Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lowassa ameniumiza – Mbowe
Habari za SiasaTangulizi

Lowassa ameniumiza – Mbowe

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesikitishwa na hatua ya “waziri mkuu mstaafu,” Edward Lowassa, kukihama chama hicho. Anaripoti Hamisi Mguta … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, tarehe 14 Machi, mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, amesema kuwa kitendo cha Lowassa kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemsikitisha yeye binafsi, chama chake na kimedhoofisha upinzani kwa ujumla.

Alisema, “niseme ukweli, nilipopata taarifa kuwa Lowassa amekihama Chadema na kurejea CCM, nilisikitika sana. Nikisema nilifurahi, hapana. Nitakuwa muongo. Kuondoka kwake, kumepunguza kwa kiasi fulani nguvu yetu katika kukabiliana na CCM.”

Amesema, “siyo kwamba tutadhoofika moja kwa moja kwa moja. Hapana. Tutayumba, lakini tutarejea kwenye uimara wetu.”

Lowassa, ambaye alikuwa mgombea urais wa vyama vinne vya upinzani katika uchaguzi mkuu uliyopita chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), alirejea CCM 1 Machi mwaka huu.

Alipokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano na ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho, Dk. John Magufuli.

Hata hivyo, Mbowe amesema, kazi ya Chadema ni kupigania haki na demokrasia; kazi ambayo inahitaji kujitoa. Hivyo basi, kama kuna mtu yeyote anaona wajibu huo ni mzito kwake, ni bora akajiweka pembeni, kama ambavyo Lowassa amefanya.

Alisema, “kazi ya kupinga uovu, kuhubiri haki na yaliyo mema na kulaani yasiyo haki, siyo kazi rahisi. Ni kazi inayohitaji kujitoa sana. Unapoona maovu, lakini ukashindwa kuyakemea, unapoona watu wanagongwa bila sababu usikemee, unapoona watu wanapigwa risasi ukakaa kimyaa, ni bora ukishindwa kulia na sisi usiwe na sisi.”

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa upinzani bungeni ameeleza kuwa wapo watu  alioanza nao waliishia katikati na wale aliowakuta katikati wakashindwa hivyo haoni ajabu kwa Lowassa kuondoka.

“…wapo tulioanza nao, wakashindwa katikati. Wapo tuliowakuta katikati, wakashindwa pia. Hivyo mtu yeyote ambaye anaona wajibu huu ni mzito kwake, ni bora asiwepo kuliko kuwapo nusu huku, nusu kule,” amesisitiza.

Amesema, vyama vyote vinakusanya watu kwa mahitaji maalumu na kwamba watu hao wanakuwa pia na malengo yao, ndiyo maana wanaingia na kuondoka.

Aidha, Mbowe ametumia nafasi hiyo kumtuma ujumbe kwa Lowassa, kwamba akishauri CCM kusimamia haki za raia.

“Naomba Lowassa akawaambie ukweli chama chake, kisiwatese Watanzania na wala chama hiki hakitamwaga damu. Chama cha siasa kama dodoki ukiliweka kwenye maji machafu litanyonya, ukiliweka kwenye maji masafi litanyonya,” amefafanua.

Kauli ya Mbowe kuwa Lowassa akishauri chama chake hicho alichorejea, inashahibiana kwa kiwango kikubwa na kile ambacho Rais Magufuli alimshauri Lowassa kukiambia Chadema.

Magufuli alisema, ikiwa chama hicho, kitaendelea na siasa zake za kiharakati, basi viongozi wake wakuu, watajikuta matatani. Lowassa alitekeleza ushauri huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

error: Content is protected !!