FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anatarajia kuongoza kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, cha kuteua wagombea wa nafasi mbalimbali za mabaraza. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Mabaraza hayo ni pamoja na Baraza la Wazee Chadema (Bazecha), Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) na Baraza la Vijana Chadema (Bavicha).
Taarifa iliyotolewa Tumaini Makene, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema tarehe 6 Desemba 2019, inaeleza kikao hicho kitaketi kwa siku moja (Jumamosi) kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
“Kamati Kuu ya chama itakutana kwa siku moja katika kikao chake cha kikatiba ambapo agenda kuu, itakuwa uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi wa mabaraza ya chama. Kikao hicho kitakuwa chini ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mbowe,” inaeleza taarifa ya Makene.
Taarifa hiyo imeeleza zaidi kuwa, baada ya kikao hicho kuketi, Chadema itatoa taarifa kwa umma kuhusu majina ya watakaoteuliwa kuendelea na mchakato wa uchaguzi.
Chadema inatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wake wa kitaifa tarehe 18 Desemba 2019. Ambapo kwa sasa, uchaguzi wa viongozi wa chama hicho wa kanda, umeshafanyika.
Leave a comment