Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Meya wa CCM ang’olewa Dodoma
Habari za SiasaTangulizi

Meya wa CCM ang’olewa Dodoma

Antony Mavunde, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini
Spread the love

MADIWANI wa Manispaa ya Dodoma wamemng’oa Meya wa Manispaa hiyo, Jafary Mwanyemba (CCM) kwenye wadhifa wake baada ya kusaini mkataba wa kuchimba visima vya maji katika kata ya Zuzu kinyume na sheria, anaandika Dany Tibason.

Maazimio hayo yamefikiwa leo na kikao maalum cha baraza la madiwani kilichokutana kwa ajili ya kupokea taarifa ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo zikiwemo za upotevu wa Sh. 31 milioni ambazo hazijulikani zilipokwenda.

Hata hivyo katika taarifa ya tume ya uchunguzi iliyokuwa ikiongozwa na Ofisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Dodoma, Cosmas Kanyika ilibainika kuwa fedha hizo zililipwa kwa mkandarasi wa mradi huo, Kallago Interprises kwa ajili ya kuchimba visima vya maji ambapo hata hivyo baada ya kushindwa kuifanya kazi hiyo alishindwa kuirudisha fedha hiyo.

Aidha mkandarasi huyo alitumia kiasi cha Sh. 18 milioni kwa ajili ya kuchimba visima viwili katika Kata ya Zuzu lakini hata hivyo visima hivyo havikuweza kutoa maji mpaka sasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya tume ya uchunguzi iliyoundwa baada ya ubalozi wa Japan nchini kutembelea mradi huo na kuona matunda yaliyokusudiwa hayajapatikana walitaka fedha zilizotolewa kwa mkandarasi zirejeshwe ambapo Mstahiki Meya Mwanyemba alilazimika kurejesha fedha hizo kiasi cha Sh. 30 milioni baada ya kuombwa kufanya hivyo na Mkurugenzi wa manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde ili kunusuru mradi huo usiondolewe kwa wananchi wa kata ya Zuzu.

Hata hivyo tume hiyo haikuonyesha mahali popote ambapo Mstahiki Meya Mwanyemba alihusika na utengenezwaji wa mkataba huo licha ya kuusaini tu na kusema kuwa tuhuma zote hazikuwa za kweli dhidi yake baada ya kuwahoji madiwani wanaompinga, madiwani wanaomuunga mkono na watumishi wa Manispaa ya Dodoma.

Lakini hata hivyo baada ya taarifa ya tume ya uchunguzi iliyoundwa kusomwa madiwani walitaka kura za siri zipigwe na ndipo wengi wao waliposema kuwa hawana Imani na Mstahiki Meya huyo.
Sakata la kutokuwa na Imani na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma liliibuliwa na baadhi ya madiwani wa Manispaa hiyo baada ya Meya huyo kusaini mkataba wa kuchimba visima virefu vya maji katika Kata ya Zuzu uliokuwa na thamani ya Sh. 122 milion kinyume na taratibu.

Mradi huo ulikuwa unafadhiriwa na ubalozi wa Japan nchini ulikuwa na lengo la kuchimba visima virefu viwili kwa ajili ya kupunguza upungufu wa maji kwa wakazi wa kata hiyo.

Hata hivyo kabla ya mkataba kati ya Manispaa na Mkandarasi aliyepewa kazi ya kuchimba visima hivyo Kalago Interprises haujarudi kutoka kwa mwanasheria mkuu wa serikali Mstahiki Meya alisaini mkataba mwingine uliotengenezwa na Mwansheria wa Manispaa ya Dodoma, Salma Kambona ulioidhinisha kuwa mkandarasi huyo alipwe asilimia 25 ya malipo ya kazi hiyo.

Ilibainika kwamba mwezi mmoja baadaye mkataba uliokuwa kwa mwanasheria mkuu wa serikali ulikuja na kusema kuwa mkandarasi huyo alipwe asilimia 15 tu ya malipo ya awali kwa ajili ya kazi hiyo.

Katika taarifa ya tume ya uchunguzi iliyotolewa mwanasheria wa Manispaa alipohojiwa amesema kuwa alilazimika kuandaa mkataba mwingine kutokana na uharaka uliokuwepo wa kusaini mkataba huo kwa kuwa ubalozi wa Japan ulikuwa umetoa muda wa siku saba tu wa kusaini mkataba huo na ule uliotumwa kwa mwanasheria mkuu wa serikali ulikuwa unachelewa.

Akihoji uharaka wa kusainiwa kwa mkataba huo, diwani wa kata ya Chahwa, Sospeter Mazengo amesema kulikuwa na ulazima gani wa kuwahi kusainiwa kwa mkataba huo na ilhali wakazi wa Kata ya Zuzu hawana maji mpaka sasa na kuisababishia serikali upotevu wa fedha?

Amesema Mstahiki Meya angetumia busara ya kusubiri mkataba kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali hadi uje ili ausaini kuliko ule uliotengenezwa na watumishi wa Manispaa ya Dodoma ambao umemletea shida na kuonyesha kuwa hana uelewa wa kutosha kuhusiana na uendeshaji wa taratibu wa shughuli za kiserikali.

Wajumbe waliotakiwa kupiga kura walikuwa 56 ambapo kati ya hao nane hawakupiga kura na hivyo kura halali zilizopigwa zilikuwa 48 ambapo 43 walisema hawana Imani na Meya na wanne wakisema kuwa wanaimani na meya huyo huku kura moja ikiharibika.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!