Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbunge Tundu Lissu amvaa Prof. Kabudi 
Habari za SiasaTangulizi

Mbunge Tundu Lissu amvaa Prof. Kabudi 

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

MBUNGE wa Singida Mashariki (CHADEMA) na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu, “amempasha,” Prof. Palamagamba Kabudi. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Lissu anasema, waziri huyo mpya wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, anapaswa kufahamu kuwa huu siyo tena wakati wa watu wa kufokewa; au kutishiwa kama watoto wa shule wa zamani.

Anasema, “nimemsikia waziri wetu mpya wa Mambo ya Nje, akifokea na kutishia watu anaodai wanaisema vibaya na kuibagaza nchi yetu. Huyu ni profesa wa sheria, lakini anayeelekea kutokufahamu au kutoamini matakwa ya Katiba na Sheria za nchi yetu. 

Lissu anasema, “kwa mujibu wa Katiba yetu, kuna tofauti kubwa kati ya Nchi na Serikali. Matendo maovu ya vyombo vya usalama kama Jeshi la Polisi au Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi; au ya viongozi wa serikali kama Rais, Mawaziri au Wakuu wa Mikoa na Wilaya; na au watendaji wake wengine, sio matendo ya Nchi bali ni matendo ya Serikali.”

Lissu alitoa maelezo hayo kufuatia Prof. Kabudi, kuhutubia taifa na kusema, “nchi hii iliyojengwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, siyo nchi ya kuchezewa. Siyo nchi ya kubezwa. Siyo nchi ya kudharauliwa. Siyo nchi kudhihakiwa.”

Alisema, “kama kuna Mtanzania mwenye matatizo na nchi hii, ni vema akae kimya kama yamemshinda kuyasema matatizo hayo ndani ya nchi yake.”

Prof. Kabudi alitoa kauli hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuapishwa kushika nafasi hiyo ya uwaziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa.

Alikuwa mbele ya rais, Dk. John Pombe Magufuli, Jaji mkuu, Spika wa Bunge na viongozi wengine mbalimbali, wakiwamo wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Prof. Kabudi aliteuliwa na Rais Magufuli kushika nafasi hiyo, Jumatatu iliyopita. Kabla ya kushika wazifa huo, waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, alikuwa mwanadipromasia mahiri na mbobezi wa masuala ya kimataifa, mtalaamu wa utatuzi wa migogoro na jasusi aliyebobea, Dk. Augustine Philip Mahiga.

Prof. Kabudi alikuwa waziri wa katiba na sheria. Kufuatia mabadiliko hayo, Dk. Mahiga sasa ndiye waziri wa katiba na sheria.

Hata hivyo, katika hotuba yake hiyo, Prof. Kabudi hakutaja jina la mtu anayedai kuwa amekuwa akiisema vibaya nchi yake mbele ya jumuiya ya kimataifa.

Lakini ni Lissu pekee kwa sasa, anayetajwa na viongozi wakuu wa serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wabunge wa chama hicho, kuwa anazunguuka mataifa mbalimbali kueleza mabaya ya serikali na kuichafua nchi mbele ya uso wa dunia.

Mbali na kumshambulia anayedai kuchafua nchi ulimwenguni, Prof. Kabudi aliwageukia nchi wahisani kwa kusema, “mwenye matatizo na Tanzania, milango iko wazi na anakaribishwa kueleza matatizo yake.”

Akaongeza, “lakini tunawakaribisha wale wanaotutakia mema.”

Akijibu madai hayo, Lissu anaendelea kusisitiza, kwa mujibu wa maelezo ya Katiba, “Nchi’ ya Tanzania ni ile inayotamkwa kwenye Ibara ya 1 na 2(1) ya Katiba kuwa “… ni Jamhuri ya Muungano (inayojumuisha) … eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.”

Anasema, kwa upande mwingine, serikali Tanzania imefafanuliwa katika ibara ya 6 ya Katiba. Kwamba, “… ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali za mitaa na pia mtu anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali yoyote.”

Akinukuu sheria hiyo kuu ya nchi, Lissu anaeleza, “kwa mujibu wa Ibara ya 3(1) ya Katiba yetu, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia; yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Siyo nchi ya chama kimoja kama ilivyokuwa zamani, kwa hiyo kuipinga au kuikosoa Serikali iliyoko madarakani sio kosa, bali ni kutekeleza matakwa ya Katiba,” anafafanua.

Lissu, mwanasiasa, wakili wa mahakama kuu na mwanaharakati wa haki za binadamu na utawala bora anasema, kwa mujibu wa Ibara ya 8(1)(a), wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi….”

