Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Mamia wamzika mpigapicha wa waziri mkuu Tanzania
Habari Mchanganyiko

Mamia wamzika mpigapicha wa waziri mkuu Tanzania

Spread the love

MKUU wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Tom Apson ameongoza mazishi ya Chris Mfinanga, aliyekuwa mpigapicha wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yaliyofanyika kwenya kijiji cha Mangio, Vuchama, wilayani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza na waombolezaji kijijini hapo jana Jumatano, tarehe 3 Juni 2020, Mkuu huyo wa Wilaya ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwira alisema Chris Mfinanga alikuwa mtu aliyejaa upendo ndiyo maana wengi wanahuzunishwa na kifo chake.

“Chris alikuwa mtu mcheshi na mwenye upendo, alisaidia wengi lakini tusisahau kwamba Mungu ndiye mtoa riziki. Msikate tamaa kwa sababu Mungu yupo na alimwezesha Chris na ndiyo maana aliweza kuwasaidia wengine na hata kuwasomesha watoto wenu,” alisema.

“Ninawasihi muamini kuwa Yesu yupo na kwake kuna faraja. Amini Yesu yupo na usiamini katika mganga wa kienyeji au ushirikina. Tuache ramli, tumtegemee Mungu nasi tutapata faraja,” alisisitiza.

Mapema, akiongoza ibada hiyo, Mchungaji Kiongozi wa KKKT Usharika wa Vuchama, Bill Graham Msangi aliwataka waombolezaji waweke mambo yao sawa na Mungu wao pamoja na majirani wanaoishi nao.

Akitoa mahubiri kutoka kitabu cha Ufunuo wa Yohana (14:13), Mchungaji Msangi alisema watu wanaomwamini Kristo wana heri kwa sababu wanapoaga dunia ni sawa na watu wanaoenda kupumzika baada ya taabu zao hapa duniani. “Wanaokufa katika Bwana wanaenda kupumzika baada ya taabu zao. Wana heri sababu matendo yao yanafuatana nao.”

“Kama wewe ni mchawi au mpiga ramli na kazi yako ni kuchonganisha watu, au wewe ni kibaka au mfitini, je hayo matendo yako utaenda nayo wapi? Kule kwenye pumziko siyo kwao watu wa aina hiyo,” alisema.

“Neno la Mungu limesema; bali wao wasioamini, waongo wote, wachukiao na wezi wote na waabuduo sanamu, sehemu yao ni kwenye ziwa la moto ambao hata mende hawaungui. Hata uwe tajiri kiasi gani, au uwe mzuri kiasi gani au uwe baunsa, hautaweza kuzuia kuingia kwenye jehanamu ya moto eti kwa sababu ya ubaunsa wako.”

“Tunapaswa tujiandae kwa sababu siku ikifika, Mungu haatangalia uzuri ulionao. Yeye Mungu ni mzuri kuliko huo uzuri wako. Shetani alikuwa mzuri sana lakini alipoasi alifukuzwa.”

Aliwasihi wafiwa na wakazi wa kijiji hicho hao wawe na umoja ili amani iweze kutawala.   “Umoja ukae miongoni mwa familia, ukae miongoni mwa kaya nyingine na wanavijiji wote. Tukiishi kwa namna hiyo, amani itatawala kwa sehemu kubwa.”

Naye Padre Japhet Njaule wa Parokia ya Vuchama ambaye aliongoza mazishi ya Baba yake Chris tarehe 21 Mei, 2020, aliwataka waombolezaji wamtumaini Mungu na waishi kwa kujiandaa na kuwa tayari wakati wote.

“Sisi sote ni mali ya Bwana. Tuishi leo na sasa kana kwamba ni saa hii tunaondoka na wala tusiwaze kuhusu kesho yetu. Tukumbuke kuwa Mungu ana mpango na maisha ya kila mmoja wetu,” alisisitiza.

Akizungumzakwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Fadhili Liwaka aliwataka wanafamilia wapate faraja kutoka kwa Mungu na wala wasiumizwe na msiba wa Chris.

“Tusione ajabu ya msiba huu kwa sababu hili ni jaribu la moto na Mungu anatukumbusha juu ya kuzaliwa, kuishi na kufa. Hakuna binadamu ambaye anaweza kukwepa kifo na hakuna mahali mapenzi ya mwanadamu yanaweza kuzuia kifo cha yule unayempenda,” alisema

Alisema, “Msiba unapotokea, unatukumbusha kuwa tutarejea kwa Mungu, pia utakuja kutuunganisha kama ndugu na kutujulisha kuwa hii neema ya Mungu na si jambo la kibinadamu na tatu unatukumbusha juu ya kujenga, amani, utulivu na kukubaliana na matokeo.”

Naye Baba mdogo wa marehemu, Alhaj Mzee Yusufu Mfinanga aliwashukuru madaktari na wauguzi waliomhudumia Christopher wakati akipatiwa matibabu.

Pia, aliwashukuru ndugu, jamaa, marafiki, majirani na wafanyakazi wenzake kwa ushirikiano mkubwa waliounesha. “Ushirikiano huo ni dalili tosha kwamba Christopher alikuwa akiishi vizuri na watu.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari Mchanganyiko

Mume auwa mke kwa kumchoma visu, ajisalimisha Polisi

Spread the loveJACKSON Kalamji (49), anashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza,...

error: Content is protected !!