wakati huu wa msimu wa joto.

“Kwa kuongezea, Balozi mpya wa China Nong Rong amekuja na msingi imara wa uchumi ambao unatizamiwa kutoa msukumo katika utekelezwaji wa mradi huu wa Ukanda wa Kiuchumi kati ya China na Pakistan,” Mushahid aliongeza.

Alisema, maandamano ya Chama cha Demokrasia cha Pakitan hayatadhoofisha maendeleo ya mradi huo muhimu kwa uchumi wa mbili washirika.

“Kuongezeka kwa shinikizo kutoka katika nchi na jumuiya za kimagharibi hasa Marekani dhidi ya mradi huo, kumeifanya Pakistan ioneshe dhamira ya dhati, utayari na uwezo wa kuhimili shinikizo hilo,” aliongeza Mushahid.

Alisisitiza, maendeleo mapana ya uchumi wa Pakistan kutokana na mradi wa Ukanda wa Kiuchumi ni muhimu na kwamba, kuchelewesha shughuli za maendeleo za mradi huo si chaguo sahihi.

Mradi mkuu (ML-1) ambao ndiyo mkubwa zaidi kwenye ujenzi wa miundombinu inayoendelea ambao unakusudiwa kuunganisha Mji wa Karachi, Kusini na Peshawar Kaskazini kupitia reli yenye urefu wa kilomita 2,655 kwa gharama ya dola za Kimarekani 6.8bilioni.

Mradi huo unakusudia kurekebisha miundombinu ya reli ya enzi za Wakoloni na kutoa ajira nyingi mpya zipatazo 150,000 na kuongeza mapato ya ziada ya usafirishaji bada ya kukamilika.

China inafahamu vyema kuwa mapambano kati ya vikosi vya taifa vya ukombozi na vikosi vilivyojitenga katika majimbo ya Baloch na Sindh vimezorotesha shughuli za maendeleo ya mradi huo ambapo hivi karibuni imeshuhudia wafanyakazi na wahandisi wa Kichina wakilengwa katika mashambulizi ya vikosi vya waasi wa Pakistan.

Waasi hao wanadai kuwa, jeshi la Pakistan linashirikiana na China kupora mali asili za miji ya Baloch na Sindh huku gharama ya kusimamia usalama wa wafanyakazi raia wa China kukiongeza zaidi gharama ya mradi wakati huu ambao uchumi wa Pakistan ukizidi knayumba.

Kutokana na hali hiyo, taarifa zinadai, Pakistani imeomba asilimia moja ya kiwango cha riba cha mkopo wa China kwa mradi wa reli (ML-1).

Hata hivyo, mamlaka husika ya China imesita kutoa mkopo kwa kiwango hicho cha chini na wamekuwa wakitumia mbinu ya kuchelewesha ili kuishinikiza Pakistan kukubali masharti magumu ya China.

Taarifa zinadai, Khan na Bajwa wanakusudia kupeleka ombi hilo kwa Rais Xi Jinping ambaye wanaamini ataweza kuafikiana nao juu ya masharti ya mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya China na Benki ya Export-Import ya China kwa matarajio kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa kwenye mradi wa reli.

Taaarifa zinaonesha kuwa mradi wa ML-1 unaweza usikamilike kwa wakati ingawa Waziri wa Reli wa Pakistan Sheikh Rasheed Ahmad mara kwa mara amekuwa akitangaza kuwa mradi wa reli ML-1 uko mbiyoni kuanza.

Vivyo hivyo, mradi mkubwa wa usafirishaji wa Peshawar, Swat Express Way awamu ya II na Peshawar – D1, Khan Motorway, nayo pia imechelewa kukamilika na haipo katika ajenda za mkutano unaofuata wa Kamati ya pamoja ya kuratibu mradi huo kati ya China na Pakistan.

Profesa msaidizi katika Kituo cha Mafunzo ya Kimataifa cha Jan Masaryk, Chuo Kikuu cha Uchumi na Biashara cha Prague, Jeremy Garlick alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari vya Pakistan akisema kuwa China inatumia mbinu ya kuchelewesha mradi wa ML-1 kwani haitaki kuishia na hasara mikononi mwake.

“Beijing haitaki kusema hapana kwenye mradi wa ML-1. Inataka kuonekana kuwa mshirika wa Pakistan lakini wakati huohuo inafahamu kuwepo kwa mazingira hatarishi kwa uwekezaji wa Wachina nchini Pakistan,” aliongeza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!