Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa akerwa wanaotafuta uongozi kwa rushwa
Habari za Siasa

Majaliwa akerwa wanaotafuta uongozi kwa rushwa

Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ihakikishe Watanzania hawarubuniwi ili watumie vizuri utashi wao wa kisiasa kuchagua viongozi bora. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

“Sote tunatambua kuwa Oktoba, mwaka huu Taifa letu litaendesha uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani…mna jukumu zito la kuhakikisha Watanzania hawarubuniwi na msimuonee au kumpendelea yeyote kwa maslahi yenu binafsi.”

Taarifa aliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu imesema Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Jumatano tarehe 12 Agosti 2020 alipofungua jengo la Intelijensia Takukuru Makao Makuu Dodoma.

Majaliwa aliwasihi watumie vizuri ofisi hiyo kukusanya taarifa muhimu za kiintelijensia zinazowahusu wagombea, vyama au wananchi watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi mkuu.

Waziri mkuu alisema, wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 na kwamba wanawajibu wa kuchagua Serikali bora na kiongozi bora atakayewaletea maendelea maendeleo.

“Chagueni kiongozi mwenye maono aliyetenda na atakayetenda,” alisema Majaliwa

“Tayari tumeshuhudia mking’ata baadhi ya wagombea waliojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye hatua za awali za uteuzi wa wagombea kupitia vyama vyao. Msiache; endeleeni kukaza uzi na kuwadhibiti wote wenye kujihusisha na vitendo hivyo,” alisisitiza.

“Niungane pia na Rais John Pombe Magufuli, kuwasihi wanasiasa na wagombea wenzangu wa nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu tuache kutumia rushwa kwa lengo la kununua uongozi.”

Waziri mkuu alisema, wanapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, ni vema Watanzania wote na viongozi wakazingatia nasaha za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika moja ya hotuba zake alipowataka wajiulize kwamba mgombea anayetumia rushwa kununua kura amepata wapi fedha hizo na je, akipata uongozi, fedha hizo atazirudishaje.

“Kwa hivyo, nasi ifike mahala tuwahoji hawa wanaotutia doa. Je, wewe mwenzetu unayetumia rushwa kununua uongozi umepata wapi fedha hizo? Na je? tukikuchagua, utarejesha vipi fedha hizo? Nitoe wito kwa Watanzania wote, msikubali kuwachagua wagombea wanaotumia rushwa ili kupata nafasi za uongozi,” alisema

Kadhalika, Majaliwa alitumia fursa hiyo, kuwapongeza viongozi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na watendaji wa Takukuru kwa kusimamia vyema mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ndani na nje ya Serikali.

Majaliwa alisema, hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa udhibiti wa matumizi ya hovyo ya fedha za umma; imeongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuziba mianya ya ukwepaji kodi.

Pia, waziri mkuu alisema, ni lazima wafanye uchunguzi wa kutosha juu ya matumizi ya fedha zote za umma na kujua kama matumizi hayo yanaenda sambamba na matakwa ya kisheria na pale ambapo watabaini ukiukwaji wa sheria wachukue hatua.

“Nyote mtakubaliana nami kuwa miongoni mwa mambo yaliyopewa uzito mkubwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Jemedari na Rais wetu mpendwa, John Pombe Magufuli ni kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.”

“Rais Magufuli amemudu kurejesha imani ya Watanzania kwa watumishi wa umma na zaidi ya yote amerejesha uwajibikaji. Ni ukweli usiopingika kwamba tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa kulikabili tatizo la rushwa na ufisadi ndani ya Taifa letu,” alisema

“Kwa upande mwingine, mafanikio tuliyoyapata hayajajikita katika kukabili mafisadi na wala rushwa tu, bali pia katika kuijengea uwezo wa kiutendaji Takukuru. Lengo ni kuiwezesha taasisi hii itekeleze majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Jengo hili tunalolifungua leo, ni kielelezo tosha cha baadhi ya jitihada hizo.”

Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na kitendo cha TAKUKURU kurejesha fedha na mali za wanyonge waliodhulumiwa mauzo ya mazao yao na kutozwa riba za kubambikiziwa na zisizolipika. “Hatua hiyo, imeudhihirishia umma kuwa TAKUKURU sasa inang’ata kwelikweli.”

“Kama mtakumbuka, operesheni ya urejeshaji wa fedha za wakulima zilizotokana na mauzo ya korosho na ufuta, ilianzia mkoani Lindi na baadaye kuhamia katika mikoa ya Mtwara, Pwani, Simiyu na hatimaye nchi nzima.”

Pia, Waziri Mkuu alisema Takukuru imewafuta machozi Watanzania wengi hususan wastaafu ambao kwa kutotambua haki zao, walikopa fedha kidogo kutoka kwa wajanja fulani fulani.

Alisema wajanja hao, wakatumia hila kupitia makubaliano ya taratibu za mikopo hiyo, kuwataka wakopaji warejesha kiasi kikubwa cha fedha kilichojumuisha riba ya zaidi ya asilimia 100. Jambo hilo, si tu ni kinyume na taratibu za ukopeshaji wa fedha bali pia ni uvunjanji wa sheria na ni uonevu mkubwa kwa wananchi.

Ufunguzi huo umehudhuliwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Brigedia Jenerali John Mbungo.

Wengine Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kicheere, Katibu Mkuu Ikulu, Dk. Moses Kusiluka, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge na maofisa wengine wa Serikali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!