January 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Majaliwa achambuliwa bungeni, athibitishwa waziri mkuu

Spread the love

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limemthibitisha Mbunge wa Ruangwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Majaliwa amethibitishwa leo Alhamisi tarehe 12 Novemba 2020 bungeni jijini Dodoma, baada ya jina lake la kuteuliwa na Rais John Pombe Magufuli, kuwasilishwa bungeni mapema leo na mpambe wa Rais.

Majaliwa anakuwa waziri wa mkuu wa kumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kabla ya kuthibitishwa na Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi aliwasilisha azimio la Bunge la kumthibitisha Majaliwa kuwa Waziri Mkuu.

Baada ya wabunge wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumthibitisha, walichangia azimio lililotolewa na Profesa Kilangi kisha upigaji kura ukafanyika.

Akitangaza matokeo hayo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema, jumla ya kura zilizopigwa ni 350, “hakuna kura iliyoharibika. Kura ya hapana hakuna hata moja, zote 350 zimemthibitisha Kassim Majaliwa Majaliwa.”

Baada ya Bunge kumthibitisha, kilichobaki sasa ni Majaliwa kuapishwa na Rais Magufuli, shughuli ambayo bado haijafahamika itafanyika lini.

Kesho Ijumaa saa 3:00 asubuhi, Rais Magufuli, atalihutubia Bunge la 12 kwa mara ya kwanza lilipokutana tarehe 10 Novemba 2020 jijini Dodoma. 

 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi

Wabunge CCM walivyomwelezewa 

Awali, wakichangia azimio hilo, William Lukuvi, mbunge wa Isman akisema, Rais Magufuli, mambo mengine anayoyafanya unajiuliza “lakini anakuwa na baraza za Mungu. Alipomchagua Majaliwa kwa mara ya kwanza, kinyume kabisa na wengi walivyodhani, lakini wameendena, amemsaidia vizuri sana.”

“Magufuli amemtea Majaliwa katika miaka mitano, bila unafiki, Majaliwa katika miaka mitano ametenda mengi, katika ubinadamu ni mtu mzuri sana. Mimi nimekaa nae muda mrefu tangu akiwa naibu waziri, sijawahi kuona amekasirika,” amesema Lukuvi

“Ni mwenye upendo, mchakazi, hana majivuno. Tunaweza kusema mengi, lakini huyo baba ametendea katika mikoa na wilaya zote kwa miaka mitano akiwa waziri mkuu.”

“Amezunguka majimbo karibu asilimia 90 ya wabunge amefika kuwaombea kura. Majaliwa anatosha sana kuwa waziri mkuu,” amesema Lukuvi.

Kapteni mstaafu George Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini (CCM) amesema “ninawaomba wabunge wote, kura zote tumpigie Majaliwa. Mimi namfahamu vizuri, nimefanya nae kazi tawala za mikoa.”

“Hakuna mtu mstaarabu ninayemfahamu mimi, hajikwezi, anamsikiliza kila mtu, anatenda haki kwa kila mtu kama Kassim Majaliwa,” amesema Mkuchika

“Wale mlioko vyama mbali na CCM, lakini muda wote aliotuongoza hapa ndani, hakuweza kutubagua, tumpe kura, ni mtu msikivu sana,” amesema.

Wiliam Lukuvi, Mbunge wa Isimani

Naye Mbunge wa Mchinga (CCM), Salma Kikwete amesema, “ninashukuru Rais John Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri ambazo ameweza kusimamia Taifa letu la Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania inajua, Afrika inajua na dunia inajua jinsi Dk. Magufuli alivyosimamia.”

Salma ambaye ni mke wa Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema, anamfahamu Majaliwa kwa kazi zake zilizotukuna.

“Majaliwa ni mnyenyekevu, hajikwezi, ni mpole na si mpole tu bali unaendana na ushupavu mkubwa na huyu ndiye Majaliwa tunayemfahamu,” amesema Salma.

