MBUNGE Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Mariam Kisangi ameishauri serikali kuongeza idadi ya shule za watoto wenye mahitaji maalumu, akisema wengi wao wanakosa elimu kutokana na changamoto ya uhaba wa shule hizo. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Akizungumza bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 31 Mei 2019 Mariamu amesema kume kuwepo na ongezeko la watoto wenye mahitaji maalum, na kwamba shule zilizopo hazina uwezo wa kubeba idadi hiyo.
“Kumekuwa na ongezeko la watoto wenye mahitaji maalum, kwa kuwa shule maalum zilizopo zinakuwa hazitoshelezi mahitaji, serikali haioni sababu ya kuongeza vitengo vya watoto wenye mahitaji maalum ili na wao waweze kupata elimu kwenye maeneo wanayotoka?” amehoji Mariam.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mwita Waitara amesema serikali imekwisha toa agizo kwa halmashauri nchini kuhakikisha kwamba wanajenga miundombinu rafiki kwa watoto wenye uhitaji kwenye shule zilizopo nchini.
“Baada ya kuona unapotenga shule maalum unakuwa unawatenga, sasa imekuja elimu jumuishi, na tumetoa agizo kwenye ujenzi wa miundombinu iweke miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, na wanafunzi wawaone kuwa hao ni wenzao, na tunaongeza nguvu na ombi lako tutalifanyia kazi,” amejibu Waitara.
Leave a comment