Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli azungumzia uchaguzi mkuu 2020
Habari za Siasa

Magufuli azungumzia uchaguzi mkuu 2020

Spread the love

TUME ya Taifa ya uchaguzi (NEC), imemkabidhi cheti cha ushindi wa urais wa Tanzania, mgombea wa nafasi hiyo, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Makabidhiano ya cheti hicho yaliyofanyika katika ofisi za NEC, eneo la  Njedegwa, jijini Dodoma, yalihudhuliwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa, Bunge, Mahakama, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na baadhi ya wagombea urais walioshiriki katika uchaguzi mkuu wa 28 Oktoba 2020.

Akizungumza katika hafla hiyo, leo Jumapili, tarehe 1 Novemba, mwenyekiti wa tume hiyo ya uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage amesema, Magufuli ameshinda uchaguzi huo baada ya kupata kura milioni 12.5 kati ya milioni 15.9 zilizopigwa.

Alisema, aliyekuwa mshindani wa karibu wa mwanasiasa huyo, mgombea wa Chadema aliyeungwa mkono na ACT- Wazalendo, Tundu Lissu, aliambulia kura 1.9 milioni.

Kwa mujibu wa NEC, watu waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, walikuwa 29 milioni.

Kwa upande wa nafasi za ubunge, kati ya majimbo 264, CCM kimejikusanyia viti 258; ACT-Wazalendo imepata viti 4, Chadema 1 na CUF 3 (vitatu).

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, matokeo haya, ni anguko kubwa zaidi kutokea tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1995.

Hata hivyo, Chadema na ACT-Wazalendo, wametangaza kutotambua matokeo yote ya uchaguzi huo, pamoja na ule uliosimamiwa na NEC na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Vyama hivyo viwili vimedai kuwa uchaguzi huo wa Jamhuri ya Muungano na ule wa Zanzibar, ligubikwa udanganyifu, wizi na uliendeshwa kinyume na sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.

Kwa mujibu wa viongozi wa vyama hivyo viwili vikuu vya upinzani nchini, hawakubaliani na uchaguzi huo na matokeo yake yote, na kwamba tayari wamepanga kufanya maandamano ya amani yasiyokuwa na kikomo kuanzia kesho Jumatatu, tarehe 2 Novemba, ili kushinikiza kurejewa upya kwa uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa tamko la pamoja la viongozi wakuu wa vyama hivyo, lililotolewa jijini Dar es Salaam, jana Jumamosi, Chadema na ACT- Wazalendo, wanadai kuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi wa Jumatano iliyopita, kwa kuwa ”kilichofanyika si uchaguzi, bali ni unyang’anyi.”

Mkutano wa viongozi wa vyama hivyo na waandishi wa habari, ulihudhuriwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe; katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika; makamu mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Bara), Doroth Semu; Lissu, pamoja na mgombea wake mwenza, Salum Mwalimu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbowe amesema, “uchaguzi ulioendeshwa na ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar) na NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi), haukuwa huru na haki,” na kwamba wamejiridhisha pasipo na shaka kuwa kulikuwa na udanganyifu.

Katika hotuba yake fupi aliyoitoa mara baada ya kukabidhiwa “cheti chake cha ushindi,” rais huyo mteule alisema, “nawashukuru wananchi wote kwa kunichagua kuongoza kipindi kingine cha pili cha uongozi wangu,” yeye na makamu wake, Samia Suluhu.

Baadhi ya wagombea urais mwaka 2020 wakimsikiliza rais Magufuli

Dk. Magufuli amesema, uchaguzi umemalizika, “kilichobaki ni kuchapa kazi.” Amedai kuwa uchaguzi huo, umekwenda vizuri sana tena kwa kiwango kikubwa.

Amesema, “mwaka huu kulikuwa na karatasi za kupigia kura kwa wasioona na matokeo yametolewa kwa haraka hivyo kupunguza taharuki.

“Niwaahukuru sana Watanzania wenzangu kwa kunichagua kwa kura nyingi kuwa Rais na Samia Suluhu kuwa makamu ambao kitakuwa kipindi chetu cha mwisho.”

Ameongeza: “…kwangu mimi nina deni kubwa sana. Nina mwomba Mungu anisaidie na viongozi wenzangu tuweze kutimiza haja kwa Watanzania. Kupata asilimia 84.4, ni imani kubwa na imani yao nitaitimiza kwa kufanya kazi usiku na mchana.

“Ushindi huu si wangu au wa chama changu CCM. Ni ushindi wa Watanzania wenzangu, aliyenipigia kura na asiyenipigia kura. Nitawatumikia wote bila kujali itikadi za chama, dini, ukanda au rangi.”

Aliwashukuru wagombea wenzake walioshiriki uchaguzi huo na kusema, “mmetusaidia kutuonyesha Watanzania wanataka nini. Kuja kwenu ni ishara ya kukomaa. Siasa si ugomvi wala uadui, niwaahidi kushirikiana nanyi. Ni kweli kwamba wananchi wametupa ushindi mkubwa lakini hatuwezi kusahau ushauri wenu kwangu kwani Tazania kwanza, mengine baadae.”

Rais huyo mteule amewashukuru viongozi wa dini kwa kuombea taifa kabla na baada ya uchaguzi.

Kuhusu vyombo vya ulinzi na usalama, Dk. Magufuli alisema, “nivipongeze vyombo vya ulinzi na usalama kwa kudumisha usalama wakati wa uchaguzi na ni imani yangu vitaendelea kulinda amani yetu hata baada ya uchaguzi.”

Dk. Magufuli ambaye anatarajiwa kuapishwa Alhamisi ya tarehe 5 Novemba 2020 Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, amesema kuwa “tumepiga kura kwa usalama na tumepokea matokeo kwa usalama na tumeionyesha dunia tumekomaa kisiasa.”

Amesema, yeye na wenzake wanatarajiwa kutekeleza na kusimamia Ilani ya uchaguzi ya CCM na kuhakikisha wanaitendea haki kwa kutafua kero mbalimbali za wananchi.

Amesema, “niwapongeze wanachama wa vyama vingine kwa kunipigia kura, wasanii, wanamichezo na wanahabari wote hadi kuniwezesha kuchaguliwa. Niwaombe waliochaguliwa hasa wa chama changu kwenda kuwatumikia vyema Watanzania ambao wanataka kutatuliwa matatizo yao, tukashikamane kuijenga hii nchi.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!