January 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Malalamiko wizi wa data, vifurushi yatua Serikalini

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imeagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuchunguza madai ya wananchi kuhusu wizi wa data na vifurushi, unaodaiwa kufanywa na baadhi ya kampuni za simu nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Agizo hilo limetolewa leo tarehe 23 Desemba 2020 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile, alipotembelea Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano la TCRA (CCC) jijini Dar es Salaam.

Dk. Ndugulile ameitaka TCRA kupitia baraza hilo, kuyafanyia kazi malalamiko hayo ya wananchi kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.

Waziri huyo wa mawasiliano ameagiza CCC kutoa takwimu za malalamiko hayo kila baada ya miezi mitatu, sambamba na idadi ya malalamiko yaliyotafutiwa utatuzi.
“Hatutaki kufanya kazi kwa mazoea, nitawapima kwa matokeo na sio michakato, tutakwenda kwa mwendo wa takwimu na kila baada ya miezi mitatu tupate taarifa ya malalamiko mangapi yamepokelewa,” ameagiza Dk. Ndugulile.

Dk. Ndugulile amesema “Mangapi yamefanyiwa kazi, mangapi yameisha na kwa nini mengine hayajaisha kwa kuwa haya ni mambo ya msingi ambayo tunatakiwa tuyaangalie na tuwe taasisi ya kutatua changamoto za wananchi.”

Dk. Faustine Ndugulile, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Dk. Ndugulile amesema baadhi ya wananchi wanatoa malalamiko kuhusu huduma wanazopata kwenye mitandao ya simu.

Miongoni mwa malalamiko hayo ni, vifurushi vyao kuisha kabla ya muda, kubadilishiwa gharama za matumizi ya vifurushi, kupunjwa vifurushi na fedha wanazotuma kwa njia ya mtandao.

Dk. Ndugulile amesema malalamiko yote hayo yanahitaji kutafutiwa ufumbuzi.

Waziri huyo wa mawasiliano Tanzania, ameagiza TCRA iweke mifumo ya kulinda watumiaji na walaji wa huduma za mawasiliano na bidhaa za Teknolojia, Habari na Mawasiliano( TEHAMA) na taarifa zao za siri.

“Kwa kuwa sekta hii inaendelea kukua na watu wanatumia biashara mtandao na hawaendi madukani, tumieni lugha nyepesi kuelimisha wananchi namna ya kutumia huduma na bidhaa za TEHAMA. Na muwe na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa baraza ili kutekeleza sheria ya TCRA iliyounda baraza hilo,” ameagiza Dk. Ndugulile.

Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Andrea Mathew ameitaka TCRA kupitia CCC itoe elimu juu ya matumizi ya vifurushi ili kuondoa mkanganyiko juu ya gharama na viwnago vya vifurushi hivyo.

“TCRA na CCC ni taasisi zilizo chini ya Wizara na moja inashughulika na watoa huduma na nyingine watumiaji wa huduma, ambapo ni rahisi kufanya nao kazi na kuishauri Wizara katika kutatua malalamiko ya wananchi,” amesema Mhanidisi Mathew na kuongeza:

“ Kwa kuwa mwananchi anaweza kulalamika kuwa ameibiwa bando kumbe akielemishwa atafahamu vizuri kwanini bando limeisha na hii itawafanya wananchi wavutiwe zaidi kutumia huduma za mawasiliano na hatimaye tutachangia pato la Taifa.”

Katibu Mtendaji wa TCRA-CCC, Mary Shao Msuya amesema baraza hilo limejipanga kushughulikia maelekezo yaliyotolewa kwa kuwa watumiaji wa huduma na bidhaa za TEHAMA wameongezeka tofauti na mwaka 2003.

Msuya amesema wakati baraza hilo linaanzishwa kulikuwa na huduma chache ya kupiga na kupokea simu na za vifurushi tu. Na kwamba hivi sasa kuna huduma nyingi ikiwemo za kutuma na kupokea pesa.

error: Content is protected !!