Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Majaliwa ahitimisha mkutano wa Bunge kwa kueleza mafanikio makubwa
Habari za Siasa

Majaliwa ahitimisha mkutano wa Bunge kwa kueleza mafanikio makubwa

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania
Spread the love

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli katika kipindi cha miaka mitano imepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kurekebisha nidhamu kwa watumishi wa umma na uwajibikaji Serikalini, hivyo kuwezesha watumishi kutambua majukumu yao na kuwatumikia Watanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea)

Amesema mambo mengi ya kujivunia yamefanywa na tumekuwa tukiyaeleza katika maeneo mengi kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, nyaraka mbalimbali, uwepo wa miradi mingi ya kimkakati hadi kwa wananchi wa kawaida, yakiwemo mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Serikali na nje ya Serikali ili kulinda mali na fedha za umma. “Hatua hii ni endelevu, lengo ni kung’oa mizizi ya rushwa nchini.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumatatu, tarehe 15 Juni 2020 Bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu imesema, Majaliwa ametaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, mhimili wa Bunge na Mahakama.

Akiorodhesha mafanikio hayo, Waziri Mkuu amesema, Serikali imefanikiwa katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ambayo yanalenga kujihakikishia kuwa na Taifa lenye nguvukazi inayofanya kazi na kwamba mapambano hayo bado yanaendelea nchini kote.

Waziri Mkuu amesema kuwa mafanikio mengine ni utambuzi wa watumishi hewa ambapo katika zoezi hilo wamepata mafanikio makubwa na kuokoa sh. bilioni 19.83 kwa kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo watumishi hewa 19,708 na wenye vyeti vya kugushi 15,411.

Amesema Serikali imefanikiwa katika suala la ukusanyaji wa mapato ulioiwezesha Serikali kujenga miradi na kutoa huduma muhimu.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Masanja Kadogosa, ndani ya treni inayotumia umeme alipokagua mradi wa reli ya kisasa ya SGR

“Ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka wastani wa Sh. 800 bilioni kwa mwezi mwaka 2015 hadi wastani wa Sh. 1.5 trilioni kwa mwezi katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020.”

“Tumefanikiwa kuimarisha uwekezaji kwa kujenga viwanda. Hadi Aprili 2020 jumla ya viwanda vipya 8,477 vikiwemo vidogo, vya kati na vikubwa vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuwezesha ongezeko la ajira za viwandani zipatazo 482,601.”

 Kadhalika, Waziri Mkuu amesema, Serikali imefanikiwa kuimarisha masoko na kilimo cha mazao makuu, kama korosho, pamba, chai, tumbaku, kahawa, michikichi na mkonge. Aidha, Serikali imeimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula.

Mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na kuimarisha ushirika wa kilimo na upatikanaji wa pembejeo pamoja na huduma za ugani ili kuwafanya wakulima kuzalisha kwa tija.

Amesema marekebisho ya Sheria ya madini yamefanyika sambamba na kuanzisha masoko ya madini 28 na vituo 12 vya ununuzi wa madini katika maeneo ya uchimbaji na hivyo kuongeza makusanyo ya Serikali, kupunguza biashara haramu na utoroshaji wa madini kwenda nje. Pia, Waziri Mkuu amesema kuanzia Machi hadi Septemba, 2019 jumla ya kilo za dhahabu 4,680.28 zenye thamani ya Sh. 432.49 bilioni zimezalishwa na Serikali imefanikiwa kukusanya Sh. 30.27 bilioni.

Vilevile, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imefanikiwa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma ambapo tayari Watumishi wapatao 15,361 wamehamia Dodoma na sasa fursa za uwekezaji zimeongezeka katika Jiji la Dodoma.

“Tumefanikiwa kuboresha miundombinu na taaluma ya sekta ya elimu kwa ngazi zote kuanzia awali hadi elimu ya juu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa madarasa, maktaba, maabara, nyumba za walimu na mabweni.”

“Kwa upande wa Sera ya Elimu bila ada tumetumia zaidi ya Sh. 20.8 bilioni kila mwezi kwa ajili ya fidia ya ada, posho ya madaraka kwa walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu kata kila mwezi tangu 2016 na tutaendelea. Hii imesaidia kuongeza uandikishaji na mahudhurio shuleni,” ameongeza.

Amesema mafanikio mengine ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na kuimarisha huduma za afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya, kujenga Hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na za Kitaifa, huduma za Madawa na Vifaa Tiba.

Waziri Mkuu amesema Serikali imejenga Zahanati 1,198 Vituo vya Afya 487, Hospitali za Wilaya 71, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10, na Hospitali za Kanda tatu za Kusini – Mtwara, Magharibi – Tabora na Kanda ya Ziwa – Burigi.

