Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mgogoro CUF umekwisha kweli?
Habari za SiasaTangulizi

Mgogoro CUF umekwisha kweli?

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeingia katika mgogoro zaidi. Hatua ya chama hicho kupitia kundi la viongozi wanaomtii Profesa Ibrahim Lipumba, kutangaza mabadiliko ya Bodi ya Wadhamini wa chama, iliyokuja siku nne tu baada ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali kuidhinisha, haitaridhiwa na wanaotii Katiba ya chama hicho, anaandika Jabir Idrissa.

Kundi linalowapinga, likiongozwa na kamati ya uongozi inayoongozwa na Julius Mtatiro, na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, wanatarajiwa kutoa tamko rasmi leo kuhusu hatua hiyo.

“Kutwa leo tumekuwa kwenye kesi Mahakama Kuu. Viongozi wote wapo huko. Na suala hilo ni sehemu ya kilichowashindisha viongozi wenzetu mahakamani Dar es Salaam. Sasa si vizuri kutoa tamko mpaka kikao cha mashauriano kitakachoitishwa.

Nakuahidi tamko letu litatoka kesho,” alisema Salim Bimani, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma wa CUF.

Leo kwenye ofisi kuu za CUF za Buguruni, jijini Dar es Salaam, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma, Abdul Kambaya aliitisha mkutano na waandishi wa habari na akasikika Thomas Malima akitangaza kuwa tayari chama kimepata bodi mpya ambayo yeye ndiye katibu wake.

Malima ambaye alikuwa naibu mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa chama kabla ya mgogoro uliobuka Agosti mwaka jana, kufuatia Prof. Lipumba kulazimisha kurudi kushika uenyekiti baada ya kujiuzulu kwa hiari yake Agosti 5, 2015, amesema “mgogoro sasa umekwisha.”

Akinukuu aliyoita barua ya Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali, Malima amedai kuwa bodi mpya imeidhinishwa na Kabidhi Wasii Mkuu na kwamba Peter Michael Malebo ndiye mwenyekiti.

Wajumbe wengine aliowataja ni Hajira Siria, Aziz Iss Nagesha, Abdul Magomba, Amina Msham, Asha Said, Mussa Haji Kombo, Saria Hilal Mohamed na Suleiman Makame.

Kwa mujibu wa Malima, akisoma aliyosema ni barua ya Msajili an Mfilisi wa Serikali ya kujibu barua ya awali iliyotumwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Chama, Magdalena Sakaya, nyaraka zilizowasilishwa nao ni sahihi na zimewekwa kwenye kumbukumbu kwa Msajili na Mfilisi.

Imeelezwa kuwa msingi wa Msajili na Mfilisi kuidhinisha Bodi mpya ya CUF, umetokana na usahihi wa nyaraka hizo na kwamba zimetokana na vikao halali kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Vyama vya Siasa nchini na Katiba ya CUF. Nyaraka hizo pamoja na ombi lenyewe la Sakaya, Malima amesema ziliwasilishwa na kampuni ya uwakili ya Man’s Attorney.

Kutokana na hatua hiyo, Malima amesema Bodi mpya ilikaa Juni 17, 2017 na kuamua mambo mawili: Kwanza, ni kufutwa kesi zote zilizofunguliwa wakati wa mgogoro. Na pili, Katibu wa Bodi, ambaye ni yeye, ameagizwa kuziandikia benki zote ambako chama kinaendesha akaunti, kuruhusu miamala ifanyike kuanzia sasa.

Maana yake ni kwamba Bodi iliyokuwa ikiongozwa na Abdallah Said Khatau (Mwenyekiti) na Joram Bashange (Katibu), imefutwa kazi. Bodi hiyo ambayo Septemba mwaka jana ilitangaza kutomtambua Prof. Lipumba, kwa kuwa alijiuzulu na baadaye chama kuridhia kwa kura, nayo ilikuwa na wajumbe tisa – watano kutoka Bara na wanne kutoka Zanzibar.

Malima amesema hatua ya kufuta kesi ilianza leo kwenye Mahakama Kuu ambako moja ya kesi kadhaa zilizofunguliwa ilikuwa imeitwa kwa kusikilizwa. Malima amesema mawakili wapya walioteuliwa kusimamia chama, wanashughulikia suala hilo.

Amewataja kuwa ni Mashaka Ngole na Makubi Kunju Makubi. Kwa mujibu wa taarifa yake, wanawabadilisha Mziray na Juma Nassoro ambao ndio wamekuwa wakisimamia kesi zilizofunguliwa na upande wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad.

Malima pia amesema sasa wale wote waliokuwa wakifanya shughuli za chama kwa mwamvuli wa kamati ya uongozi wasimame kufanya hivyo. Amesema Katiba ya CUF haitambui kamati ya uongozi.

Kamati ya Mtatiro, inayofanya kazi za mwenyekiti na makamu mwenyekiti, iliteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi Taifa lililoketi baada ya kuvurugika kwa mkutano mkuu maalum uliofanyika Agosti 21 2016, kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Ibara ya 98(2) ya CUF, Bodi ya Wadhamini ina majukumu makuu mawili: Kwanza kusimamia mali na madeni ya chama. Kusimamia fedha za chama. Kupitia bodi hiyo, chama hicho kinashitakika kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Kambaya alisema sasa CUF ni moja – yenye Bodi ya Wadhamini moja, Baraza Kuu moja na Kamati ya Utendaji moja. Naye Khalifa Suleiman Khalifa, mbunge mstaafu wa Gando, Kaskazini Pemba, ametoa wito kwa wanachama wote kurudi kwenye chama.

