January 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe aruhusiwa kutoka hospitalini

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

FREEMAN Mbowe, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Aga Khani jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alilazwa Hospitalini hapo tangu Jumanne tarehe 9 Juni 2020 akitokea Hospitali ya DCMCT Ntyuka jijini Dodoma.

Mbowe alifikishwa DCMCT baada ya kudaiwa kushambuliwa na watu wasiojulikana akiwa anapandisha ngazi nyumbani kwake Area D Dodoma usiku wa kuamkia Jumanne ya tarehe 9 Juni 2020.

Inadaiwa, watu hao walimkanyanga kanyanga mguu wake wa kulia na kuuvunja.

Leo Jumamosi tarehe 13 Juni 2020, Tumain Makene, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, ametoa taarifa kwa umma alisema, Mbowe ameruhusiwa kutoka Hospitalini saa 10:30 jioni.

“Ripoti ya matibabu yake inaonesha ataendelea kupata matibabu na uangalizi wa karibu akiwa nyumbani hadi hali yake itakapoimarika kabisa na kupona,” amesema Makene

“Chama na familia kinapenda kutoa shukrani kwa madaktari, wauguzi, wa DCMC, Dodoma na Aghakhan, Dar es Salaam. Aidha, tunawashukuru madereva, marubani, wauguzi na wote waliosaidia kumsafirisha majeruhi kutoka DCMC hadi Aghakahan,” amesema

Makene amesema, shukran pia ziwaendee baadhi ya wabunge, viongozi wa chama, baadhi ya biongozi wa Serikali, wapenzi, wanachama wa Chadema na Watanzania wote wenye mapenzi mema kwa Salaam, Sala na misaada mbalimbali waliyotoa na kuhudumu kwa kipindi chote tangu Mbowe aliposhambuliwa.

“Shukrani za kipekee ziwafikie Mabalozi wote wa nchi mbalimbali, pamoja na asasi mbalimbali zilizotoa salaam za pole na kulaani shambulio hilo huku wakitaka uchunguzi wa haki na wa haraka ili kuwabaini wahalifu “wasiojulikana” waliohusika na kuwachukulia hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Katika taarifa hiyo ya Chadema imesema,”Chama na familia kimesikitishwa sana na kauli na taarifa mbalimbali za upotoshaji, kudukua, kugushi, nia mbaya na uongo zilizotolewa kwa nyakati tofauti na watu mbalimbali, zikiwemo za Spika wa Bunge, baadhi ya Wabunge wa CCM (na washirika wao) na Jeshi la Polisi kupitia kwa Msemaji wake David Misime kuhusu tukio hili.”

“Tumekwazwa na juhudi kubwa za kujaribu kulinda uhalifu na hata kuzuia Uhuru wa vyombo vya habari kuhusiana na kadhia hii,” amesema

Amesema pamoja na kauli mbalimbali za viongozi za chama kutolewa, katika wakati mwafaka, Chama kupitia mkutano na waandishi wa habari, kitaeleza, kufafanua na kutoa taarifa za kweli na kina kuhusu tukio zima la kuvamiwa, kushambuliwa, kujeruhiwa na kutibiwa kwa Mbowe.

Jana Ijumaa, Jeshi la Polisi Tanzania, lilitoa taarifa za uchunguzi wa awali wa tukio hilo ambapo lilieleza kwamba Mbowe alifikishwa hospitalini akiwa amelewa chakari.

Taarifa hiyo ilitolewa na David Misime, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania ambaye alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

“Napenda kujulisha Jeshi la Polisi limeendelea kufanya upelelezi wa kina kuanzia kwa mhanga mwenyewe wa tukio ambaye alidai muda wa saa saba hivi usiku akiwa kwenye ngazi ya kuingia nyumbani kwake, akiwa anatokea kwa mzazi mwenzake aitwaye Joyce Mukya Mbunge wa Viti Maalum Chadema anayeishi eneo la Medeli jijini Dodoma, alishambuliwa na kuumia kwenye mguu wa kulia.”

“Mhanga wa tukio alidai, wakati anashambuliwa alipiga kelele nyingi kuomba msaada ambao aliupata toka kwa dereva wake ambaye naye alipiga simu kwa Joyce Nkya kumjulisha tukio.”

Taarifa hiyo ya Polisi inasema, “upelelezi wetu umepata ushahidi wa kutosha kutoka kwenye eneo la tukio unaonesha kulikuwa na watu ambao kwa namna yoyote wangeweza kusikia makelele yaliyopigwa na Mbowe kuomba msaada, na wengine walikuwa na uwezo wa kuona bila kizuizi kitendo cha kushambuliwa.”

Alisema, hata hivyo, kwa mujibu wa mashahidi hawa, hakuna hata mmoja aliyeweza kusikia kelele hizo au kuona Mbowe akishambuliwa.

“Kwa mantiki hiyo, ushahidi pekee unaozungumzia kushambuliwa ni maelezo ya mhanga wa tukio (Mbowe) pamoja na dereva wake ambayo kwa hali ilivyo sasa yanatia shaka kuhusu ukweli wa tukio hili,” alisema

Akihitimisha taarifa yake, Misime alisema, “tunaendelea na uchunguzi kutafuta ukweli wa tukio hili, hivyo tunaomba wananchi wote wenye taarifa zitakazoweza kusaidia upelelezi huu wazilete kwetu.”

error: Content is protected !!