Wabunge wakimshangilia Kassim Majaliwa baada ya kutangazwa kuwa Waziri Mkuu

 

Kwa upande wake,  January Makamba, Mbunge wa Bumbuli (CCM) amesema, kumpigia kura nyingi Majaliwa, inaonyesha imani kwa Majaliwa na kura ya imani za burasa na hehima za Rais Magufuli.

“Nimwombe Mungu aendelee kuibariki nchi yetu, Rais wetu, Majaliwa na wasaidizi wote wa Rais atakaowateua siku zijazo, ili nchi yetu iendelee kuwa na amani kubwa,” amesema January

Naye, David Silinde, Mbunge wa Tunduma (CCM) amesema, “tumpongeze Rais Magufuli kwa kumrudisha Majaliwa kuwa waziri mkuu wetu.”

“Kassim Majaliwa anauwezo wa kusimamia maono ya Rais ya kubadilisha nchi yetu. Majaliwa ana uwezo wa kuiunganisha nchi yetu yote kupitia Bunge na kuifanya kazi ya Rais kuwa nyepesi katika miaka mingine mitano,” amesema Silinde

… nawashukuru sana

Mara baada ya kuthibitishwa, Majaliwa amepewa wasaa wa kuzungumza akianza kwa kutoa pongeza kwa wabunge na Rais Magufuli “kwa imani yake kubwa aliyonayo juu yangu na kuendelea kuniamini kwamba naweza kuendelea kuyafanya kwa miaka mitano ijayo.”

“Natambua Rais kwa mamlaka anayoyafanya, anaweza kumsikiliza Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa ushiriki wake katika kuridhia jina langu kuja hapa katika Bunge tukufu na kuungwa mkono,” amesema Majaliwa

Majaliwa amesema, yeye na familia yake “na wapiga kura wangu wa Ruangwa, tunamhakikishia kwamba matamanio yake, yaliyopelekea kutoa jina lake na kulileta hapa, mataminio yake na wabunge, niwahakikishie nitafanya kazi.”

Majaliwa amesema “namshukuru sana sana na Mungu amwongezee afya, busara ili aendelee kulitumikia Taifa hili na mimi kama msaidizi wake nitaendelea kumsaidia.”

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania

“Kupata kura asilimia 100 inainyesha hata wale wa vyama vingine rafiki, wamenipigia kura. Nitashirikiana na kila mmoja wetu, nitapita tena katika maeneo yenu, kuona shughuli za maendeleo mnazozisimamia na kukutana na wananchi wenu, katika majimbo ya CCM na ndugu zetu wa vyama rafiki na maendeleo hayana chama,” amesema Majaliwa

Majaliwa amesema “hapa ndani ya Bunge, nitapokea ushauri wenu, kutoka maeneo mbalimbali, nitaendelea kusikiliza yale mtakayotokana nayo kwa wananchi.” 

Waziri mkuu huyo amesema, mawaziri watakaoteuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli “tutawatumikia wabunge wote bila kuwabagua.”

Majaliwa aliyezaliwa tarehe 22 Desemba 1961 ambaye kitaaluma ni mwalimu, atahudumu nafasi hiyo kwa miaka mitano hadi 2025 akiwa waziri mkuu wa kumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majaliwa aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010 baada ya wananchi wa Jimbo la Ruangwa Mkoa wa Lindi walipomchagua katika uchaguzi mkuu wa wakati huo.

Rais wa wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete, alimteua kuwa naibu waziri, ofisi ya waziri mkuu-tawala za mikoa na serikali za mitaa (Tamisemi) kuanzia 2010-2015.

Mara baada ya uchaguzi mkuu kumalizika wa mwaka 2015 na Dk. Magufuli kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania tarehe 5 Novemba 2015, alifanya uteuzi wa waziri mkuu.

Uteuzi huo ulifanyika tarehe 19 Novemba 2015 na kuliwasilisha bungeni ambapo lilithibitishwa akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Mizengo Pinda.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu kwa taarifa na habari mbalimbali

error: Content is protected !!