Mahakama Kuu yazuia ‘njama’ za Serikali

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), amegonga mwamba mahakamani. Ni baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, “kuzima” mkakati wake wa kuchelewesha kesi ya kupinga muswaada wa vyama vya siasa. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Jopo la majaji watatu wa mahakama kuu, wanaosikiliza kesi hiyo ya kikatiba, linaloongozwa na Jaji Barke Sahe, wameeleza mahakamani hapo kuwa suala lililopo mbele yake, “lina maslahi mapana kwa umma.”

Maelezo ya mahakama yamefuatia upande wa mwanasheria mkuu wa serikali, kuwasilisha maombi ya kupewa muda wa miezi miwili, ili kuweza kujibu kwa ufasaha hoja za wadai.

Kesi ya kupinga kuwasilishwa bungeni muswaada wa vyama vya siasa, imefunguliwa mahakamani hapo na Zitto Zuberi Kabwe, kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo.

Wengine walioshirikiana na Zitto, ni Joran Bashange, naibu katibu mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara na Salim Biman, mkurugenzi wa mawasiliano ya umma ya chama hicho.

Akisoma maamuzi madogo yaliyotokana na maombi ya mwanasheria mkuu na yale ya upande wa wadai, Jaji Sahe alisema, “kwanza kabisa, mahakama imeona hakuna sababu ya kuchukua muda mrefu kwa serikali kujibu hoja za walalamikaji.”

Amesema, “Mahakama inatoa siku saba (7) za kujibu hoja hizi. Hii ni kutokana na suala lililoletwa mahakamani, kuwasilishwa kwa hati ya dharura na kubeba maslahi mapana ya jamii.”

Pili, jopo hilo la majaji limesema, “mahakama imeona hakuna sababu kwa sasa ya kutoa zuio kwa mwanasheria mkuu wa serikali kuwasilisha bungeni, muswaada huo. Maamuzi yetu haya yanatokana na ukweli kuwa kesi hii, itasikilizwa kabla ya tarehe 29 Januari.”

Shauri hilo la madai Na. 31/ 2018 lilikuja mahakamani kwa mara ya kwanza leo Ijumaa kwa ajili ya kutajwa na kupanga siku ya kusikilizwa.

Katika shauri hilo, wadai hao watatu – Zitto, Bashange na Bimani – wanawakilishwa mahakamani na mawikili, Mpoki Mpare, Daim Halfan na Frederick Kihwelo.

Kabla ya maamuzi hayo, mawakili hao wa wadai  waliiomba mahamakama kutoa zuio la muda la kupelekwa bungeni muswada wa sheria ya vyama vya siasa.

Kufuatia maombi hayo, upande wa serikali uliomba mahakama hiyo kutoa muda wa miezi miwili kuweza kujibu hoja hizo.

Serikali italazimika sasa, kujibu hoja zote zilizowasilishwa na wadai, siyo zaidi ya tarehe 11 Januari mwaka huu.

Muswaada wa sheria ya vyama vya siasa, tayari umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni; kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, unatarajiwa kujadiliwa katika mkutano ujao wa Bunge.

Mkutano ujao wa Bunge, umepangwa kuanza tarehe 29 Januari mwaka huu.

Tangu kuwasilishwa kwa muswada huo bungeni, kumeibuka madai kadhaa kutoka vyama vya siasa, asasi za kiraia, makundi ya kijamii, wakieleza kuwa kilichowasilishwa bungeni, “ni ukandamizaji wa haki za wananchi.”

Makundi hayo yamekuwa yakidai kuwa kilichowasilishwa bungeni kinakwenda kuuwa moja kwa moja demokrasia. Wanasema, ndani ya muswaada, kujazwa mamlaka ya msajili wa vyama vya siasa, kuingilia uhuru wa vyama hivyo na kufuta hata uwanachama wa wanachama wake.

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), amegonga mwamba mahakamani. Ni baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, “kuzima” mkakati wake wa kuchelewesha kesi ya kupinga muswaada wa vyama vya siasa. Anaripoti Faki Sosi … (endelea). Jopo la majaji watatu wa mahakama kuu, wanaosikiliza kesi hiyo ya kikatiba, linaloongozwa na Jaji Barke Sahe, wameeleza mahakamani hapo kuwa suala lililopo mbele yake, “lina maslahi mapana kwa umma.” Maelezo ya mahakama yamefuatia upande wa mwanasheria mkuu wa serikali, kuwasilisha maombi ya kupewa muda wa miezi miwili, ili kuweza kujibu kwa ufasaha hoja za wadai. Kesi ya kupinga…

Review Overview

User Rating: 4.4 ( 2 votes)

About Faki Sosi

error: Content is protected !!
Visit Us On FacebookVisit Us On TwitterVisit Us On YoutubeVisit Us On Instagram