Akizungumza bungeni leo Jumanne, Bungala alisema, ni jambo la kusikitisha kuona serikali inaruhusu viwanda vya nyavu vinatengeneza bidhaa hiyo yenye matundu madogo na kuziuza kwa wananchi na kisha serikali kukusanya kodi.
“Mimi sielewi serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Siielewi kabisa. Yaani mimi binafsi, jamni siielewi serikali ya Rais John Pombe Magufuli. Inaruhusu viwanda vya nyavu kutengeneza nyavu zenye matundu madogo; na kisha inapokea kodi ya viwanda hivyo, lakini baadaye inashughulika na wavuvi. Siwaelewi,” alieleza Bungala.
Alisema, “Serikali ya CCM chini ya Rais Maguli, inatoa leseni kwa wavuvi, lakini ghafla inawageuka wavuvi hao hao wenye leseni na kuwanyang’anya nyavu zao na kisha kuwaita wavuvi haramu.”
Mbunge huyo ambaye anafahamika kwa jina la utani la Bwege alisema, “namtaka rais wa wanyonge, awaruhusu wavuvi hawa wa Kilwa Kusini na maeneo mengie, watumie nyavu zao, ili mradi wana leseni ya uvuvi. Maana kama wanyonge, basi wanyonge wenyewe ni wavuvi.”
Bungala alitoa kauli hiyo wakati akichangia hotuba ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi na Maliasili. Bunge limepanga kwa siku mzima ya leo, kujadili ripoti ya kamati hiyo na ile ya Kilimo, Maji na Mazingira.
Leave a comment