Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli alivyowachambua mawaziri, wapa maagizo
Habari za Siasa

Magufuli alivyowachambua mawaziri, wapa maagizo

Rais John Magufuli
Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Magufuli amewachambua mawaziri wake 21 na manaibu waziri 22, aliowateua tarehe 5 Desemba 2020 na kuwataka kwenda kufanya kazi ili kuwaletea wananchi maendeleo na kutatua kero zinazowakabili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Rais Magufuli ametoa nasaha hizo jana Jumatano tarehe 9 Desemba 2020 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, mara baada ya kumaliza kuwaapisha na kuwakabidhi mwongozo wa baraza la mawaziri.

Uchambuzi huo ulianza kwa Waziri wa Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, ambapo Rais Magufuli amesema, alimteua ili baraza lake liwe na mchanganyiko wa vijana na wazee.

Rais Magufuli amesema, Kapteni Mkuchika atakuwa mshauri wake, kwa kuwa ana uzoefu kuhusu masuala ya uongozi, baada ya kuhudumu katika Serikali za awamu ziliyopita.

Kapteni Mkuchika alifanya kazi na Rais wa awamu ya kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Ali Hassan Mwinyi (awamu ya pili)., Hayati Benjamin Mkapa (awamu ya tatu) na Jakaya Kikwete (awamu ya nne).

George Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora

“Ndio maana tume-balance wazee wamo, Mkuchika alianza kufanya kazi tangu Mzee Nyerere, wakati wa Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Ni lazima tubakishe kumbukumbu katika Taifa hili, hata kwenye baraza nahitaji wazee wa kunishauri,” amesema Rais Magufuli.

Amesema, amemteua Ummy Mwalimu kuwa Waziri wa Muungano na Mazingira, kwa kuwa alifanya vizuri alipokuwa Waziri wa Afya, hivyo atamsaidia kuimarisha wizara hiyo inayosimamia masuala ya Muungano, iliyokuwa inalegalega.

“Tumemchukua Ummy mama wa Corona, alifanya kazi nzuri sana lakini tukaona kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais pana legalega, juzi tumeshika zaidi ya magari saba yanasomba vyuma vinaitwa chakavu lakini ni vyuma ambavyo vinajenga SGR,” amesema Rais Magufuli.

Prof. Kitila Mkumbo

Amesema, Wizara ya Maliasili na Utalii amteua Dk. Damas Ndumbaro kuiongoza wizara hiyo, ili akaitumie taaluma yake ya sheria katika kukusanya mapato.

Amesema hakutaka kumteua mtu atakayetumia ndege za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), kufanya starehe badala ya  kazi.

“Kwenye utalii Dk Ndumbaru ukafanye kazi kweli kweli, ukaitumie sheria yako katika kuhakikisha tunapata pesa, sio kila siku unachukua ndege za Tanapa unakwenda kustarehe huko, tunataka kazi,” amesema.

Rais Magufuli amesema, ameamua kuwarudisha kwa pamoja, William Lukuvi (waziri) na Angelina Mabula (naibu), katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa kuwa walifanya kazi vizuri.

George Simbachawene

Katika Baraza la Mawaziri lililopita, Lukuvi na Mabula walikuwa katika wizara hiyo waliodumu mwanzo hadi mwisho.

“Wizara ya ardhi tunataka kuwe na mageuzi, ndio maana tume warudisha wote. Mkikosea tuna waondoa wote, mawaziri wote mmerudi mkaisimamie sekta ya ardhi,” amesema Rais Magufuli.

Katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Rais Magufuli amesema amemrudisha Profesa Joyce Ndalichako kwa sababu alifanya vizuri katika baraza lililopita.

“Wizara ya elimu tumerudisha Profesa Ndalichako, tukamleta mtu mwingine, tunataka mageuzi mazuri kwenye wizara na kwenye hili nataka mkaanzishe historia yetu, somo la historia liwe la lazima,” ameagiza Rais Magufuli.

Profesa Ndalichako ameagizwa na Rais Magufuli alifanye somo la Historia kuwa la lazima shuleni, pamoja na kuanzisha mtaala wa historia ya Tanzania.

Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu

“Ifundishe historia ya Tanzania, tunasoma historia za mbali, tunataka watoto wetu wafundishwe historia  na hiyo itasaidia kujenga uzalendo. Watanzania wajue walikotoka sababu saa nyingine vijana wetu hawajui historia ya nchi yetu,” ameagiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema amemrudisha tena Seleman Jaffo kuwa Waziri wa Ofisi ya Rais-Tamisemi, kwa kuwa alifanya vizuri awamu iliyopita, licha ya wizara yake kuwa na dosari.

“Tamisemi kuna mambo mengi hasa matumizi mabaya ya fedha.  Kuzunguka umefanya vizuri lakini kwenye matumizi mabaya ya fedha bado, na nilifikiria kukurudisha ama kutokukurudisha hapo,” amesema Rais Magufuli.

Ametaja dosari hizo kuwa ni, matumizi mabaya ya fedha, na kutoa mfano wa mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita aliyetumia Sh.400 milioni kwa ajili ya kununua gari akimtaka “nenda kaanze na huyu, haiwezekani anakuwa na gari la kutembelea ambalo RC hana.”

Rais Magufuli amesema amemrudisha Dk. Medard Kalemani katika Wizara ya Nishati, kwa kuwa alifanya kazi nzuri ya kusambaza umeme vijijini.

Huku Doto Biteko akimrudisha tena katika Wizara ya Madini kwa kuwa awamu iliyopita alifanya vizuri katika ukusanyaji kodi. Hata hivyo, amemuagiza Biteko aongeze nguvu katika kudhibiti utoroshaji wa madini.

Rais Magufuli amesema, amemteua Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Abdalla Ulega (naibu), ili wakaisimamie vyema sekta hiyo.

Huku akiwaonya kwamba, ikifanya vibaya hususan kwa timu za taifa kufungwa ovyo, atawaondoa.

“Wizara ya michezo tumekupeleka tukacheze, ole wako tukalale na mabao kumi mtaondoka wote siku hiyo hiyo, msifikiri mmepelekwa wizara rahisi. Nataka tukashinde kweli na timu ya taifa si lazima iwe na u-Simba na Yanga,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, ameteua Elias Kwandikwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kwa kuwa ni mpole.

“Wizara ya Ulinzi tumeona tukupeleke huko sababu ni mpole ili watu wa jeshi wafanye vizuri, nitashangaa na wewe uende na ‘WhatsApp’ ukapige picha mzinga, ukaseme sasa naendesha kifaru,” amesema Rais Magufuli.

Profesa Adolf Mkenda amemwapisha kuwa waziri wa kilimo kwa kuwa ana taaluma ya masuala ya uchumi, ambapo atamsaidia kuinua uchumi wa Tanzania kupitia sekta ya kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania.

“Katika Wizara ya kilimo, Prof. Mkenda umechukua uchumi ukawa profesa, sasa tunataka uchumi ukafanyike kwenye kilimo, kimeajiri watu zaidi ya asilimia 70,” amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo, Rais Magufuli amesema hajateua manaibu waziri kwenye wizara hiyo kama ilivyokuwa huko nyuma na kumrudisha Hussein Bashe peke yake.

“Bashe, alijitahidi kufanya kazi yake, ndio maana hatukuweka manaibu wawili ili akaishike yote, tunataka Watanzania wakauze mazao yao nje, matajiri wakatoke kwenye kilimo,” amesema Rais Magufuli.

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi amemteua Dk. Leonard Chamriho kuwa waziri, akisema alisimamia vyema sekta ya ujenzi alipokuwa Katibu Mkuu katika wizara hiyo, hasa kwa kusimamia ununuzi wa rada, bandari na Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA).

Rais Magufuli amesema, amemteua Prof. Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Uwekezaji, kwa kuwa ana uzoefu wa kuzungumza, ili akatumie vyema kipaji chake hicho katika kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania.

“Prof. Mkumbo wizara ya maji hukufanya vizuri, ulikuwa katibu mkuu, tumekupa uwekezaji sababu unajua kuandika na kuzungumza, kazungumze na wawekezaji. Nataka wawekezaji wawe wengi na majibu yawe haraka, nataka wawekezaji angalau ndani ya siku 14 wawe wamepata kila kitu,” amesema Rais Magufuli.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!