January 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli, Spika Ndugai wampa pole AG Kilangi

Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG) akiapa

Spread the love

JOHN Magufuli, Rais wa Tanzania, amempa pole Mwanasheria Mkuu wa Serikali nchini humo (AG), Profesa Adelardus Kilangi kwa majukumu mazito yaliyo mbele yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Pia, amemtaka Profesa Kilangi kuiangalia ofisi yake kwa umakini ili kuhakikisha kesi zinazofunguliwa dhidi ya Serikali na wananchi masikini wanaibuka washindi.

Rais Magufuli amesema hayo muda mfupi baada ya kumuapisha, Profesa Kilangi kuwa AG, hafla iliyofanyika leo Jumatatu tarehe 9 Novemba 2020 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Profesa Kilangi ameapishwa baada ya kuteuliwa tarehe 5 Novemba 2020 na Rais Magufuli.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Kilangi alikuwa AG katika muhula wa kwanza wa utawala wa Rais Magufuli uliokoma tarehe 5 Novemba 2020 na kuanza muhula mwingine wa pili wa miaka mitano kati ya kumi siku hiyo.

Rais John Magufuli

Kwa mara ya kwanza, Profesa Kilangi aliteuliwa kuwa AG, tarehe 1 Februari 2018 kuchukua nafasi ya George Masaju ambaye Rais Magufuli alimteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali, Rais Magufuli amemtaka Profesa Kilangi ajipange kuhakikisha majukumu ya ofisi yake yanatimiza kikamilifu kwani Watanzania wana matumaini makubwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Amesema, wanataka kuona Serikali yao inapata uwakilishi mzuri katika masuala ya kisheria, hivyo ahakikishe anasimamia vizuri kesi za Serikali na kuzitetea kwa uharaka mali za Serikali.

“Pamoja na kukupongeza, nakupa pole, mwanasheria mkuu wa serikali ni mtu mwenye majukumu mengi. Kwa hiyo waliokupa pole na mimi nakupa pole hivyo hivyo.”

“Ukajipange kweli kweli na ukaisimamie vizuri ofisi yako ili yale yanayohusu ofisi yako yakashughulikiwe kikamlifu. Kazi hii ni dhamana na sisi tumekupa,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, “Watanzania wanapenda kuona mafanikio mengi kupitia ofisi yako, wasingependa kuona kesi za Serikali zinashindwa na wakati mwanasheria mkuu wa Serikali yupo mwenye sifa nzuri, ni profesa kitaaluma amefanya kazi hata katika jumuiya za kimataifa.”

“Nina hakika Watanzania watapenda waone kesi zinazopelekwa mahakamani zinazohusu Serikali na mali zao zinatetewa kwa haraka na zinapata ufumbuzi mapema,” amesema Rais Magufuli.

Awali, Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza kwenye hafla hiyo alimpongeza kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo nzito na kuahidi kutoa ushirikiano pindi atakapouhitaji.

“AG ni nafasi nzito na huwa najiuliza anapata wapi muda kufanya kazi zake. Sababu ni mtu wa huku na huku, kushtakiwa mahakamni ni yeye kila siku kwa niaba ya watumishi wa Serikali. Kwa hiyo katika kukupongeza nakupa pole sababu ni mtu mwenye majukumu makubwa,” amesema Spika Ndugai.

Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG)

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amemshauri Profesa Kilangi kuhakikisha sheria za nchi zinafanya kazi ipasavyo kwa manufaa ya Watanzania wote hasa masikini.

“Ushauri wangu mdogo sana, umezungumzia muktadha wa sheria utakao kuongoza kutatua matatizo ya kisheria, ningekuomba usome andiko moja liliandikwa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa, kuhakikisha sheria inafanya kazi kwa manufaa ya wote,” amesema Profesa Juma.

Amesema andiko hilo la Kamisheni ya Umoja wa Mataifa linaelekeza wasimamizi wa sheria wahakikisheria zinasaidia na kuwawezesha wananchi masikini.

“Andiko linasema hakikisha sheria isaidie na kuwezesha watu masikini ambao ni wengi sababu shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinaongozwa kisheria na wewe ndio msimamizi mkuu wa sheria,” amesema Jaji Juma.

Profesa Juma amesema “na baada ya uchaguzi kuna ilani ambayo inatekelezwa, itakuja mbele yako kuitafsiri kwa mujibu wa sheria, unapoitafsiri utafsiri kwa kukumbuka watu masikini sababu wengi wao huwa wanaachwa katika tafsiri za kisheria.”

Kwa upande wake, Profesa Kilangi ameahidi kukabiliana na kesi zinazofunguliwa nje ya nchi dhidi ya Serikali.

Amesema anajua kutakuwa na mapambano ya kisheria ndani na nje ya nchi yatakayoibuliwa kupingana na msimamo wa Rais Magufuli kutetea rasimali za nchi pamoja na kuondoa utegemezi.

“Katika mazingira ya hapa kwetu, nimeiona nia ya Serikali yako kuleta maendeleo kwa watu kwa haraka zaidi lakini kupunguza utegemezi, sikujua ukitangaza nia hizo wakati huohuo unakua umetangaza vita ambayo inaibua mapambano ya kisheria.”

“Najua mapambano hayo yanapiganwa ndani na nje ya nchi, sehemu ya mapambano iko ndani na nje. Naelewa vizuri hali halisi naona changamoto zipo,” amesema Profesa Kilangi.

Prof. Kilangi amesema “naomba nitoe ahadi ya kufanyia kazi changamoto hizo. Naahidi kufanya kazi kwa akili yangu yote na nguvu zangu zote nikishirikiana na viongozi mbalimbali wa Serikali katika kutatua changamoto hizo.”

error: Content is protected !!