January 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mdee, wenzake 18 kufunguka

Halima Mdee, Mbunge wa Chadema Viti Maalim

Spread the love

SIKU moja baada ya Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, kuwafukuza uanachama, Halima Mdee na wenzake 18 kwa tuhuma za usaliti, wabunge hao wa viti maalum, watazungumza na waandishi wa habari kesho Jumapili 29 Novemba 2020 jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa jana usiku Ijumaa, baada ya kikao cha siku nzima kufanyika chini ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe jijini Dar es Salaam kuazimia kwa kauli moja wafukuzwe.

Mdee na wenzake, walikuwa wakituhumiwa kwa “usaliti, kughushi na uasi” wa chama hicho kwa kujipeleka kuapishwa tarehe 24 Novemba 2020 na Spika Job Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum, wakijua chama hicho, hakijapendekeza majina yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wabunge wengine waliofukuzwa ni wale waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ester Bulaya na Esther Matiko. Katibu Mkuu wa Bavicha, Nusrat Hanje. Katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Grace Tendega.

Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga. Naibu Katibu Mkuu Bawacha, Jesca Kishoa na Katibu Mwenezi Bawacha, Agnesta Lambat.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Mtwara, Tunza Malapo, Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao.Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Mbowe aliyetoa maazimio ya kikao hicho alisema, Mdee na wenzake 18, wanaweza kukata rufaa ndani ya siku 30 kwa Baraza Kuu la Chadema au kuomba radhi hadharani kwa walichokifanya.

Leo Jumamosi, MwanaHALISI Online, limezungumza na baadhi ya wabunge hao wa viti maalum kujua msimamo wao mpaka sasa ni upi mmoja wao amesema, “kwa sasa siwezi kusema lolote, tunamzungumzaji mmoja na atazungumza katika mkutano na waandishi wa habari.”

Mwingine ambaye alikuwa mjumbe wa kamati kuu amesema, “kesho tutazungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam. Karibuni na ninyi kwenye mkutano wetu. Mtaelezwe baadaye utakapofanyikia.”

error: Content is protected !!