“Ninafuraha kubwa sana leo. Kwamba tumefika mwisho wa mgogoro. Sasa sote turudi kujenga umoja, utulivu na mshikamano kwa manufaa ya chama chetu,” alisema.

Baada ya mkutano huo, viongozi hao walitarajiwa kuhutubia wanachama waliokuwa kwenye uwanja wa chama hicho Buguruni.

Kitendo cha Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali kuidhinisha Bodi iliyopendekezwa na uongozi wa Prof. Lipumba kilitabiriwa na Maalim Seif. Alitoa indhari akisema ni mbinu ya mwisho ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumwezesha Prof. kushika hatamu za chama na hatimaye kumsimamisha yeye kuwa kiongozi.

Aprili 9, mwaka huu, kwenye Hoteli ya Lamada, Dar es Salaam, Maalim Seif akizungumzia alichoita “Njama za kuitumia RITA kuhitimisha mpango wao” alisema:

• Baada ya kuona hawajafanikiwa na CUF imesimama imara kujilinda kupitia hatua za kisheria, sasa Dola imeamua kukamilisha mpango wake mchafu kwa kutumia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

• Tokea kuanza kwa njama ovu na mbinu chafu hizi, moja ya vinavyoonekana vikwazo vikubwa vinavyokwamisha kufanikiwa malengo yake imekuwa ni Bodi ya Wadhamini ya The Civic United Front (CUF)ambayo imechukua hatua madhubuti za kukilinda Chama kupitia Mahakama na taratibu nyingine za kiutawala na kisheria. Sasa njama mpya zinazofanywa ni kukiondosha hiki kinachoonekana kuwa ni kikwazo kwao.

• Tunazo taarifa zisizo na shaka kuwa, kuna shindikizo kubwa la kumtaka Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA kusajili wajumbe feki wa Bodi ya Wadhamini ya CUF kwa kutumia majina yaliyowasilishwa na kibaraka Ibrahim Haruna Lipumba ili kuhujumu majina halali yaliyowasilishwa na kikao halali cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kilichofanyika makao makuu ya Chama, mjini Zanzibar tarehe 19 Machi, 2017.

• Nitoe maelezo mafupi kuhusiana na hili ili lieleweke vizuri. Kimsingi, Bodi ya Wadhamini ya CUF ilikwisha sajiliwa tokea 1993, kwa kufuata taratibu zote zilizoelekezwa na Sheria ya Wadhamini (The Trustees’ Incorporation Act – Cap 318) na Hati ya Usajili tunayo.

Kinachofanyika kila baada ya kipindi fulani ni kuweka sawa kumbukumbu za bodi hiyo kwa kuwalipia wadhamini na kuingiza kwenye kumbukumbu mabadiliko ya wajumbe kadiri yanavyofanyika kwa mujibu wa Katiba ya CUF.

• CUF, kupitia Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lililochaguliwa kihalali katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa mwaka 2014, na kwa kufuata masharti ya Ibara ya 98 ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 (Toleo la 2014) imefanya mabadiliko machache ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na kuyawasilisha RITA, ambapo yalipokelewa na kupatiwa stakbadhi ya malipo yake.

• Hata hivyo, mara baada ya kuwasilisha mabadiliko hayo machache, Lipumba na yeye akatakiwa haraka aandae majina yake na kuyafikisha RITA huku akihakikishiwa kwamba RITA itapewa maelekezo ya nini cha kufanya.

Lengo la njama hizi ni kumuwezesha kibaraka Lipumba kuwa na ‘Bodi ya Wadhamini’ ambayo itatumika, kwanza, kufuta kesi zote zinazomkabili yeye na genge lake na Msajili wa Vyama Vya Siasa ambaye yuko katikati kwenye hujuma hizi zote.

• Lengo la pili ni kufungua akaunti mpya ya benki na kuwezesha kupatikana kwa fedha za ruzuku za Chama na mwisho Bodi hiyo mpya kudhibiti Ofisi za Makao Makuu ya Chama zilizopo Mtendeni, Zanzibar na kumuondoa Katibu Mkuu wa Chama.

• Kufikia hatua hiyo watawala wanadhani watakuwa wamejiridhisha kuwa wameweza kuidhibiti CUF na khofu yao kwa CUF itakuwa imeondoka. Wanavyojidanganya ni kwamba madai ya Wazanzibari juu ya haki yao ya ushindi ulioporwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 yatakuwa yameishia hapo na hatua zote zilizofanyika zitakuwa zimekwamishwa. Na mwisho, wanajiaminisha kwamba kufikia hapo Watanzania walioiamini CUF kama taasisi imara ya kuwaletea mabadiliko ya kweli watasambaratika.

• Tunajua kwamba Msajili amekuwa akiwasiliana na RITA kutia shinikizo wajumbe feki ndiyo wasajiliwe. Ni wazi Msajili ana maslahi ya ziada katika hili kwa sababu anahitaji RITA isajili wajumbe feki wa Bodi watakaokwenda kumfutia kesi zinazomkabili zilizofunguliwa na Bodi halali ya Wadhamini wa Chama. Tunayasubiri maamuzi ya RITA tuone kama na wao watageuka kama Msajili wa Vyama vya Siasa na kukubali kutumika katika kusajili wajumbe feki wa Bodi ya Wadhamini.

Maalim Seif alihitimisha hotuba yake kwa kusema: CUF ni taasisi imara na imepita katika misukosuko mingi tokea kuasisiwa kwake. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, tumevuka salama kote huko tulikotoka. Nawaambia watawala walio nyuma ya hujuma hizi kwamba kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na msukosuko huu wa kumtumia kibaraka nao tutauvuka salama na tutaushinda.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!