Tuesday , 19 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Maaskofu waicharukia serikali
Habari Mchanganyiko

Maaskofu waicharukia serikali

Askofu Mkuu wa KKKT Askofu Dk. Frederick Shoo
Spread the love

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo, amesema ya kuwa kuna watu duniani leo wanaotumia nguvu kuuficha ukweli, bila kujua kuwa ukweli unaasili ya kutofichika. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Alisema, na upendo wa dhati ndiyo uliowafanya kina mama waliokwenda kaburini kwa Yesu wakadiriki hata kuhatarisha maisha yao.

Baba Askofu Shoo alitoa kauli hiyo, wakati wa Misa ya Pasaka iliyofanyika jana Jumapili.

Alisema, Wakristo ni wafuasi wa Yesu Kristo, hivyo wanapaswa kuukumbatia ukweli katika mambo yote.

“Wakati wa Yesu, maaskari waliokuwa wakilinda kaburi walipewa fedha nyingi ili kuuficha ukweli, lakini haikuwezekana na leo wapo watu ambao wanajaribu kuwazuia Wakristo kutangaza habari za Yesu na kulizuia Kanisa kufanya kazi ya Kitume bila kujua kuwa tendo hilo ni la Mungu mwenyewe.”

Naye Askofu wa Jimbo Katoliki Kayanga, mkoani Kagera, Almachius Rweyongeza, amesisitiza kuwa “amani ni tunda la haki.” 

Amesema, amani inayozungumzwa siyo tu ya nchi kutokuwa na vita au utawala wa mabavu, “ni katika muktadha wa utoaji haki sawa kwa wote.”

Askofu Rweyongeza alikuwa akihutubia Misa takatifu ya Pasaka, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu George, mkoani Kagera.

Alisema, “Amani ni kazi ya haki. Ni matunda ya haki. Amani haiwezi kufikiwa mara moja, bali inajengwa siku kwa siku, hivyo ni kazi endelevu na huwezi kusema leo umekamilisha.”

Askofu Rweyongeza amesema, kwa sababu binadamu ni dhaifu na wamejeruhiwa na dhambi; kila mmoja wao kwenye taifa anatakiwa kutawala tamaa zake ili aweze kuilinda amani hiyo.

“Serikali inapaswa kujihusisha katika kulinda amani ya nchi na kutaka makundi yote kuitumia sikukuu ya Pasaka kujitathmini,” amesisitiza.

Alinukuu kauli kuu ya chama cha Tanganyika African National Union (TANU) inayosema, “binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja.” Aliasa kuwa kila mmoja anapaswa kushiriki katika mapambano ya kiroho ya kuhakikisha amani inaendelea kutawala nchini.

Alisema, “…Aluta Kontinua, ni mapambano endelevu ya kiroho, yatupasa kukaa chonjo kama hekima ya Walatini isemavyo ‘wakati wa vita miili ya watu hujeruhiwa kwa silaha lakini wakati wa amani hujeruhiwa kwa anasa na tafrija.”

Alisema, baada ya kupata Uhuru, Mwalimu Julius Nyerere alibaini maadui watatu wa taifa ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.

“Hatutafurahia uhuru kama bado hao maadui wanatuchachafya, wanatuhangaisha. Hivyo lazima tujiulize ni kwa njia gani au mbinu gani au rasilimali gani taifa limeweza kutumia kupambana hasa na adui ujinga na maradhi ili kupata maendeleo ya kweli,” alieleza.

Akizungumzia kuhusu elimu, Askofu Rweyongeza alisema, kuna maneno yameandikwa katika chuo kikuu kimoja kwamba, ukitaka kuangamiza Taifa huhitaji kutumia silaha za nyuklia, njia nzuri ni kuharibu mfumo wa elimu.

Alisema, “ruhusu mbumbumbu waonekane wamefaulu na wasonge mbele hadi vyuo vikuu, matokeo yake yatajionyesha baada ya muda.

“Mbumbumbu hao wakihitimu kwa kupata vyeti hewa, wagonjwa watafia mikononi mwa madaktari na manesi, majengo yataporomoka mikononi mwa wahandisi, pesa zitapotea mikononi mwa wachumi na mafisadi, utu utapotea mikononi mwa viongozi wa juu na Serikali na haki zitapotea mikononi mwa mahakimu na wanasheria.”

