Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mdee, Bulaya waponea ‘tundu la sindano’
Habari za Siasa

Mdee, Bulaya waponea ‘tundu la sindano’

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapa onyo kali,  Halima Mdee, Mbunge wa Kawe na Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kwa kukiuka masharti ya dhamana. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Onyo hilo limetolewa jana tarehe 24 Januari 2020, na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, kwenye kesi  namba 112/2018, ya uchochezi inayowakabili Bulaya, Mdee pamoja na viongozi saba wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wakati anatoa uamuzi huo ,hakimu Simba amesema mahakama hiyo imeridhishwa na ushahidi wa Jamhuri ,  juu ya kukiukwa kwa dhamana kulikofanywa na wabunge hao.

“Mahakama imejitosheleza kwamba hakuna wasiwasi wowote kama mshtakiwa namba 7 (Mdee) na namba tisa (Bulaya) wamekiuka masharti ya dhamana …kwa sababu hizo, barua ya Daktari haina maana yoyote kwa sababu yeye hana lolote kwenye mkataba wa dhamana,” ameeleza Hakimu Simba na kuongeza;

“Mahakama inatoa onyo kali, sijaona kuwa ni vizuri kuwafutia dhamana washtakiwa. Lakini pia sijaona ni vizuri wadhamini kulipa bondi ya dhamana waliyosaini. Kwa kipindi hiki, mahakama inawaonya na  walichokifanya kina hatarisha usalama wa dhamana zao. hiyo ni huruma ya mahakama.”

 Hakimu Simba ameeleza kuwa, pamoja na upande wa mashtaka kuthibitisha ukiukwaji wa mashart hayo na kutaka mahakama hiyo kushikiria hati zao za kusafiria(Passport) , lakini  mahakama hiyo imewaacha waendelee kubaki na hati hizo.

Awali tarehe 20 Januari 2020, upande wa Jamhuri kupitia wakili wake Mkuu, Faraja Nchimbi ulidai kwamba una taarifa za uchunguzi zinazoonesha kuwa, wiki mbili zilizopita Bulaya na Mdee walionekana uwanja wa ndege.

Wakirejea safari ya Kenya, kwa hati ya kusafiria ya Bulaya yenye namba TBE 011989, na ya Mdee yenye namba TBE 011991, ambapo aliiomba mahakama hiyo, iamuru watuhumiwa hao waeleze kama walisafiri kwa kibali cha mahakama.

John Mallya, Wakili wa Utetezi aliieleza mahakama hiyo kuwa, isipoteze muda wake kusikiliza hoja hizo. Hata hivyo, Hakimu Simba amesema kuwa ipo haja ya watuhumiwa kueleza iwapo walisafiri kwa kibali cha mahakama.

 Mdee alieieleza mahakama hiyo kuwa, hakwenda Kenya bali alikwenda Nchini Afrika Kusini kwa Matibabu. Na kwamba, alipata kibali cha mahakama baada ya Daktari wake kutoka Hospitali ya Agha Khan, kuandika barua ya kumuombea ruhusa na pamoja na Wakili wake.

 Ambapo Bulaya naye aliombewa kwa ajili ya kumsindikiza. Bulaya aliieleza mahakama hiyo aliruhusiwa kusafiri na Mdee, kwa ajili ya kumsindikiza.

Wakati huo huo, Wakili wa Jamhuri,  Nchimbi aliiomba mahakama hiyo iwaite wadhamini wa washtakiwa hao,  ili waeleze kwanini wadhamana wao walisafiri bila kibali cha mahakama. Kwa kuwa   wamekiuka masharti ya dhamana

Pia,  aliiomba mahakama hiyo iamuru watuhumiwa hao,  kueleza kwa nini wasifutiwe dhamana zao.

“Tarehe 13 Januari 2020 Wakili Hekima Mwasipu,  aliwasilisha ombi mahakamani juu ya kuwaombea washtakiwa wote tisa waende Kenya. Lakini tarehe 15 Januari 2020, mahakama iliyakataa maombi hayo na hapakuwa na maombi ya kusafiri kwenda Afrika Kusini,” amedai Wakili Nchimbi.

Wakili wa upande wa utetezi, Mallya aliieleza mahakama hiyo kwamba, maombi ya watuhumiwa hao yalikuwa ni ya kisheria, na mahakama inasimamia sheria. Lakini ombi la jamhuri halina msingi wowote wa kisheria.

 Washtakiwa wengine kwenye shauri hilo ni; Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa ; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini ; John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chama hicho (Hakuwepo mahakamani); Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini; Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; Salum Mwalim, Naibu Katibu Mkuu- Zanzibar na Vincent Mashinji -Mwanachama Mwandamizi wa chama hicho.

Washtakiwa hao wanadaiwa tarehe 16 Februari 2018 walifanya kusanyiko lililokinyume cha sheria, lilosababisha kifo cha Mwanafunzi wa chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwelina Akwelin, na kutoa maneno ya uchochezi.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!