April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Membe ‘aitwa’ ACT-Wazalendo

Bernard Membe, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Tanzania

Spread the love

BERNALD Membe, aliyekuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya awamu ya nne, amekaribishwa ndani ya Chama cha ACT-Wazalendo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communication (MCL), jijini Dar es Salaam, Maalim Seif Sharif Hamad, Mshauri Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema, milango ya chama hicho ipo wazi kwa kila Mtanzania kujiunga.

Hata hivyo amesema, Membe ambaye alitimuliwa CCM kwa madai ya utovu wa nidhamu, kama mwanachama yeyote anayetaka kujiunga na chama hicho, hapaswi kutoa masharti kama ilivyokuwa kwa Edward Lowassa alipojiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Alipoulizwa kama chama chake kipo tayari kumpokea Membe, Maalim Seif amesema “Membe? Sie tunapokea yeyote atakayekuja, asije na masharti, tunampokea.”

Amesema, utaratibu wa chama hicho ni kuwa, mtu yeyote anaruhusiwa kujiunga na chama hicho lakini si kuingia kwa masharti, ikiwa ni pamoja na kuteuliwa kugombea urais.

Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, alitokea CCM na kujiunga na Chadema kwa sharti la kugombea urais kupitia chama hicho.

Ujio wa Lowassa Chadema na kuteuliwa kugombea urais akiwakilisha vyama vilivyokuwa chini ya mwavuliwa wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ulisababisha mgogoro mkubwa.

Miongoni mwa matokeo ya mgogoro huo, Dk. Wilibrod Slaa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema alijiuzulu na mgogoro uliongezeka kati ya Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF na Prof. Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa chama hicho hivyo CUF kupasuka.

error: Content is protected !!