“Ujenzi wa miradi ya maji vijijini na mijini tumefikia asilimia 84 mijini na asilimia 70.1 vijijini. Pia tumefufua Shirika la Ndege kwa kununua ndege mpya 11, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege kwenye mikoa isiyo na viwanja vya ndege pamoja na ununuzi wa rada nne mpya za kuongoza ndege za kiraia zilizo Mwanza, Mbeya, Dar-es-Salaam na Kilimanjaro.”

Waziri Mkuu ametaja mafanikio mengine ni ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme (Mwalimu Nyerere Dam) utakaozalisha Mw 2,115 ambao kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 40, gharama za ujenzi huo ni sh. 6.5 trilioni.

Amesema usambazaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umefikia asilimia 80 ambapo hadi Aprili 2020 Sh. 2.27 trilioni zimetumika na kufanikisha jumla ya vijiji 9,112 kati ya 12,268 vya Tanzania Bara kuunganishwa na umeme kutoka vijiji 2,118 mwaka 2015.

Amesema ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kimataifa (SGR) wa kilomita 300 Dar-es-Salaam–Morogoro, umefikia asilimia 78 huku kipande cha Morogoro hadi Makutupora chenye urefu wa kilomita 422 mradi wake umefikia asilimia 30 ya kazi.

“Lengo ni kukamilisha mradi huu ifikapo Juni 2021 kwa gharama ya sh. trilioni 7.5,” amesema

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kwenye miradi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya zenye thamani ya zaidi ya Sh. 7.6 trilioni, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kujenga barabara ya njia nne kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19.2).

“Ujenzi wa madaraja: ujenzi wa daraja la juu la Mfugale (Dar es Salaam), daraja la Furahisha (Mwanza) na daraja la Magufuli (mto Kilombero) umekamilika; ujenzi wa barabara ya pete (Ubungo interchange) umefikia asilimia 77 kwa shilingi bilioni 247; Aidha,  ujenzi unaendelea kwa daraja la New Selander (Dar es Salaam) kwa Sh. 270 bilioni. Daraja la Kigongo- Busisi shilingi Bilioni 699.2”.

Kuhusu, ujenzi wa Bandari, Waziri Mkuu amesema uboreshaji na upanuzi wa bandari za Tanga, Dar-es-Salaam na Mtwara umegharimu zaidi ya Sh. 1.2 trilioni.

Pia, Waziri Mkuu amezungumzia ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria na ujenzi wa chelezo; ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama ambapo katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi Aprili, 2020 jumla ya Sh. 111.7 bilioni zimetumika.

Maabara mpya ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyopo Mabibo Dar es Salaam

Vilevile, Serikali imekamilisha ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo katika Ziwa Nyasa; na ukarabati wa meli ya mafuta ya MV Sangara katika Ziwa Tanganyika. Ujenzi wa vivuko vya MV Kigamboni, MV Pangani, Kigongo -Busisi, MV Sengerema na Nyamisati.

“Tumefanikiwa katika suala zima la urejeshaji na usimamizi wa mali za Ushirika zilizokuwa zimechukuliwa kinyume na utaratibu, kama NYANZA, SHIRECU, KNCU na Mamlaka ya Mkonge Tanzania. Pia tumeweza kusimamia maboresho kwenye sekta ya uvuvi na mifugo kwa kuvua na kufuga kisasa, kujenga viwanda na masoko yake.”

“Kwa namna ya pekee kabisa nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kutokana na fikra na uongozi makini katika ujenzi wa Taifa letu. Ni dhahiri kuwa maono yake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 na mipango ya Serikali, zimeleta mafanikio makubwa ambayo hivi sasa wote tunayaona.”

“…nyote mtakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Rais na Makamu wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawafikia Watanzania, wanawasikiliza na kutatua kero zao.”

Amesema lengo la ziara hizo, pamoja na mambo mengine lilikuwa ni kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ikiwemo kukagua miradi ya maendeleo; kuzungumza na watumishi na kuwafahamisha kuhusu falsafa ya Serikali ya awamu ya tano ya Hapa Kazi Tu.

Amesema ziara hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma. “Hivi sasa, wananchi wanapokwenda katika ofisi za umma wanapokewa, wanasikilizwa na kuhudumiwa vizuri. Aidha, usimamizi wa miradi ya maendeleo umeimarika sambamba na kuakisi thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwakyembe : Zanzibar waliongoza kutaka Serikali 2 za muungano

Spread the love  MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema mjadala wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

error: Content is protected !!