Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli atonesha kidonda cha Mkapa
Habari za SiasaTangulizi

Magufuli atonesha kidonda cha Mkapa

Spread the love
JINAMIZI la sera ya ubinafsishaji wa rasimali za nchi, ikiwamo viwanda, mashamba na mabenki, mradi ambao uliasisiwa wakati wa utawala wa Benjamin William Mkapa, bado linarindima. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Machungu hayo ya ubinafshaji, sasa yameanza kuhubiriwa na mmoja wa watu walioshiriki kupitisha maamuzi na kusimamia zoezi hilo, Rais John Pombe Magufuli.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 72 kutoka Chunya kuelekea jijini Mbeya, leo tarehe 27 Aprili 2019 na Rais Magufuli alisema, “Nyerere (Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania) alijenga viwanda mbalimbali. Lakini tulikuja tukaviuza.”

Alisema, “matokeo yake, kijana unamaliza chuo kikuu, unakosa ajira. Ni kwa sababu, tulifanya makosa haya wakati fulani.”

Alisema, “…lazima tuseme ukweli, tulifanya makosa. Siwezi kuwa rais wa milele; ni lazima katika kipindi change, napaswa kueleza ukweli.

Alisema, “siwezi kuwa rais wa maisha, ni lazima nitaondoka madarakani. Lazima niseme ukweli. Najua wapo watakaochukia na wapo watakaofurahi. Lakini lazima niseme ukweli, kwamba tulikosea sana katika suala hili la ubinafisishaji.” 

Katika mkutano wa Nane wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofayika katika Ukumbi wa Nkurumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), tarehe 14 Juni 2016, Mkapa alikiri kuwa sera yake ya kuuza viwanda, mashamba, mabenki; na kwa ujumla, “sera yake ya ubinafsishaji njia za uchumi, haikuwa sahihi.”

Alisema, hatua ya kuleta sera ya ubinafsishaji bila kuweka chombo maalum cha kudhibiti, kumesababisha hasara kuhbwa kwa taifa.

Rais Mkapa alihudumu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano, kati ya mwaka 1995 hadi 2005. Alipokea madaraka hayo kutoka kwa mtangulizi wake, Rais Ali Hassan Mwingi aliyeanza kuhudumia taifa kuanzia 1985 mpaka 1995.

Mwalimu Nyerere alikuwa rais wa Tanzania, tangu taifa hili lililopopata uhuru wake kutoka Uingereza, tarehe 9 Desemba 1961. Aling’atuka madarakani, mwaka 1985.

Rais Magufuli alikuwa mmoja wa wajumbe wa mawaziri katika serikali ya Mkapa; baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanasema, “bila Mkapa, Magufuli asingekuwa rais.”

Miongoni mwa ubinafshaji na uuzaji wa mali za umma, unaolalamikiwa na wananchi waliowengi, ni ule wa uuzaji uuzaji wa nyumba za serikali, kazi inayodaiwa kusimamiwa  na Rais Magufuli, wakati akiwa waziri wa ujenzi, katika serikali ya Mkapa. 

Rais Magufuli amekuwa mgumu kulizungumzia suala hili. Alipoulizwa na mwandishi wa gazeti la kila wiki la Raia Mwema, tarehe 15 Septemba mwaka 2015, katika mahojiano maalumu yaliyofanyika mjini Tabora, juu ya suala hilo, Rais Magufuli aliahidi kulitolea jibu swala hilo muda mwafaka. Mpaka sasa, hajafanya hivyo.

Gazet lilimuuliza: “Suala la uuzaji wa nyumba za serikali ambalo limetekelezwa katika wakati ambao ukiwa Waziri wa Ujenzi bado gumzo na limekera Watanzania wengi. Unasemaje kuhusu hili?” 

Mkapa na serikali yake, waliuza mithili ya mali ya wizi, nyumba zaidi ya 8,000, baadhi zikiwa zimejengwa katika maeneo nyeti ya serikali. 

Sera ya ubinafsishaji ilibuniwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuridhiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, Januari mwaka 2004. Mwenyekiti wa CCM wakati huo, alikuwa Mkapa.

Kabla ya NEC kupitisha sera hiyo, chama hicho kiliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa ubinafsishaji, “hoja kuu za ubinafsishaji ni nzito na hazipingiki kama zinavyoimarishwa na mafanikio yaliyokwishapatikana.”

