July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Membe amkosoa Jaji Warioba

Bernard Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,

Spread the love

MWANADIPLOMASIA mashuhuri nchini Tanzania, Bernard Kamillius Membe, amekosoa utaratibu unaotumika na Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kumtafuta mgombea wake wa urais. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Akiandika katika mtandao wake wa twitter, Membe amesema, utaratibu wa sasa wa CCM, kuzuia wanachama wengine wa chama hicho kujitosa katika mbio za urais, ili kushindana na rais wa sasa, John Pombe Magufuli,  “ni uminyaji wa demokraisa.”

 Amesema, “hata Marekani, wanaruhusu rais aliyeko madarakani na ambaye anataka kutetea nafasi yake kwa muhula wa mwingine, kupingwa na baadhi ya wanachama wa chama chake.”

Kuibuka kwa Membe kupinga utaratibu huo, kumekuja siku moja baada la waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, kujitokeza kuunga mkono Rais Magufuli, kuwa mtia nia pekee katika kinyang’anyiro cha uteuzi wa mgombea urais, kupitia CCM.

Jaji,Joseph Warioba Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Katika maoni yake, wakati akihojiwa na MwanaHALISI ONLILE,  Jaji Warioba alisema, kama chama kinachoshika dola kinaona rais aliyeko madarakani, anafaa kuendelea tena, hakuna sababu ya watu wengine, kujitokeza kuomba nafasi hiyo.

Jaji Warioba alitoa kauli hiyo jana tarehe 23 Juni 2020, kufuatia mwandishi wa MwanaHALISI kumtaka maoni yake kuhusiana na mchakato wa uchukuaji fomu za urais wa Tanzania na Zanzibar, kupitia chama hicho tawala.

Hadi sasa Rais Magufuli ndiye kada pekee wa CCM aliyechukua fomu ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano, tangu chama hicho kifungue zoezi hilo, tarehe 15 Juni 2020. Mchakato wa uchukuaji fumo za urais – Muungano na Zanzibar – limepangwa kufungwa 30 Juni.

Jaji Warioba alirejea kilichotokea nchini Marekani, ambako alidai kuwa chama tawala cha Republicans, kimempitisha Donald Trump, rais anayemaliza muda wake, kugombea tena nafasi hiyo.

Hata hivyo, Membe amekosoa kauli hiyo akisema, Marekani hawana utamaduni wa kukataza wanachama wengine wa chama kilichoko Ikulu, kushindana na rais anayetaka kutetea tena kiti chake.

Membe ambaye amepata kuhudumu kwenye nafasu ya waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa amesema, “Republicans kimepitisha Trump kugombea tena urais, lakini baada ya kushinda katika kura za maoni.”

Amesema, “lakini kimempitisha Trump kuwa mgombea, kwa sharti la kushinda kura ya maoni iliyompambanisha na wenzake watatu, Bill Weld, Joe Walsh na Roque de la Fuente.

Ameongeza: “Marekani hawana utamaduni kama wa kwetu wa kukataza na kubeza wagombea wengine!”

Membe ambaye anadaiwa kuwa amefukuzwa uanachama wa CCM, amekuwa kwenye mgogoro na chama chake, tangu alipoonesha nia ya kutaka kugombea urais wa Tanzania, kukabiliana na Rais Magufuli, miaka mitatu iliyopita.

Hivi karibuni, mwanasiasa huyo amekuwa akitoa kauli zenye kukosoa mchakato wa utafutaji mgombea urais wa Tanzania ndani ya CCM, kwa madai kwamba umegubikwa na vitisho.

Katika mahojiano yake na Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW), yaliyorushwa hewani jana Jumanne, Membe alidai  kuwa makada takribani sita wa CCM, wana nia ya kuchukua fomu ya kugombea urais wa Tanzania, lakini wanahofia kufukuzwa kwenye chama.

Amesema, ana majina ya wanachama wa chama hicho wanaotaka kuchuana na Rais Magufuli kwenye mchakato unaoendelea, lakini anaogopa kuanika majina yao hadharani, kwa maelezo kuwa wakijulikana watafukuzwa uanachama.

Aidha, Membe amesema, hata alipokuwa anahojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM, tarehe 6 Februari 2020, makao makuu ya chama hicho, mjini Dodoma, walimuuliza kwa nini anataka kugombea urais, wakati rais aliyeko madarakani muda wake wa kuongoza haujaisha.

Membe na wenzake wawili – Abdulrahaman Kinana na Yusufu Makamba – walihojiwa na kamati ya maadili ya chama hicho tawala nchini Tanzania, kufuatia kukabiliwa na tuhuma za utovu wa maadili.

Makamba na Kinana wamewahi kuhudumu kwenye nafasi ya katibu mkuu wa CCM.

Kuhojiwa kwa makada hao watatu, kumefuatia “vuta ni kuvute” ya muda mrefu ya muda ndani ya chama, baada ya wote watatu, kumtuhumu Rais Magufuli, kukiendesha vibaya chama chao na serikali anayoingoza.

Makada wengine watatu, Januari Makamba, Nape Nnauye na William Ngeleja, walisamehewa baada ya kumuomba radhi mwenyekiti wa CCM, Rais John Pombe Magufuli.

error: Content is protected !!