ALEX Kimbe, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo tarehe 28 Machi 2020, ameondolewa madarakani na Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Iringa … (endelea).
Hatua hiyo imechukuliwa katika kikao maalumu cha baraza la madiwani kilichoketi leo, kwa ajili ya kujadili tuhuma zilizokuwa zinamkabili Meya Kimbe, ikiwemo za matumizi mabaya ya madaraka na mamlaka.
Meya Kimbe ameondolewa madarakani kwa kura za ndio 14 kati ya 26, zilizopigwa na wajumbe katika kikao hicho.
Kwa mujibu wa Hamid Njovu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Meya Kimbe ameondolewa madarakani, baada ya Tume ya Uchunguzi dhidi yake iliyoundwa na Ally Hapi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, kumkuta na hatia.
Njovu amedai kuwa, Meya Kimbe aliamuru baadhi ya wajumbe wa halmashauri hiyo, kufanya ziara mkoani Mbeya na Njombe, pasipo kupata kibali cha Mkuu wa Mkoa.
“Amekuwa akitumia nafasi yake vibaya ya madaraka na mamlaka, matokeo ya uchunguzi ni kama ifuatavyo, kuamuru wajumbe wa halamshauri kufanya ziara pasipo kupata kibali cha mkuu wa mkoa,” amedai Njovu.
Leave a comment