NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula ameagiza zoezi la kupima upya mipaka ya vijiji vya Kono na Ketembere kuanza haraka. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).
Vijiji hivyo vipo katika Kata ya Nata na Rigicha wilayani Serengeti Mkoa wa Mara ambapo ameagiza ifikapo Desemba 2018, ramani ya mipaka ya vijiji hivyo iwe imekamilika na kutolewa.
Agizo la Mabula linafuatia mgogoro wa muda mrefu uliokuwepo baina ya mipaka ya vijiji hivyo jambo linalosababisha shughuli za maendeleo ikiwemo mpango wa matumizi bora ya ardhi kushindwa kufanyika.
Akiwa katika ziara yake ya kutatua mgogoro huo,Mabula amesema, mgogoro wa mpaka baina ya vijiji hivyo ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi kushindwa kufuata taratibu za kupima mipaka kwa kuwashirikisha wananchi wa pande zote mbili.
“Makosa yaliyofanywa na ofisi hayawezi kuleta ugomvi katika vijiji hivyo na ramani ya eneo hili itarekebishwa kulingana na dira na wizara itaangalia namna ya kushughulika na waliokwepesha mipaka ili kujua walikuwa na maana gani” amesema Mabula.
Kwa mujibu wa Mabula lengo la kupima mipaka ni kuwezesha kuwepo mpango wa matumizi bora ya ardhi ambapo kupitia mpango huo wananchi wataweza kupatiwa hati miliki ikiwemo hati za kimila kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi na kusisitiza kuwa ardhi ndiyo mtaji pekee kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Awali aliwapa nafasi wananchi wa vijiji vya pande zote mbili kueleza jinsi wanavyoifahamu mipaka ya vijiji vya Kono na Ketembere ambapo wengi waliutambua Mto Masara kama mpaka wa vijiji hivyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kono, Michael Oyatason amesema, vijiji hivyo awali havikuwa na mgogoro wowote ila tatizo lilianza mara baada ya uwekaji alama za mipaka ambao haukushirikisha pande zote mbili kinyume kabisa na utaratibu wa kuainisha mipaka.
Mpima Ardhi Kanda ya Simiyu, Godwin Saiguran amemuahidi Mabula kuwa zoezi la uanishaji mipaka ya vijiji vya Kono na Ketembere kwa kushirikisha wananchi wa pande zote mbili litakamilika ndani ya siku nne.
Katika hatua nyingine Mabula ametatua mgogoro mkubwa baina ya vijiji vya Kazi na Rwamchanga vilivyopo katika Kata ya Manchira, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Mgogoro katika eneo hilo unachangiwa na msuguani wa wananchi wanaotaka kuwa na vijiji viwili kama ilivyoainishwa katika mipaka ya kiutawala ama kuwa na kijiji kimoja.
Awali kabla ya kuzungumza na wananchi wa vijiji hivyo Mabula alizungumza na wajumbe wa serikali ya vijiji ambapo alipowahoji viongozi wanaotaka kuwepo kijiji kimoja ama viwili ni wajumbe wawili kati ya nane waliokuwa wakihitaji kijiji kimoja.
Leave a comment