Thursday , 18 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli, Nyusi waweka jiwe la msingi hospitali ya Kanda Chato
Habari za SiasaTangulizi

Magufuli, Nyusi waweka jiwe la msingi hospitali ya Kanda Chato

Spread the love

MARAIS John Magufuli wa Tanzania na Filipe Nyusi wa Msumbiji, wametoa maagizo kwa watendaji wanaosimamia ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato mkoani Geita kuhakikisha inamalizika kwa wakati. Anaripoti Mwandihshi Wetu, Geita … (endelea).

Jiwe hilo limeweka leo Jumatatu tarehe 11 Januari 2021 na marais hao, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya kikazi ya Rais Nyusi, nchini Tanzania.

Rais Nyusi amewasili mapema leo asubuhi na kupokewa na mwenyeji wake, Rais Magufuli katika Uwanja wa Ndege wa Chato Mkoa wa Geita.

Wakizungumza kwa awamu, baada ya kuweka jiwe la msingi la msingi la hospitali hiyo, Rais Nyusi ameipongea Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza ujenzi wa hospitali hiyo, akisema itasaidia kuokoa maisha ya wananchi.

“Serikali imeangalia afya ya wananchi kwa sababu inapenda wananchi.  Tunaweza kusema kila kitu lakini bila maisha, yote tunayosema hayataeleweka,” amesema Rais Nyusi.

“Hii hospitali haina chama, ni ya wananchi na kila mtu atakuja,” amesema

Kiongozi huyo wa Msumbiji amesema, atafuatilia kwa ukaribu ujenzi wa hospitali hiyo, ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na “Mheshimiwa Rais, nitakuwa nakupigia simu kila Jumamosi kuulizia maendeleo yamefikia wapi.”

Akielezea ujenzi huo, Rais Nyusi amesema, Serikali ya Msumbiji pia inajenga hospitali kila wilaya za nchji hiyo, ili kuokoa maisha ya wananchi wake.

Hospital ya Kanda Chato

“Hii ni zawadi kubwa ya kupata nafasi ya kuweka jiwe la msingi na hii ni hospitali kubwa sana, sisi Msumbiji tuna mradi wa kujenga hospitali kamili kila wilaya, itakuwa rahisi ndugu zetu pia waliokaribu wasiende mbali zaidi kwa shauri ya maisha,” amesema Rais Nyusi.

Amewaomba Watanzania kuendelea kuchapa kazi kwa ajili ya kujenga nchi yao kwa kutumia rasilimali zilizopo.

“Kitu kikubwa ni kazi tu, kuchapa kazi. Maana yake Mungu ametupa mali, tunaweza kutumia tukalima, kuchimba madini, kuvua samaki. Lazima tufanye kazi,” amesema Rais Nyusi.

Kuhusu ziara yake ya kikazi, Rais Nyusi amesema atazungumza na Rais Magufuli kuhusu ushirikiano wa mataifa hayo mawili katika masuala ya usalama, uchumi na diplomasia.

“Nitaongea na rais mpaka jioni ya leo, tutazungumza kuhusu maendeleo ya nchi zetu maana yake sio tu kwa shauri ya mpaka unao tuunganisha,  lakini kwa watu wetu wengi sana ambao wako Tanzania na Msumbiji,” amesema Rais Nyusi.

Hospitali ya Kanda Chato

Kwa upande wake, Rais Magufuli, amemshukuru Rais Nyusi kwa ujio wake sambamba na kukubali kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo.

“Mheshimiwa Rais Nyusi kwetu sisi wananchi wa kanda hii tunaiona hii ni zawadi kubwa kwa wewe kukubali kuja kuweka jiwe la msingi la hospitali hii itakayohudumia Watanzania,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amesema, hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi wa nchi jirani ikiwemo Msumbiji.

“Lakini nina uhakika kwa kuwa itakuwa hospitali kubwa itahudumia wananchi wa Msumbiji na nchi jirani,” amesema Rais Magufuli.

Akielezea utekelezwaji wa mradi huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwjaima, amesema utatekelezwa kwa awamu tatu chini ya mkandarasi ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Dk. Gwajima amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo ilianza tarehe 18 Septemba 2017 na inatarajiwa kukamilika Machi 2021.

“Awamu ya kwanza ujenzi wa hospitali hii ilianza  kwa lengo la kujenga majengo ya huduma za wagonjwa. Ujenzi wa awamu ya kwanza umekamilika kwa asilimia 90. Na kwamba makabidhiano yatafanyika 21 Machi 2021,” amesema Dk. Gwajima.

Waziri huyo wa afya amesema, ujenzi wa awamu hiyo unagharimu Sh.16 bilioni ambapo Serikali imetoa Sh.14 bilioni.

“Katika kukamilisha awamu hii ya kwanza, jumla ya Sh.16 bilioni zilikadiriwa kuhitajika. Hadi sasa, Serikali  imeshatoa Sh.14 bilioni sawa na asilimia 87.5,” amesema Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima amesema, awamu ya pili ya ujenzi huo unaokadiriwa kugharimu Sh.14 bilioni umeshaanza ambao utahusisha ujenzi wa majengo ya jiolojia, wodi za upasuaji mifupa na magonjwa ya ndani.

“Awamu ya pili, itahusisha majengo mengine ya jiolojia, wodi za upasuaji mifupa na magonjwa ya ndani. Endapo tutakamilisha kutakuwa tumeweza kupata vitanda 201. Sh. 14 bilioni zinakadiriwa na tayari Sh.4 bilioni zimeshalipwa na utekelzaji umefika asilimia 37,” amesema Dk. Gwajima.

Kuhusu awamu ya mwisho, Dk. Gwajima amesema ujenzi wake ambao bado haujaanza, utahusisha ujenzi wa majengo ya upasuaji, huduma za utakasaji vifaa, afya ya uzazi na vyumba vya kuhifadhia maiti.

Amesema ujenzi huo ukikamilika utakuwa na majeno 13, vitanda 436 na itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 700 hadi 1,000 kwa siku.

Amesema hospitali hiyo ikikamilika itahudumia wananchi milioni 14 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Utekelezaji wa mradi mradi huu, Serikali inatekeleza  kwa awamu kupitia, itakapiokamilima itahudumia wananchi takribani milioni 14 kutoka mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora, Rukwa, Geita na wilaya za Mwanza na Shinyanga inayopakana na Geita,” amesema Dk. Gwajima.

Dk. Gwajima amesema, Hospitali ya Rufaa ya Ngazi ya Kanda Chato, itafikisha idadi ya hospitali za ngazi hiyo kuwa tatu kati ya sita zilizopangwa kujengwa na Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Dk. Gwajima amesema, ujenzi wa hospitali hizo ni muendelezo wa kazi ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ya kuwasogezea karibu wananchi huduma bora za afya.

“Hatua hii ni kielelezo cha kazi kubwa uliyoanza kuifanya tangu ulipokuwa madarakani kama Rais wa Tanzania ya kuhakikisha unasogeza huduma za afya zilizo bora karibu zaidi kwa wananchi, kuanzia ngazi ya msingi hadi ubingwa bobezi,” amesema Dk. Gwajima.

Waziri huyo wa afya amesema, hadi sasa Serikali imejenga zahanati mpya 1,198, vituo vya afya vyenye uwezo wa kufanya upasuaji 487, hospitali za halmashauri 99 na hospitali za rufaa za mikoa tano.

“Watanzania wanafahamu kuwa umeboresha hospitali za Taifa katika kiwango kikubwa na hii yote imepelekea kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kuharakisha matibabu ya kibingwa bobezi,”amesema Dk. Gwajima na kuongeza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!