MBUNGE wa jimbo la Itilima, Njalu Silanga (CCM) amekataliwa kupewa usajili wa shule ya msingi Njalu iliyopo wilayani Itilima Mkoani Simiyu kwa sababu ya kutokidhi vigezo, anaandika Mwandishi wetu.
Usajili wa shule hiyo iliyojengwa na wananchi kwa kushirikiana na Mbunge Njalu Silanga wa jimbo la Itilima (CCM) umekataliwa na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako.
Profesa Ndalichako amesema shule hiyo haijakidhi vigezo vya usajili hivyo amekataa ombi la mbunge huyo kuisajili na kuagiza upungufu uliopo urekebishwe kwanza kabla ya wizara kuisajili shule hiyo ya umma.
Miongoni mwa upungufu huo ni kuwa na vyumba vitano pekee vya madarasa kati ya vinane vinavyohitajika.
Mengine ni matundu ya vyoo, ambayo kati ya 10 yanayohitajika, yapo matano pekee, huku ikiwa na chumba kimoja cha ofisi ya walimu.
Hata hivyo, Profesa Ndalichako amesema wizara itatoa mifuko 100 ya saruji kusaidia kuondoa upungufu uliopo.
“Tumeona kuna upungufu hatutaweza kutoa kibali cha kuisajili, badala yake mkamilishe yanayohitajika kwa utaratibu wa kisheria wa kufungua shule. Niwahakikishie kuwa, Wizara ya Elimu hatuna urasimu ni lazima tuwe makini kwa kusimamia vigezo hivyo,” amesema Profesa Ndalichako.
Amesema licha ya kuwapo kwa mahitaji ya shule katika eneo hilo ambalo lina wanafunzi wapatao 633, ni lazima kuzingatia vigezo ambavyo vitakaguliwa na wataalamu kutoka idara ya udhibiti ubora wa elimu na ofisi ya ofisa elimu wilaya.
Silanga alimwomba Waziri Ndalichako kuwapatia usajili wakati wakiendelea kushughulikia upungufu uliojitokeza kwa kipindi cha muda mfupi kabla ya shule kufunguliwa Januari 8 mwakani ombi ambalo hata hivyo, lilikataliwa.
Leave a comment