February 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mdee, Bulaya wapata pigo jingine 

Spread the love

HALIMA James Mdee, aliyekuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),” amepata pigo jingine. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam  … (endelea).

Mdee na wenzake watatu, walipata pigo hilo, baada ya aliyekuwa wakili wao, Peter Kibatala, kujiondoa kwenye kesi ya jinai inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Mbali na Mdee, wengine waliopata pigo hilo, ni pamoja na swahiba wake mkuu, Ester Bulaya na aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jessa Kishoa.

Hilo ni pigo la pili kwa Mdee, Bulaya na wenzake,  baada ya wiki iliyopita, kutimuliwa uanachama wa Chadema na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, kufuatia madai ya usaliti, uasi, utovu wa maadili na kwenda kinyume na maelekezo ya chama.

Makosa mengine yaliyowakabili, ni kujipeleka bungeni na kuapishwa, kinyume na msimamo wa chama; kuhujumu chama, kusingizia viongozi wakuu wa chama, kughushi nyaraka za chama, kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama, kutengeneza migogoro ndani ya chama, kuleta taharuki, kujenga mifarakano na upendeleo.

          Soma zaidi:-

Kwa sasa, wote 19 ni wabunge wa Bunge la Muungano, wanaotambuliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, wanachama wa hiari wa Chadema na wabunge “wasiokuwa na chama rasmi” kilichowapeleka bungeni.

Wengine waliofukuzwa Chadema na kubaki kuwa wabunge kwa “amri ya Spika,” kuwa wanachama wa hiari wa Chadema na kutokuwa na chama rasmi kilichowapeleka bungeni, ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga; aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Serengeti, Esther Matiko na aliyekuwa katibu mkuu Bawacha, Grace Tendega.

Katika orodha hiyo, yumo pia aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Nusrat Hanje; aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat; Mwenyekiti wa Chadema mkoa Mtwara, Tunza Malapo na aliyekuwa mbunge wa Same Mashariki, Naghenjwa Kaboyoka.

Wengine, ni waliokuwa wabunge wa Viti Maalum, Kunti Majala, Sophia Mwakagenda, Cecilia Pareso, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Lwamlaza, Asia Mwadin Mohamed, Stella Siyao na Felister Njau.

Katika kesi hiyo, Mdee na wenzake 26, wanatuhumiwa kuvamia gereza la mahabusu la Segerea, kuharibu mali za gereza, kutoa lugha ya matusi na kuhatarisha usalama wa mahabusu na wafungwa.

Kibatala ameieleza mahakama ya Kisutu kuwa amelazimika kujiondoa kuwatetea Mdee, Bulaya na Kishoa, baada ya watuhumiwa hao, kufukuzwa uanachama wa Chadema, ambako yeye ni mmoja wa mawakili wa chama hicho.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi 19 Januari 2020, huku Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, akilazimika kutoa hati ya kukamatwa kwa  washtakiwa wawili, Edgar Adelini, Reginald Masawe, kutokana na kutofika mahakamani bila kutoa taarifa.

Kabla ya kesi hiyo yenye mashtaka saba, Kibatala alijitoa kuwatetea Mdee na wenzake watatu.

Mara baada ya Kibatala kujitoa kuwatetea Mdee, Bulaya na Kishoa, watuhumiwa hao walimtambulisha wakili wao mpya, Emmanuel Vkandis.

error: Content is protected !!