Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Membe: Mimi ni mgombea halali, awajibu Zitto na Maalim Seif
Habari za SiasaTangulizi

Membe: Mimi ni mgombea halali, awajibu Zitto na Maalim Seif

Spread the love

BERNARD Kamilius Membe amesema, yeye bado ni mgombea halali wa urais kupitia ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, Watanzania wako tayari kwa mabadiliko kwa kuiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimeanza kuiongoza nchi hiyo tangu kupata uhuru.

Membe aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania kati ya 2007 hadi 2015 amesema hayo leo Jumatatu tarehe 19 Oktoba 2020 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mwanadiplomasia huyo amejitokeza kuzungumza na waandishi wa habari akiwa na mgombea wake mwenza, Profesa Omar Fakh zikiwa zimesalia siku tisa kufikia Uchaguzi Mkuu.

Membe amenza kuzungumza kwa kusema, “Mimi Bernard Membe ni mgombea halali wa ACT-Wazalendo wa nafasi ya Urais. Na chama chetu ni kizuri kabisa ambacho nitakipeleka 28 Oktoba 2020 vizuri kabisa.”

Amesema, ukimya wake wa muda wa kutoonekana majukwaani alikuwa anafanya mikakati ya chini kwa chini na sasa umewadiwa muda wa kurejea kufanya kampeni alizoziita za kimbunga.

“Nataka kufunga bao dakika ya 89 kutoka benchi. Watanzania mkae macho na mkae chonjo. Tumefanya kazi huku chini sasa tunakuja juu kupata bao la ushindi dakika 89 na dakika za nyongeza,” amesema Membe aliyewahi kuwa Mbunge wa Mtama Mkoa wa Lindi.

Katika kusisitiza hilo, Membe amesema, ” katika kipindi cha siku nane zikizobaki, wote walionipigia simu wananiuliza niko wapi, nawaomba muende kupiga kura. Niwaombe Serikali wakubali matokeo na wasimamie haki. Mazingira yaliyopo sasa Tanzania ni wa mabadiliko.”

Membe amejibu swali aliloulizwa kwamba Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo na Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad wamekwisha kutangaza hadharani kumuunga mkono Tundu Lissu, mgombea urais kupitia Chadema.

Akijibu swali hilo kwa ufupi, Membe amesema “Waliosema ni wao binafsi na tumeyamaliza. ACT-Wazalendo ina mgombea urais ambaye ni Bernard Kamilius Membe na katika orodha ya karatasi ya kupigia kura Membe yupo.”

Katika mazungumzo yake ya awali, Membe amesema “Sisi ndani ya ACT-Wazalendo hatuna matatizo, tunaheshimiana na kubishana kwa hoja. Nawaombea kura za madiwani na wabunge woote kuanzia kwa Zitto Kabwe huko Kigoma Mjini. Zanzibar kuna Maalim Seif Sharif. Nawaombea kura kwa wooote.

Mwanasiasa huyo mkongwe amesema, kuna wana CCM wengi wamekichoka chama hicho na watatumia fursa ya uchaguzi mkuu kukiondoa madarakani.

Amesema, mpasuko uliopo ndani ya CCM uliongezeka baada ya kura ya maoni ya ubunge ambapo siku ya pili baada ya CCM kutangaza wagombea ubunge “tulipokea maombi 42 ya waliotaka kujiunga na ACT-Wazalendo. Hii inaonyesha ndani ya CCM kuna kundi la wana CCM wamechoka.”

“Nimezungumza nao wengi, kweli inaonyesha wamechoka na kwa mazingira haya, CCM inakwenda kushindwa uchaguzi huu,” amesema Membe

Membe ametumia fursa ya mkutano huo, kuwaomba viongozi wa dini “Ninawaomba sana viongozi wetu wa dini wote, watushabikie kimya kimya. Tunaweza kuleta vita ya udini ambayo inaweza isiishe. Ninaomba kwa moyo mkunjufu, viongozi wa dini mna kazi mbili ya kuhubiri amani, haki na utulivu. Ombeeni Taifa kuwa na utulivu.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!