Bernard Membe, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Tanzania

Membe: Mwaka huu nitagombea urais

Spread the love

BERNARD Membe, aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, atagombea urais. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 23 Juni 2020, wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (D.W), kuhusu msimamo wake wa kugombea nafasi hiyo.

Membe ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nnne amesema, dhamira ya kugombea ipo pale pale lakini hadi sasa hajafahamu atagombea kupitia chama kipi, baada ya CCM kumfukuza uanachama kutokana na utovu wa nidhamu.

“Ni kweli kabisa mwaka huu 2020 nataka kugombea, kwa chama gani sijui, kwa sababu moja CCM kama ikinisafisha, naweza kugombea kupitia CCM, ni haki yangu, ni furaha yangu na furaha ya watu wengine kuona watu wakishindana,” amesema Membe.

Mwanadiplomasia huyo amesema, hata alipohojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM kuhusu nia yake hiyo, aliwajibu wajumbe wa kamati hiyo kwamba, yuko tayari kugombea.

“Tarehe 6 Februari 2020 Dodoma nikiwa kwenye kamati ya maadili waliniuliza swali hilo, unataka kugombea urais, nikawaambia kwa mazingira yaliyoko Tanzania, ndio niko tayari kugombea,” amesema Membe.

Bernard Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,

Hata hivyo, Membe amedai kuwa, kuna wanachama sita wa CCM wana nia ya kugombea urais wa Tanzania, lakini hawataki kujitangaza wakihofia kufukuzwa uanachama.

“Siwezi kuwasema wenzangu  (wanaotaka kugombea urais CCM) sababu watafukuzwa chama, nakuapia leo kama tusingekuwa tunafukuzana, ningekupa majina yote sita mimi ni wa saba, lakini watafukuzwa kesho asubuhi,” amesema  Membe.

Licha ya kwamba hajaweka wazi kama atahamia katika vyama vya siasa vya upinzani ili kupata nafasi ya kugombea urais wa Tanzania, Membe amesema kama mtu hataipata haki yake katika chama chake, anawajibu wa kuitafuta haki hiyo katika vyama vingine.

“Kama hupati haki kwenye chama chako unaweza kuitafuta haki hiyo kwenye vyama vingine, mimi siogopi.  Unaweza kwenda Dar es Salaam kwa basi , kama basi limekuacha chukua pikipiki,” amesema Membe.

Bernard Membe (kulia) akisalimiana na Rais John Magufuli walipokutana katika mkutano Mkuu wa CCM 2015

Aidha, Membe amesema chochote kinaweza kutokea kwa kuwa atakwenda katika chama kitakachompendeza.

“Ninasema kutoka kwenye dhamira ya moyo wangu mpaka dakika hii, watu wanasema Membe anakwenda ACT mara Chadema, mpaka nikaeleza mimi sijaandika barua kwenda kwenye chama chochote, siwazi kwenda Chadema au ACT,” amesema Membe na kuongeza:

“Uwanja uko mezani chochote kinaweza kuja,  kitakachonipendeza (chama) naweza kufika,” Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje Mstaafu.

Membe ameviasa vyama vya siasa vya upinzani kwamba, kutorudi nyuma katika kushiriki uchaguzi huo, kwa kuwa sio dhambi kushindana na rais aliyeko madarakani

“Wala si dhambi kugombea, na mimi naomba kutumia nafasi hii kuwaambia wapinzani wasije kudhani hata siku moja kwamba ni dhambi kupambana na rais aliyeko madarani, ukidhani ni dhambi ni ujinga hii  ni haki yako kikatiba, unayohaki ya kuchagua na kuchaguliwa,” amesema Membe.

BERNARD Membe, aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, atagombea urais. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea). Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 23 Juni 2020, wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (D.W), kuhusu msimamo wake wa kugombea nafasi hiyo. Membe ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nnne amesema, dhamira ya kugombea ipo pale pale lakini hadi sasa hajafahamu atagombea kupitia chama kipi, baada ya CCM kumfukuza uanachama kutokana na utovu wa nidhamu. “Ni kweli kabisa mwaka huu 2020 nataka kugombea, kwa chama…

Review Overview

User Rating: Be the first one !

About Regina Mkonde

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!