Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Maulid Mtulia asotulia kivita
Makala & Uchambuzi

Maulid Mtulia asotulia kivita

Spread the love

MAULID Said Mtulia, mwanasiasa kijana aliyejiuzulu ubunge ghafla, na kuhamia CCM hivyo kusababisha fadhaa upande wa upinzani, anaweza kutangazwa mshindi tena katika uchaguzi mdogo. Anaripoti Jabir Idrissa … (endelea).

Mfumo wa uchaguzi ambao unadhibitiwa na dola, unaweza kumpenyeza akarudi bungeni. Lakini, ushindi wake hautazamiwi kuwa uliotokana na kura za wananchi.

Tangazo lake la tarehe 2 Disemba mwaka jana la kujivua uanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), kilichompitisha kugombea nafasi hiyo kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, limeibua mjadala mrefu ndani ya jimbo la Kinondoni – achilia mbali nchini kote – ambao sasa unaonekana kumuonesha kama mwanasiasa asiyeaminika tena.

Ufuatiliaji wa mijadala ya suala hili kwenye mitaa tangu hapo, unamnyima alama za uwezekano wa kuungwa mkono mara ya pili hasa kwa kuwa amehamia kwa watawala walioshika madaraka kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho mvuto wake mbele ya umma unazidi kuonekana unaopotea kwa kasi siku hadi siku.

Alipoingia ulingoni kwa mara ya kwanza baada ya CUF kunufaika na mgao wa makubaliano kusimamisha mgombea jimbo la Kinondoni, Mtulia alipanda chati haraka.

Kuwa kwake mwanasiasa kinda na akisimama upande wa chama kinachojulikana kuamini katika mabadiliko ya kweli, kulimbeba.

Bali na ule ukweli kwamba kugombea kupitia chama hicho kulimaanisha ndio chaguo la wapenda mabadiliko dhidi ya CCM, kulimuongezea mvuto kwa watu.

Mtulia hakuathirika hata chembe na kutokuwa mkakamavu jukwaani. Kampeni yake ilivutia umma kwa sababu wanajimbo waliamini ndiye chaguo lao kupitia mwamvuli wa umoja wa upinzani uliopewa jina la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Mpaka leo unapoandaliwa uchaguzi mdogo, wengi wanaamini Mtulia alipigiwa kura na hata waliobeba kadi ya kijani – kadi ya CCM.

Kwenye maskani za wananchi wakiwemo vijana wenzake, kunasemwa sana kwamba Mtulia alinufaika na mgawanyiko uliogubika CCM wakati ule baada ya wananchi kuchokwa na aliyekuwa anataka ubunge mara ya pili kutokea upande huo, Iddi Mohamed Azzan. Wapo wanaoamini kuwa aliponzwa na kauli zake baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa 2010.

Viongozi wenzake katika CCM walijumuika naye kutosoma alama za nyakati kwa kumpa tena kijiti atetee kiti.

Ni hatua iliyozaa simanzi kubwa fikirani mwa wananchi; na kwa bahati mbaya jitihada za kuziba ufa ikiwemo kugawia fedha vijana ili wamuunge mkono kwa kumpigia kura Azzan, hazikufua dafu.

Walimkataa. Azzan alipigwa kumbo katika matokeo yaliyocheleweshwa kwa siku mbili ikiaminika kuwa wakubwa wakitaka kulazimisha atangazwe mbunge mteule.

Eneo la kujumlisha kura na kutangaza matokeo liligeuka uwanja wa vita, likijaa wananchi waliokuwa wamekusanyika kutaka haki yao ya kutangaziwa mbunge waliyemchagua, huku wakiangaliana na wanaulinzi na usalama waliowekwa tayari kwa kila hali kukabiliana na nguvu ya umma mara tu amri ya kuwadhibiti itakapokuwa imetolewa.

Nguvu ya umoja wa upinzani wakiwemo pia wafuasi na viongozi wa vyama vya NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD), ilionekana dhahiri kuogofya watawala na matakwa yao.

Mtulia akiwa chini ya ubavu wa viongozi shupavu wa vyama hivyo shirika pamoja na wabunge wateule wa majimbo ya Kawe (Halima Mdee), Ubungo (Saed Kubenea), Kibamba (John Mnyika), Temeke (Abdalla Mtolea), Ukonga (Mwita Waitara) pamoja na madiwani waliochaguliwa kupitia UKAWA, alitangazwa mshindi baada ya saa 48.