Aidha, Lissu ambaye amepata kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), anasema huku akivavadua Katiba, “Ibara ya 8(1)(c) ya Katiba ya Jamhuri inasisitiza, “serikali kuwajibika kwa wananchi” na kwamba  “sisi wananchi ndio tuko juu ya Serikali.

“Hivyo basi, kuipinga, kuisema vibaya, kuibagaza au kuichafua serikali hiyo kutokana na matendo yake maovu, hakuwezi kuwa kosa hata kidogo, bali ni sehemu ya kuiwajibisha kwetu.”

Amemtaka Prof. Kabudi kuelewa kuwa serikali ina wajibu mbele ya jumuiya ya kimataifa wa kuheshimu haki za binadamu zilizoainishwa kwenye Katiba yetu.

Anasema, Ibara ya 9(f) ya Katiba inaitaka “… Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote … kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha … kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu.”

Anasema, serikali imesaini mikataba mbali mbali ya kimataifa na ya kikanda inayoilazimisha kuheshimu haki za binadamu za wananchi wake; serikali imekubali, kwa kusaini Mkataba wa Roma unaounda Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Kupitia mkataba huo, serikali imeahidi itawajibika kwa jumuiya ya kimataifa kwa vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyokatazwa na Mkataba wa Roma.

“Kama sehemu ya uwajibikaji wetu mbele ya jumuiya ya kimataifa kuhusu masuala ya haki za binadamu, Lissu anasema, “Serikali yetu inatakiwa kupeleka taarifa ya utekelezaji wa wajibu wake huo kwenye vyombo vya uwajibikaji vya kimataifa, kama vile Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

“Hivi ndivyo alivyofanya Profesa Kabudi mwenyewe wiki iliyopita kule Geneva, Uswisi.

“Kwa sababu hiyo, kuisema vibaya Serikali yetu nje ya Tanzania, kwa sababu ya matendo yake maovu dhidi ya Watanzania, ni sehemu tu ya kuitaka Serikali yetu iwajibike kwa jumuiya ya kimataifa kwa mambo ambayo tumekubali kuwajibika nayo kimataifa. Katiba yetu imetupatia Haki ya Uhuru wa Mawazo na Uhuru wa Maoni.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 18(1), kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”

Lissu anasema, kwa muktadha huo, “matendo haya ya serikali yanaweza yakapingwa, kubezwa, kubagazwa, kusemwa vibaya au kuchafuliwa bila kuichafua au kuibeza au kuibagaza Nchi.

“Kuisema Serikali vibaya, au kuibagaza, au kuichafua – ndani au nje ya nchi – kwa sababu ya matendo yake maovu, sio kosa bali ni wajibu wa kila mtu na hasa kila raia wa Tanzania.”

Kwa sababu zote hizi, Lissu anaeleza, “kama Prof. Kabudi yeye na serikali anayoitumikia hawaamini matakwa haya ya Katiba yetu, sisi tunayaamini na tutayatekeleza matakwa hayo kwa nguvu zote.”

Alipoulizwa iwapo baada ya kauli hiyo ataweza kunyamaza, Lissu anasema, “mwambieni Prof. Kabudi, kwamba hatutanyamazishwa na uovu wao, au vitisho vyao, au na ulaghai na propaganda zao, au na hongo na rushwa zao.

“Tutaendelea kuyasema hadharani, popote pale, ndani na nje ya Tanzania, maovu ya Serikali yetu, na ya vyombo vyake, na ya viongozi wake na ya watendaji wake.”

Maelezo ya Lissu yako kwenye andishi lake alilolisambaza kwenye mitandao kadhaa ya kijamii na kuthibitishwa kwa kauli yake na yeye mwenyewe.

Katika siku za hivi karibuni, Lissu ambaye yuko kwenye matibabu nchini Ubelgiji, amefanya mikutano na watu mbalimbali katika nchi za Ubelgiji, Ujerumani, Marekani na Uingereza.

Amefanya mahojiano pia na vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa, akiituhumu na kuishutumu Serikali ya Rais Magufuli, kuminya uhuru wa kujieleza na kuvunja misingi ya kidemokrasia.

Lissu yuko nchini Ubelgiji, tokea 6 Januari 2018, kufuatia kushambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika,” nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma.

Shambulio dhidi ya Lissu lilitokea tarehe 7 Septemba 2017, muda mfupi baada ya kushiriki mkutano wa Bunge wa asubuhi na kulihutubia Bunge.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo akomalia matumizi nishati jadidifu kuondoa uhaba wa umeme

Spread the love  MBUNGE wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea...

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

error: Content is protected !!