Semina hiyo iliyochochea mjadala ulioibuliwa na Dk. Abdallah Kigoda ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Ubinafishaji. Dk. Kigoda ndiye aliyekuwa utetezi mkubwa wa sera hiyo ya CCM.

Mkapa na wenzake, taarifa zinasema, alilazimisha kila mtu kuamini na kukubali bila kuhoji ubinafshaji uliokuwa unafanyika.

Alisema, hatua ya serikali ya kubinafsisha mashirika yake ya umma, kutajenga ushirikiano wa kudumu baina ya wawekezaji wa nje, serikali na wawekezaji wa ndani kwa nia ya kuongeza ufanisi, kuboresha utendaji, kupanua wigo wa ajira, kuongeza ubora wa bidhaa na kuyapatia mitaji na utaalamu mashirika yaliyobinafsishwa.”

Akiwa kwenye tamasha hilo, Rais Mkapa alisema, “kukosekana kwa mfumo mzuri wa udhibiti wa ubinafishaji, kumesababisha kuwepo kwa watu waliotumia fursa hiyo kwa maendeleo yao binafsi na siyo kwa taifa.”

Alisema, “kwenye uongozi wangu, kitu ambacho mpaka sasa ninajuitia, ni kuanzisha sera ya ubinafsishaji na kushindwa kuweka mfumo au chombo cha kuudhibiti.”

Aliongeza, “kuhusu ubinafsishaji huo, ndio kitu naweza kukiri nilikosea na ninachoweza kuwaomba Watanzania msamaha.”

Mbali na kuweka jiwe la msingi katika barabara ya Chunya – Mbeya Mjini, Rais Magufuli, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kilomita 39, inayotoka Chunya hadi Makongorosi.

Barabara hiyo, inatarajiwa kuungunisha mkoa wa Mbeya na wilaya za Sikonge, mkoani Tabora pamoja na mkoa wa Singida.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametoa siku saba kwa wakuu wa mikoa yenye machimbo ya madini, kuanzisha masoko ya madini.

Ameagiza wateule wake hao, kuhakikisha ndani ya wiki moja, wanaanzisha masoko hayo hata kwenye ofisi zao au magari yao, kama mchakato wa upatikanaji wa maeneo na majengo utakuwa mgumu.

“Ndani ya siku saba, hili soko liwe limefunguliwa hapa. Kama   mkuu wa mkoa wa Geita amefungua, sioni sababu ya mikoa mingine kutofanya hivyo. Mnasubiri nini mpaka malaika Gabriel aje,” alihoji mkuu huyo wa nchi.

Alisema, “nimeshatoa maagizo kazi ni kutimiza, hili soko litakuwa jaribu lako la shetani, wakuu wa mikoa mnanisikia, kama Mkuu wa Mkoa wa Geita ameanzisha nyie mnasubiri nini, hata gari la mkuu wa mkoa tumieni polisi wapo wekeni muuze.”

Akioneshwa kutofurahishwa na wakuu hao kutotekeleza agizo lake la uanzishwaji wa masoko ya madini, Rais Magufuli amesema, hawezi kukubali kuwa na wakuu wa mikoa ambao hawatekelezi maagizo yake, bali anataka viongozi hao wafanye kazi kwa ajili ya kusaidia wananchi.

Amesema, “na hili agizo si la mkuu wa mkoa wa Mbeya, wa Katavi ajiandae hivyo hivyo, Singida, Arusha wajiandae hivyo hivyo. Siwezi  kuwa na wakuu wa mikoa naagiza, hawatekelezi. Kwangu hapana, ukuu wa mkoa ni kufanya kazi na kuwahudumia wananchi.” 

Aliongeza, “nilitoa maelekezo wakafungiwe masoko ya madini, tangu nimefika hapa sijaliona soko, Geita amefungua mkuu wa mkoa wa pale, na dhahabu halihitaji jumba kubwa sana hata ukiwa na chumba kimoja, viwili unauza, sasa nakuagiza ili shetani akupitie mbali nataka soko la dhahabu hapa Chunya lianze, hakuna sababu ya soko hilo kutoanzishwa hapa, tafute jengo lolote.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Chadema: Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

error: Content is protected !!