Ni ushindi wa kihistoria kwa upinzani kufanikiwa kwa mara ya kwanza kubeba kiti hicho tangu uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia chini ya mfumo wa vyama vingi uliopigwa Oktoba 1995.

Hakuna matunda ya kupigiwa mfano ya ubunge wa Mtulia. Sababu zaweza kuwa nyingi. Lakini ya kutokuwa mkakamavu wa kuongoza wananchi kimaendeleo, inapewa uzito zaidi. Anachukuliwa kama aliye tofauti na wabunge wa upinzani wenzake hao. Walijitahidi kuhangaikia maendeleo japokuwa ndani ya kutopendeza kwa washika utawala.

Ukweli huo waweza kupuuzwa na wananchi. Kwamba mtazamo mpya wa kisera juu ya siasa za ushindani chini ya dola inayoshikwa na CCM, umegeuka adui wa maendeleo ya umma wote, bali maeneo ya majimbo wayashikayo CCM.

Hatua ya Mtulia kuhama kambi ya upinzani kwa alichokieleza kumuunga mkono Rais John Magufuli anayemuona anafanikisha hata yale yaliyokuwa kiu ya upinzani, ndiyo hasa inayomchongea.

Mtulia anatajwa kama msaliti kisiasa mbele ya umma. Hatua aliyoichukua ya kujiuzulu ubunge na kuhamia CCM, imelazimisha wananchi kupigakura mara ya pili ndani ya kipindi cha miaka miwili huku akijua hali ya kisiasa imekuwa ngumu kutokana na sera zinazominya uhuru wa kujieleza na ushiriki katika siasa.

Tena akiwa hakukisaidia chama cha CUF kilichompitisha kugombea ambacho kinatafunwa na mgogoro wa kutengenezwa baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kulazimisha kurudi mamlakani licha ya kujiuzulu mwenyewe uenyekiti karibu na kampeni ya uchaguzi mkuu 2015, Mtulia haionekani kama ametulia kivita.

Jibu la mwelekeo wa mijadala ndani ya mitaa ya jimbo, linamaanisha kitu kimoja tu – jina lake halisomeki kirahisi leo, tofauti na vile ilivyokuwa Oktoba 2015. Na mgawanyiko ndani ya CCM wenyewe unachangia kumjengea jabali asivuke salama.

Pale Mkwajuni, makaoni pa CCM Wilaya ya Kinondoni, panasemwa kuwa ukaribu wake na Azzan unazidi kuachana hasa kwa kuwa naye aliingia kilingeni atake kuteuliwa kugombea. Azzan pamoja na Abbas Tarimba wanatajwa kama makada wenye nguvu jimboni.

Wakati uzinduzi wa kampeni ukianza kwa ajili ya uchaguzi utakaofanyika tarehe 17 Februari, pamoja na ule wa kujaza kiti cha jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro ambako pia mbunge Dk. Godwin Mollel wa Chadema alijivua uanachama na kuhamia CCM, mvuto umegeukia kwa jina la Salum Juma Mwalimu, mwanasiasa mwingine kijana aliyejipatia umaarufu kama mwanasiasa mkakamavu na muadilifu.

Mwalimu ameteuliwa na Chadema, lakini anabeba umoja wa UKAWA. Naibu Katibu Mkuu huyu wa chama hicho upande wa Zanzibar, anatarajiwa kung’ara kwenye kampeni na hatimaye kurudisha imani ya wananchi juu ya upinzani.

Amepata bahati ya kusindikizwa na wajumbe wa kamati kuu ambao pia ni mawaziri wakuu wastaafu waliohama CCM baada ya majina yao kukatwa katika kugombea uteuzi wa kugombea urais mwaka 2015.

Natabiri kwamba iwapo dhamira ya kulazimisha Mtulia awe mbunge tena itatimia, basi itakuwa ndani ya machungu makubwa ya mgawanyiko wa jamii jimboni; maana umoja wa upinzani hautakuwa umejiachia kushuhudia hilo likitokea machoni pao.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!