Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mdee, Bulaya njia panda
Habari za Siasa

Mdee, Bulaya njia panda

Spread the love

HALIMA Halima Mdee, Mbunge wa Kawe na Esther Bullaya, Mbunge wa Bunda wamebaki ‘njia panda’. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Ni baada ya Thomas Simba, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam kutotoa uamuzi wake juu ya hatua ya watuhumiwa hao, kusafiri nje ya nchi bila kibali cha mahakama.

Leo tarehe 21 Januari 2020, Hakimu Simba aliahidi kutoa uamuzi huo, lakini hakufanya hivyo na badala yake, amesema atautoa tarehe 31 Januari 2020. Ni uamuzi wa kufuta dhamana zao ama la.

Hata hivyo, Mdee amejitetea kutofutiwa dhamana yao akidai, alilazimika kusafiri kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa ulioshindikana nchini.

Kwenye shauri hilo namba 112/2018, Bulaya na Mdee wanashtakiwa na vingozi saba wakiwemo Freman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema – Taifa; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini; John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema; Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini; Salum Mwalim, Naibu Katibu Mkuu- Zanzibar na Vincent Mashinji – mwanachama mwandamizi wa chama hicho.

Mdee amedai, tarehe 6 Januari 2020, daktari wake wa Hospitali ya Aghakan, aliyemtaja kwa jina la Kaguta, aliiandikia barua mahakama hiyo kwamba, mgonjwa wake (Halima Mdee) anatakiwa akapate matibabu ya ziada, ambayo hospitali za ndani ya nchi wameshindwa kuyatoa.

Mdee amedai, taarifa ya kwenda kwenye matibabu, aliitoa mara mbili mahakamani hapo, tarehe 25 Novemba na 18 Disemba 2019, mbele ya wakili wa serikali, Sylivia Mitanto.

Kwa upande wa Bulaya, amedai kuwa alipewa jukumu la kumuangalia Mdee akiwa kwenye matibabu nchini Afrika Kusini, kwa kuwa yeye ni mwanamke mwenzake na mama wa Halima ni mzee sana.

Akipinga hoja hizo, wakili wa serikali mwandamizi Wankyo Simon amedai, sababu zilizotolewa hazina msingi na zinatosha kuifanya mahakama hiyo kufuta dhamana zao kwa kukiuka sharti la msingi, la kusafiri nje ya nchi bila kibali.

Wankyo ameongezea, masharti ya dhamana yaliwataka kupata kibali kutoka mahakamani na sio kuwasilisha taarifa ili waweze kusafiri nje ya nchi.

Wakili wa serikali mkuu, Faraja Nchimbi amedai kuwa, ni mara ya pili washtakiwa wanakiuka masharti ya dhamana, hivyo ameiomba mahakama kufuta dhamana zao au kushikilia hati zao za kusafiria kama mbadala.

Wakitetea hoja hizo, wakili wa utetezi John Mallya amedai, watuhumiwa hawakukamatwa bali walikuja mahakamani wenyewe, hawakupita kwenye mipaka ya nchi kwa njia za panya na hawana mpango wa kukimbia nchi, hivyo hakuna sababu ya kufuta dhamana zao.

Hekima Mwasipu, wakili wa utetezi amedai, kuhusu barua kuandikwa na mshtakiwa, sio takwa la kisheria bali la msingi ilikuwa mahakama kupata taarifa.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Simba amesema, atatoa uamuzi juu ya kufutwa au kutofutwa kwa dhamana hizo Ijumaa ya tarehe 31 Januari 2020, ambapo kesi ya msingi itaendelea kusikilizwa kesho tarehe 22 Januari 2020.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

Habari za Siasa

Wizara ya afya yataja mafanikio 10 miaka mitatu Samia madarakani

Spread the loveWIZARA ya Afya imetaja mafanikio 10 iliyoyapata ndani ya miaka...

Habari za Siasa

Mbozi walilia kuwa manispaa, majimbo 3

Spread the loveHALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeeleza dhamira yake...

Habari za Siasa

Wabunge waitaka TPDC kuongeza kasi ya kuunganisha wateja gesi asilia

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini...

error: Content is protected !!