Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Membe ataja mtaji wa kumwingiza Ikulu, agusia katiba mpya
Habari za Siasa

Membe ataja mtaji wa kumwingiza Ikulu, agusia katiba mpya

Benard Membe, Mgombea Urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo
Spread the love

BERNARD Kamilius Membe, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama cha upinzani nchini humo cha ACT-Wazalendo ameeleza mikakati atakayoifanya yeye na chama chake, pindi atakapingia madarakani Novemba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Membe ambaye ni Mshauri Mkuu wa ACT-Wazalendo leo Jumatano tarehe 5 Agosti 2020 ameteuliwa na mkutano mkuu wa chama hicho, kuwa mgombea urais wa Tanzania kwa kupata kura 410 sawa na asilimia 97 kati ya kura 420 zilizopigwa huku kura kumi zikimkataa.

Pia, mkutano huo, umemteua Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa kupata kura 419 sawa na asilimia 99.6 ya kura zote 420.

Akitoa hotuba yake ya shukurani, Membe amesema, “niwashukuru wote kwa kunichagua mimi kuwa mgombea wa kiti cha urais wa Tanzania kupitia chama kambambe cha ACT-Wazalendo, nasema asanteni sana kwa imani mliyonipatia na mimi nasema sitawaangusha ng’oo,” amesema Membe huku akishangiliwa.

Kuhusu kujiunga kwake na ACT-Wazalendo, Membe amesema “nilipokuwa natafakari kuingia katika chama hiki, Zitto alinitembelea nyumbani kwangu Lindi mara tatu, tulikuwa na mazungumzo mazito na mimi nilimshawishi agombee nafasi ya urais kwani anazo sifa zote.”

“Lakini kama kungekuwa na uchumi mzuri, utawala bora, nchi imetifuliwa tifulifuwa inahitaji mwanadiplomasia kama wewe, inahitaji mwamba kama wewe usafishe njia, sijawahi kuona kijana mwenye akili na upendo aliyonayo kama Zitto,” amesema Membe.

Membe alijiunga na ACT-Wazalendo tarehe 7 Julai 2020 baada ya kufukuzwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 28 Februari 2020 akituhumiwa kuwa na mienendo isiyoridhisha tangu mwaka 2014.

Huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo, Membe amesema “wananchi wa Kigoma Mjini, hakikisheni tarehe 28 Oktoba 2020, mnamrudisha Zitto Kabwe kama mbunge wenu. Nitakuja mwenyewe Kigoma kuhakikisha anarudi bungeni, kuche au kusikuche.”

Zitto ni mbunge anayemaliza muda wake wa Kigoma Mjini kupitia ACT-Wazalendo.

Kuhusu mtaji walionao wa kushinda uchaguzi huo, Membe amesema, “tunao watumishi wa serikali na watumishi wa umma, katika kipindi chote cha miaka mitano, hawajapandishwa madaraja, hawalipwi vizuri, hawapewi hela za likizo, watumishi wa serikali na umma, katika kipindi cha miaka mitano hawajapandishwa mishara, sisi tukiingia madarakani tutarejesha matumaini yao.”

“Utumishi ni wajibu na kupata mshahara au mafao ni haki yake, iko wapi nchi na Serikali inyojigamba ina fedha. Watanzania wanapaswa kujua chama cha ACT-Wazalendo tukiingia madarakani, turekebishe mienendo hii. Tutaunda kikosi maalum cha kupitia zambi hii ili walipwe stahili zao,” amesema Membe.

Membe amesema “hivyohivyo na walimu, katika kipindi cha miaka mitano, tumezalisha walimu wengi lakini hawaajiliwi na shule hazina walimu, wanajihamisha wenyewe, hawapandishwi madaraja, hawapati mishahara ya kutosha, hawapati mafao yao. Sisi tutarejesha matumaini kwa walimu wote.

“Watanzania wanataka Serikali tutakayoiunda, lazima iangalie maslahi ya walimu, wale ambao hawajaajiliwa wanaajiliwa, Serikali itakayoiundwa, tutafanya kazi ya walimu wa Tanzania, bara na visiwani wanapata haki zao, wanapandishwa vyeo, wafundishwe na watoto wapate elimu bora kabisa,” amesema.

Kuhusu uraia pacha, Membe aliyekuwa waziri wa mambo ya nje katika utawala uliopita wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema, “suala la uraia pacha ni suala zito lakini ni muhimu sana kwa Watanzania. Nchi 21 za Afrika zinaruhusu wananchi wake kuchukua uraia pacha.”

“Serikali itakayoundwa na ACT-Wazalendo Novemba, tutarejesha suala hili kwa wananchi kupata uraia pacha na lazima tutoe uraia pacha,” amesema

Membe amegusia suala la mchakato wa katiba akisema, watakapoingia madarakani, watauanzisha mchakato huo kuanzia mwanzo hadi mwisho kwa kuanza na Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba.

“Mchakato wa katiba mpya tukiingia madarakani, tutauanza mara moja na tutauanza kwa Rasimu ya Jaji Warioba, tutahakikisha tunaukamilisha sisi bila kusubiri wengine waje kumalizia,” amesema Membe aliyewahi kuwa mbunge wa Mtama Mkoa wa Lindi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Akizungumzia suala la ugatuaji wa madaraka, Membe amesema “Serikali itakayoundwa na ACT-Wazalendo Novemba itaziachia halmashauri zijiendeshe kwa kukusanya mapato yao ya ndani na kuzitumia, si kama ilivyo sasa, fedha zinachukuliwa na mfuko mkuu. Sisi tutafanya mabadiliko tutakapoingia madarakani, huu ndio utawala .”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!