Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa: Anayeitaka fedha, ataipata shambani
Habari za Siasa

Majaliwa: Anayeitaka fedha, ataipata shambani

Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka vijana wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi waache kukaa vijiweni na badala yake waanzishe bustani ili kujiongezea kipato. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

“Biashara ya bustani inalipa sana, yeyote anayetaka fedha, ataipata shambani. Nataka niwasisitize sana twende tukalime, twende shambani.”“Shamba siyo lazima ulime mahindi, mpunga pekee ama muhogo. Bustani ya nyanya, vitunguu, karoti na mchicha inalipa sana,” amesem

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu imesema Majaliwa ametoa wito huo leo Jumamosi tarehe 18 Julai 2020 wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namahema alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa soko la mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu unaolenga kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo.

Amesema Serikali imetoa Sh.600 milioni ili zijenge masoko na kuongeza uzalishaji huko Mpumbe, Mnindu, Chiepo na Chikalala.

“Serikali imewaandalia mradi huu ili mlime wakati wote, iwe masika au kiangazi. Rais wetu ametoa fedha hizi ili vijana na akinamama walime bustani na kujipatia kipato zaidi,” amesema.

Katika hatua nyingine, waziri mkuu ameagiza kamati ya ujenzi ya mradi huo irekebishe mara moja kasoro zilizosababishwa na ukiukaji wa taratibu wa ujenzi wa majengo ya Serikali kwenye soko hilo.

Amemtaka msimamizi wa mradi huo, Kalistus Mnunduma ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Nkowe ahakikishe anatoboa milango ya ziada kwenye jengo ili kuongeza usalama wa watumiaji wakati wa kutoka na kuingia kwenye soko hilo.

Waziri mkuu alifikia hatua hiyo baada ya kubaini ujenzi wa soko hilo ulianza kwa kutumia michoro ya awali (sketch) badala ya kutumia ramani za ujenzi na matokeo yake wakajenga jengo lenye vyumba vya baridi vya kuhifadhia mazao, eneo la wazi la kupokelea mazao na kuweka mlango mmoja tu wa kuingilia na kutokea.

“Nimetoa maagizo manne. Kwanza, toboa milango, pili weka vizimba ili wananchi wauze bidhaa zao mahali pasafi, usiruhusu watu wauze bidhaa zao chini, siyo sawa kiafya.”

“Tatu, chimba visima, weka mnara, tanki na mipira ya kumwagilia ya kutosha ili wakulima wasipate taabu ya kusomba maji. Weka mashine ya kusukumia maji ili uweze kuyasambaza katika eneo kubwa. Nne, tenga eneo la kuuza bidhaa kwa rejereja ili wananchi wa hapa jirani wanufaike na mradi huu,” amesema.

Pia alimwagiza Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo, Harun Ibrahim Kiara ahakikishe wanatoa elimu ya kilimo cha bustani kwa vijana ili waanze na matuta machache.

“Pia anzisheni programu ya kukutana na vijana na akinamama na muwaeleze bonde la Mnindu linatumikaje kwa kilimo hicho,” amesema.

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Selemani Mrope alisema mradi huo unatarajiwa kutumia Sh. 127 milioni hadi kukamilika kwake na mpaka sasa wamekwishapokea Sh.50.8 milioni ambazo ni sawa na asilimia 40.

Alisema ujenzi wa soko ambao ulianza tarehe 25 Mei, 2020 ulikadiriwa kugharimu Sh. 25 milioni na mpaka sasa wameshatumia Sh.18.2 milioni ambapo ujenzi umefikia hatua ya uinuaji wa nguzo.

Mradi huo unatarajia kukamilika tarehe 30 Agosti, 2020.

Alisema Chuo cha Ufundi Stadi Mkowe kinatekeleza mradi wa kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo wa mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu kwa ufadhili wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia mfuko wa kuongeza na kuboresha elimu (SDF).

“Mradi huu umelenga kuwezesha kuwepo kwa soko la uhakika, ongezeko la ajira na uzalishaji, ongezeko la kipato kwa jamii, upatikanaji wa uhakika wa chakula lishe na uboreshiji wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya bustani,” alisema Mrope.

Alisema hadi sasa wamekamilisha kazi ya kuandaa mitala na miongozo ya kufundishia wakulima wote wa bustani kwa gharama ya Sh.4 milioni na kwamba wanaendelea na ukarabati wa darasa moja litakalotumika kutoa elimu kwa wakulima wote wa bustani ambalo gharama yake ni sh.4.2 milioni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Chadema yamtaka Rais Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

error: Content is protected !!