Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbunge wa CCM anusurika kipigo bungeni
Habari za SiasaTangulizi

Mbunge wa CCM anusurika kipigo bungeni

Baadhi ya wabunge wa Ukawa wakilalamikia jambo bungeni. Picha ndogo, Juliana Shonza akichangia bungeni
Spread the love

JULIANA Shonza, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) amenusurika kuangushiwa kipigo kikali na wabunge wa Chadema mara baada kuwatambia kuwa atahakikisha Halima Mdee, Mbunge wa Kawe (Chadema), anaendelea kukaa nje ya Bunge kwa mwaka mzima, anaandika Dany Tibason.

Tukio hilo limetokea leo katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma ambapo Shonza alisikika akisema atapeleka hoja bungeni ili adhabu ya Mdee kutohudhuria vikao vya bunge iongezewe.

Itakumbukwa kuwa Mdee na Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini wamefungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda wa mwaka mmoja huku adhabu hiyo ikipingwa vikali ambapo tayari Bulaya na Mdee wamefungua kesi mahakamani kupinga.

Suzan Kiwanga, Mbunge wa Jimbo la Mlimba (Chadema) ambaye alikuwa karibu na Shonza ambapo alimtaka mbunge huyo kuacha siasa za chuki na roho mbaya kwani hata Mdee akikaa nje ya bunge hatofaidika na lolote.

“Acha roho mbaya. Wewe ni mwanamke, unafurahia vipi mwenzako akipata matatizo? Kukaa kwake nje hakuwezi kukusaidia kitu na kumbuka malipo ni hapa hapa duniani,” alifoka Kiwanga.

Kauli ya Kiwanga iliamsha hasira za Shonza ambaye alianza kumtolea maneno machafu yasiyofaa kuandikwa gazetini. Ndipo baadhi ya wabunge wa Chadema waliokuwa jirani akiwemo Pauline Gekul, Mbunge wa Babati Mjini na Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, wakamvaa na kumtaka awe heshima kwa kuangalia umri wa mbunge aliyekuwa akimtolea maneno machafu.

Shonza hakutaka kuwaelewa wabunge hao, aliendelea kukabiliana nao huku akifoka kwa hasira na ghafla akaanza kuangua kilio ndipo Tweve na Zainab Vullu, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), wakamvuta na kumtoa nje ya geti la Bunge akipiga kelele zilizoambatana na kilio.

“Niacheni, Niacheni…..kama wanataka kunipiga waacheni wanipige tu.. niacheni niacheni,” alizungunza Shonza huku akijitahidi kujivuta kutoka mikononi mwa wabunge wa CCM waliokuwa wanamvuta.

“Mhe. Vullu hebu mfunzeni adabu huyu binti, huenda ana matatizo makubwa ya akili, haiwezekani anawatolea maneno machafu watu wazima huku akitaka kupigana nao, hii ni aibu. Huyu binti mnamuangalia tu wakati anaharibikiwa,” amesema Gekul.

Upendo Peneza, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) ambaye alikuwepo katika eneo hilo alisema “Tatizo Shonza anapenda kukurupuka. Anatia aibu sana, binti mdogo anataka kupigana na watu mtu mzima mwenye umri wa mama yake.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!