January 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli: Sina mpango kubadilisha Ma RC, DC, DED na…

Rais John Magufuli

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Magufuli, amewatoa wasiwasi wateule wake wa nafasi mbalimbali za uongozi kwamba hana mpango wa kubadilisha “nilioanza nao nitamaliza nao.” Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 9 Novemba 2020 mara baada ya kumaliza kumwapisha, Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG), Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Profesa Kilangi, amekuwa mteule wa kwanza kuapishwa tangu Magufuli alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Alhamisi iliyopita ya tarehe 5 Novemba, 2020 katika muhula wake wa pili wa utawala.

Rais Magufuli aliapishwa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba, 2020 kwa kupata kura 12 milioni kati ya kura 15 milioni zilizopigwa sawa na asilimia 84.4.

Tundu Lissu wa Chadema, aliyekuwa mshindani wake mkubwa, alipata kura milioni 1.9 sawa na asilimia 13.

Katika hotuba yake fupi leo, Rais Magufuli amesema, kumekuwa na tabia, kila Serikali inapoingia, kumekuwa na hofu haswa watendaji wa Serikali wanabadilishwa.

Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG) akiapa

Amesema, hana mapango wa kubadilisha, wakuu wa mikoa (RC), wilaya (DC), katibu tawala wa mikoa (RAS), katibu tawala wa wilaya (DAS), wakurugenzi wa halmashauri (DED), makatibu wakuu na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

“Nawashangaa kwa nini wamekuwa na hofu, kwa sababu kama ni mafanikio ya Serikali ni pamoja na wao, kama ni ushindi wa asilimia 84 ni pamoja na wao ndiyo wamewezesha kupatikana kutokana na kazi walizofanya kwenye maeneo yao,” amesema Rais Magufuli.

Amesema, wanasiasa walioguswa na hili ni pamoja na yeye aliyekwenda kuwaomba kura wananchi, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, waziri mkuu “kwa sababu lazima tuteue waziri mkuu mwingine” na wengine watakaoguswa ni spika na naibu spika ambao lazima wapigie kura na wiki ya kuwapima ni wiki hii.

“Mkuu wa mkoa unakuwa na wasiwasi gani, labda kama utendaji wako haukuwa mzuri, kwa sababu nashanaga napata meseji zingine, nimejitahidi katika kipindi changu, kana kwamba nilimwambia kipindi chake kinaisha baada ya mimi kuapishwa,” amesema Rais Magufuli huku akiibua furaha kwa wageni waalikwa.

Rais Magufuli amesema, “nimeona niwaambie kwamba wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya msiwe na wasiwasi na inawezekana wala kusitokee mabadiliko hata moja, labda kwa mtu atakayestaafu au atakayefanya mambo ya hovyo sana.”

“Kwa nini nibadili mkuu wa mkoa, kwa nini nibadili mkuu wa wilaya, kwa nini nibadilishe mkurugenzi, DAS, serikali ni ile ile, kama nilikuteua mwaka jana au miaka miwili mitano iliyopita, si uwezo ni ule ule na mtu ni yule yule.”

Rais Magufuli amewataka watetanji hao “wachape kazi, wasipochapa kazi shauri yao, wakijiandaa ili kuondoka shauri yao, labda waandike barua ya kuondoka lakini mimi najua nilianza nao na nitamaliza nao.”

“Hivyo hivyo kwa watendaji wengine, makatibu wakuu, vyombo vya ulinzi si ni hivyo hivyo, sasa unabadilisha nini na makamu wa Rais ni huyo huyo, inawezekana na spika ni huyo huyo, naibu spika huyo huyo na mwanasheria mkuu amekuwa huyo huyo, katibu mkuu kiongozi ni huyo.”

“Natoa wito kwa watendaji serikalini wachape kazi, kuchaguliwa kwetu haina maana kwamba tumekuja kubadilisha. Kwa hiyo, watu wachape kazi katika nafasi zao na kwa maana nyingine hakuna mabadiliko. Tulianza wote na tutamalia wote,” amesema.

error: Content is protected !!