HAJI Manara, Msemaji wa Klabu ya Simba na wenzake watatu, tarehe 6 Agosti 2019 wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kudaiwa Sh. 83.5 milioni. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).
Msemaji huyo na wenzake (Beatrice Ndungu na Palm General Supply), wamefikisha kwenye Mahakama ya Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakidaiwa kupokea bidhaa zenye nembo ya Dela Boss bila kufanya malipo yoyote.
Mlalamikaji ni Abu Masoud Al Jahdhamy LLC ambaye anaiomba mahakama kumwamuru Manara na wenzake kumlipa fedha hizo, fidia pamoja na gharama ambazo anamlipa wakili wake.
Abu Masoud ameeleza, kwamba aliwasambazia bidhaa (pafyumu) walalamikiwa zenye nembo ya Dela Boss ambazo zilitengenezwa Dubai akitarajia malipo.
Katika madai hayo namba 128/2019, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Wanjah Hamza mlalamikaji aliingia mkataba na Manara tarehe 19 Desemba 2018 kwa ajili ya kuchapa bidhaa zenye maneno hayo.
Na kwamba, mkataba huo ulieleza kuwa mlalamikaji atachukua asilimia 70 na Manara asilimia 30. Hata hivyo, mkataba huo umeeleza, faida itakayopatikana itafanywa marejesho kwenye mtaji wa mlalamikaji.
Kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa tena tarehe 29 Agosti 2019.
Leave a comment