Thursday , 18 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Mdhamini wa Lissu afunguka
Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Mdhamini wa Lissu afunguka

Robert Katula
Spread the love

ROBERT Katula, mdhamini wa kwanza wa mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu, ametaja sababu tatu kubwa za kuomba kujitoa kwenye udhamini wa mwanasiasa huyo. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Katula, meneja mkuu wa kampuni ya uchapishaji ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL) – wachapishaji wa magazeti ya MwanaHALISI, MSETO na wamiliki wa MwanaHALISI ONLINE na MwanaHALISI TV – amesema, “kujitoa kwangu kunatokana na kutopata ushirikiano wa kutosha na mdhaminiwa na masharti mapya niliyopewa na Mahakama.”

Akizungumza na MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV, Katula ametaja masharti hayo, kuwa ni pamoja na kutakiwa kufika mahakamani kila siku ambayo kesi hiyo inatajwa, ili kutoa taarifa ya hali ya Lissu na maendeleo ya matibabu yake.

Lissu anayekabiliwa na mashitaka ya uchochezi, yuko nchini Ubelgiji anakopatiwa matibabu kufuatia kushambuliwa kwa risasi na “watu wasiojulikana,” mchana wa tarehe 7 Septemba 2017, nje ya nyumba yake, maeneo ya Area C, mjini Dodoma.

“Mahakama inajua kuwa taarifa za mgonjwa na maendeleo ya ugonjwa wake, ni siri ya mgonjwa mwenyewe. Sasa kunitaka mimi kufika mahakamani ili kueleza maendeleo ya mgonjwa, ni kuniingiza kwenye kitu ambacho kiko nje ya uwezo wangu,” ameeleza Katula.

Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, Thomas Simba, aliagiza Katula na mdhamini mwingine wa Lissu aitwaye Ibrahim Ahmed, kufika mahakamani kila shauri hilo linapotajwa na kutoa taarifa za kuwapo mwanaisasa huyo wa upinzani nchini Ubelgiji kwa matibabu na hali yake inavyoendelea.

Kwa mujibu wa Katula, tangu mahakama itoe maelekezo hayo, ameshindwa kupata ushirikiano kutoka kwa mdhaminiwa wake na hivyo kumfanya kushindwa kutekeleza maelekezo ya mahakama.

Amesema, “…sijatishwa, wala sijashawishiwa au kupokea shinikizo lolote, kutoka kwa mtu yeyote; na au mamlaka nyingine yeyote, ili mimi niweze kujiondoa kwenye shauri hili. Kwa kweli, hapana.

“Nimeomba kujiondoa kwa sababu, tangu mahakama itoe maekelezo hayo na mimi kumueleza mheshimiwa Lissu juu ya maamuzi hayo, nimeshindwa kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwake wa kuniwezesha kutekeleza maelekezo ya mahakama.”

Katula amesema, “nimejitahi kuongea na Lissu na yeye muda wote, amekuwa akisisitiza kuwa ugonjwa wake na matibabu yake, ni suala linalomhusu yeye binafsi.”

Katula ametoa kauli hiyo, kufuatia madai ya baadhi ya wafuasi wa mwanasiasa huyo machachari wa upinzani nchini kudai kwamba, hatua yake ya kujitoa kwenye udhamini, imetokana na shinikizo kutoka nje.

Amesema, mara mara ya mwisho walivyozungumza na Lissu, alimueleza kuwa anatakiwa amfahamishe daktari wake ili amuandikie barua itakayo tumika mahakamani kama ushahidi wa kuwa yupo kwenye matibabu na sababu za yeye kuendelea kuwapo Ubelgiji.

Aidha, Katula amesema, uamuzi wake wa kuomba kujitoa kwenye udhamini, umetokana na yeye kuwa mgonjwa na hivyo, kutakiwa kwenda kwenye matibabu nchini India.

“Hata mimi mwenyewe, ni mgonjwa. Kila mara hutakiwa kusafiri kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu, jambo ambalo kuendelea kubaki kuwa mdhamini, kunaweza kukwamisha matibabu yangu,” ameeleza.

Katula ametaja sababu nyingine inayosababisha kuomba kujitoa,  ni kubanwa na majukumu yake ya kikazi kutoka kwa mwajiri wake.

Amesema, “kwa masharti haya, mimi sasa nakuwa kama ndiyo mshitakiwa. Kwamba kila siku ya kesi, natakiwa kufika mahakamani. Hii ni tofauti na ilivyokuwa wakati nachukua maamuzi ya kumdhamini.”

Anaongeza, “..wakati ule, ilikuwa rahisi; mheshimiwa Lissu alikuwa anakwenda mahakamani mwenyewe na labda ikitokea akashindwa kwenda, basi itakuwa mara moja au mbili kwa kipindi cha mitatu au hata sita.”

Lissu, mbunge wa Singida Mashariki, mwanasheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na  Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, anakabiliwa na kesi kadhaa za jinai mahakamani nchini.

Katika kesi hii, washitakiwa wake wengine, ni wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrissa, pamoja na mfanyakazi wa kampuni ya uchapishaji wa magazeti ya Jamana, Ismail Mehboob.

Hakimu Simba alikatalia ombi la Katula la kujiondoa kwenye kesi hiyo, hadi pale Lissu atakapofika mbele ya mahakamani yake.

Amemtaka mdhamini huyo kufika tena mahakamani, tarehe 25 Aprili.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!