Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa akagua ujenzi SGR, atoa maagizo kwa RC Pwani
Habari za Siasa

Majaliwa akagua ujenzi SGR, atoa maagizo kwa RC Pwani

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa wakati alipokagua ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Stesheni ya Dar es salaam hadi Ruvu mkoani Pwani
Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanznaia, Kassim Majaliwa, amekagua ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) akiridhishwa na kiwango na kasi ya maendeleo ya ujenzi huo ambao umefikia asilimia 87 kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea)

Amesema Serikali imedhamiria kuimarisha miundombinu ya usafiri wa reli, anga, maji na barabara ili kutoa fursa kwa wananchi kuchagua aina ya usafiri wanaohitaji kuutumia pia kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha biashara baina ya Tanzania na Mataifa mengine.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu leo Ijumaa tarehe 7, Agosti 2020 imesema Majaliwa alianza ziara hiyo kwa kukagua ujenzi wa jengo la stesheni ya Dar es Salaama ambalo linamuonekano wa madini ya Tanzanite.

Majaliwa amesema, ujenzi unaendelea vizuri na amemtaka mkandarasi akamilishe kwa wakati kwani Watanzania wanasubiri kwa hamu.

“Hii ni mara yangu ya tatu nafanya ukaguzi wa ujenzi wa mradi huu na wakati wote naridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake ambao unajengwa kwa kutumia fedha za Watanzania na asilimia 90 ya wafanyakazi wanaojenga mradi huu ni Watanzania,” amesema.

Waziri mkuu amesema, Watanzania waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imejipanga katika kuendelea na kuimarisha ujenzi wa miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla “na huu ndio utekelezaji wa maelekezo ya CCM iliyoyatoa kwa Serikali yake.”

Akiwa katika stesheni ya Ruvu mkoani Pwani, Majaliwa alipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi yakiwemo ya wakulima kunyanyaswa na wafugaji kwa kuingiza mifugo katika mashamba yao hivyo kuwafanya wakose chakula.

Pia, wananchi hao ambao baadhi yao maeneo yao yalitwaliwa kupisha ujenzi wa mradi wa SGR kwamba wamehamia kwenye maeneo ambayo hayana miundombinu ya maji. Kufuatia malalamiko hayo Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Pwani (RC), Mhandisi Evarist Ndikilo kesho Jumamosi aende na wataalamu wake wakasikilize kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema, mafanikio yanayoonekana katika mradi huo ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli.

Amesema tayari mkandarasi anayejenga mradi huo kampuni ya Yapi Merkezi ameanza kufanya majaribio ya kupitisha treni za kihandisi katika baadhi ya vipande vya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

“Mchakato wa manunuzi ya seti tano za mabehewa ya abiria unaendelea,” amesema

Mhandisi Nditiye amesema, licha ya ujenzi wa mradi wa SGR pia shirika la Reli linatekeleza mradi wa uboreshaji wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka na maboresho hayo yamefikia asilimia 93 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Tabora na unatarajiwa kukamilia Februari 2021.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa amesema, ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro unaendelea vizuri na umefikia asilimia 87.

“Hadi sasa mkandarasi amelipwa jumla ya hati za malipo 34 sawa na Sh.1.7 trilioni kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro. Mradi huo umetoa ajira zaidi ya 7,400 Dar es Salaam-Morogoro,” amesema.

Amesema kazi ya ujenzi inayoendelea kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro ni pamoja na ujenzi wa daraja kubwa lenye urefu wa kilimita 2.56, majengo ya stesheni za Dar es Salaam (85%), Pugu (99%), Soga (100%), Ruvu (95%), Ngerengere (93%), Morogoro (93%), eneo la karakana na mizigo Kwala (73%) na ujenzi wa madara 30 ambao umefikia (96%).

“Ujenzi wa tuta la reli umefikia asiliamia 91, ujenzi wa mfumo wa mawasiliano ukijumlisha ujenzi wa minara 28 ya mawasiliano umefikia asilimia 43, ujenzi wa umeme wa msongo kv 220 upo asilimia 99, ujenzi wa vivuko 55 vikiwemo 20 vya juu, 17 vya chini na 13 vya wanyama na vitano vya makutano ya reli ya SGR na MGR, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 92.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!