MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli amewahoji wananchi wanaotaka akae madarakani muhula mmoja tofauti na walivyokaa marais waliopita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Rais wa awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere alikaa madarakani zaidi ya miaka 20 huku waliomfuata Dk. Ali Hassan Mwinyi (awamu ya pili), Benjamin Mkapa (awamu ya tatu) na Jakaya Kikwete (awamu ya nne) waliongoza miaka 10 kila mmoja ambayo ni sawa na mihula miwili.
Rais Magufuli aliyeingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015 amesema, kwa nini watu hao wanataka wampunzishe ilihali amekaa madarakani miaka mitano.
Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Chemba mkoani Dodoma leo Jumatatu tarehe 26 Oktoba 2020, amewaomba Watanzania wamchague tena akamilishe miaka yake 10.
“Nyerere alikaa miaka 20 na kitu, alitutafutia uhuru akang’atuka mwenyewe, akaja Mzee Mwinyi akakaa miaka 10 akaondoka, marehemu Mkapa kakaa miaka 10 akapumzika, akaja Kikwete amekaa miaka 10 akampumzika, mimi nimekaa miaka mitano mnataka mnipumzishe.”
“Mtanipa miaka mitano mingine nifikishe kumi kama wenzangu,” amewahoji wananchi hao ambao walimuahidi kumchagua.
Rais Magufuli amewaahidi wananchi wa Chemba na Watanzania kwa ujumla akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania ataongeza kasi ya utatuzi wa changamoto zao sambamba na kuwaletea maendeleo.
Aidha, amewasihi Watanzania kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, ikiwa sambamba na kurudi nyumbani baada ya kupiga kura Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.
Leave a comment