January 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli azungumzia uteuzi wa mawaziri

Baraza la Mawaziri lililomaliza muda wake

Spread the love

JOHN Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema, baraza lake la mawaziri atakaloliunda, linatarajiwa kuwa na mabadiliko “wapo watakaorudi na wapo ambao hawatarudi.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumatatu tarehe 9 Novemba 2020 mara baada ya kumaliza kumwapisha, Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania (AG), Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Katika hotuba yake fupi, Rais Magufuli alianza kwa kuwatoa hofu viongozi wateule wote ambao wamekuwa na hofu ya kuondolewa ama kubadilishwa nafasi walizonazo baada ya yeye kuapishwa tarehe 5 Novemba 2020 kuwa Rais wa Tanzania kwa kipindi cha pili.

Amesema, hatarajii kufanya mabadiliko ya viongozi hao labda kwa wale watakaokuwa wanastaafu ama kutofanya vizuri katika majukumu yao.

“Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi, Viongozi wa Taasisi na Idara za Serikali na wengine wote chapeni kazi, simuondoi mtu kwenye nafasi yake labda aharibu yeye mwenyewe au astaafu,” amesema Rais Magufuli.

Akigusia uteuzi wa mawaziri, Rais Magufuli amesema, “mabadiliko yatakuwepo kwa baraza la mawaziri, wapo watakaorudi na wapo ambao hawatarudi. Na siku hizi chaguo ni kubwa, nina wabunge 264 kwa hiyo uchaguzi ni mkubwa, hili sitaki kusema uongo.”

Rais John Magufuli

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020, chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejinyakulia wabunge zaidi ya 255 kati ya 264 huku kikijipatia wabunge wa viti maalum 94.

Kati ya walioibuka washindi kwenye uchaguzi huo ni waliokuwa mawaziri kwenye baraza lake lililopita pamoja na waliokuwa wateule wake kwenye nafasi za wakuu wa mikoa (RC), wilaya (DC), wakurugenzi wa taasisi za serikali na wakurugenzi wa halmashauri (DED).

Wamo katibu wakuu wa wizara, wasomi wa sekta mbalimbali ikiwemo za kifedha pamoja na wasanii, hali ambayo imekuwa ikiibuka mjadala kwamba kuna uwezekano kukawa na sura mpya katika baraza hilo atakaloliunda.

Kassim Majaliwa, aliyekuwa Waziri Mkuu,

Katika baraza lililopita ambalo aliliunda kwa mara ya kwanza tarehe 10 Desemba 2015 baada ya kuingia madarakani, ni mawaziri sita pekee walibaki hadi mwisho ambao hawakutumbuliwa au kuhamishwa wizara zao.

Mawaziri hao ambao wamerejea tena bungeni na wizara zao kwenye mabano na majimbo ni; Jenista Muhagama (Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Wenye Walemavu- Peramiho), Dk. Philipo Mpango (Fedha na Mipango- Buhigwe) na William Lukuvi (ardha na maendeleo ya makazi- Isman).

Wengine ni; Profesa Joyce Ndalichako (elimu, sayansi na teknolojia) na Ummy Mwalimu (afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto-Tanga Mjini)

Hata hivyo, Dk. Hussein Mwinyi aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, yeye amehitimisha safari yake ya uwaziri kisha kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais Zanzibar na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kumtangaza mshindi.

error: Content is protected !!