January 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yaiamuru Halotel kulipa fidia Sh. 42 Bil.

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar Es Salaam, imeiamuru Kampuni ya Mwasiliano ya Halotel Tanzania, kulipa fidia Sh. 42 Bilioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam…(endelea).

Amri hiyo imetolewa na mahakama hiyo baada ya Kampuni ya Halotel Tanzania pamoja na Mkurugenzi wake, Son Nguyen na wenzake watano, kukutwa na hatia ya kuisababishia hasara zaidi ya Sh. 75 Bilioni, Mamlaka ya Mwasiliano nchini (TCRA).

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mameneja wa Halotel Tanzania, Nguyen Minh na Vu Tiep. Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasilia (Tehama), Ha Than. Mkurugenzi wa Fedha, Nguyen Cong na kampuni ya Viettel.

Katika hukumu hiyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapiga faini ya Sh. 24 Milioni washtakiwa hao sita au kwenda jela mwaka mmoja, baada ya kukiri mashtaka manne kati ya mashtaka 10 yaliyokuwa yanawakabili.

Vigogo hao wa Halotel Tanzania, walipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo mwezi Machi 2020 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakidaiwa kuongoza genge la uhalifu ili kujipatia faida kati ya tarehe 6 Juni 2017 na Machi 26, 2020 huko Mikocheni jijini humo.

Katika mashtaka hayo yaliyokuwa yanawakabili, washtakiwa hao walituhumiwa kutumia masafa ya redio katika maeneo mbalimbali Tanzania, bila kibali cha TCRA.

Hali kadhalika, washtakiwa hao walidaiwa kukwepa kulipa kodi kwa TCRA kupitia mitambo ya mawasiliano yaliyounganisha Kampuni ya Viettel Tanzania na Vietnam, kinyume na sheria na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh. 75 Bilioni.

Vile vile, washtakiwa hao walituhumiwa kutumia mitambo ya mtandao binafsi wa kidigitali -Virtual Private Network (VPN) kati ya tarehe 7 Julai 2016 na Machi 26 2020, na kuisababishia TCRA hasara ya Sh. 3.03 bilioni.

error: Content is protected !!