Askofu huyo alisema kila mara wamekuwa wakishuhudia mitalaa ya elimu, sera na miongozo ikibadilishwa bila kufanyiwa tafiti za kina na kujidhihirisha kwa masilahi mapana na mustakabali wa taifa.

 Alisema, “tunahitaji elimu bora inayomuwezesha mwanafunzi kutatua changamoto za maisha za kila siku nje ya darasa.”

Alisema wanafunzi hawasomi kwa ajili ya kushinda mitihani na kupata vyeti, bali kwa ajili ya maisha na mfumo wa kuwezesha hayo lazima uwe imara la sivyo, baada ya miaka michache Tanzania itakuwa taifa la ajabu.

 “Litakuwa taifa la ajabu sana ambalo vijana walioandaliwa kwa gharama kubwa kuwa wajenzi wake watajikuta wanakuwa vibarua na watumwa katika nchi yao wenyewe, au wataunguza viwanda na kuzika sekta hizo,” alisema.

Kiongozi huyo wa dini alisema tayari ilishawahi kutokea viwanda vilivyoanzishwa na Mwalimu Nyerere kupotea japo hivi sasa vinafufuliwa, lakini haijulikani kama vitaendelea kudumu baada ya Rais John Magufuli kumaliza muda wake.

 “Dunia itaharibiwa sio na watenda mabaya, bali kwa ukimya wa watu wema wakati maovu yakitendeka,” alisema wakati akimnukuu mwanasayansi wa Kijerumani, Albert Einstein aliyezaliwa Machi 14, 1879 na kufariki 18 Aprili 1955.

Akizungumzia suala la kulegeza viwango vya ufaulu, kiongozi huyo wa kiroho alisema, ubora wa elimu hauwezi kupimwa kwa kulegeza vigezo vya ufaulu ili kuongeza idadi ya waliofaulu, kwa kuwa kufanya hivyo ni kuongeza vipele na majipu ndani ya nchi.

Alisema, ni maajabu kuona wanaokuwa na ufaulu wa chini ndiyo wanaelekezwa kuwa walimu kwa kuwaandaa wanafunzi.

 “Je hiyo ni sahihi? Kama kila taaluma huundwa katika mikono ya mwalimu, tunategemea muujiza gani wa kupata wanasheria bora, mahakimu wanaohukumu kwa haki, madaktari bora waliopikwa wakaiva wakati walimu hawakupikwa wakapikika?”

Alisema, kufanya hivyo ni kuandaa taifa la wababaishaji, wazushi, wasiokuwa wazalendo, wasio na maadili na wasioamini katika misingi ya kujitegemea na kuchapa kazi.

Kwa mujibu wake, vijana wengi watakaozalishwa ni wale wanaoamini njia za mkato kama kupiga ramli, kucheza kamari, kujiunga na dini za kishetani ili kufikia maendeleo.

 Alisema, “hawa ni wale wanaosubiri mchungaji wao kuwaombea ili wapate muujiza wa kufaulu, kupata kazi na ndiyo hawa walimu wanaochekwa na wanafunzi wenye akili za kuzaliwa na matokeo yake ni hasira za walimu kwa madai ya kuwafundisha adabu.”

Alilitaka serikali kufanya tathmini juu ya ujinga na kupambana na tatizo hilo kwa kutoa elimu bora inayokidhi viwango vya ujenzi wa dhamiri safi.

Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dodoma, Job Malyampa, amewataka waumini wa madhehebu ya Kikristo kuwa wavumilivu katika kipindi hiki wanachopitia majaribu magumu kwakuwa ndiyo maisha aliyopitia Yesu Kristo.

Akihubiri katika Kanisa la Mtakatifu John jijini Dodoma, Mchungaji Malyampa alisema, “kikubwa tuangalie amani yetu tuliyonayo. Mtangulizeni Mungu kwa kila hatua; hata kama mtakutana na maisha magumu msikate tamaa wala kuyumba lakini jipeni moyo mtashinda.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Diwani, wananchi wengine 463 wahama Ngorongoro

Spread the loveMakamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro ambaye pia...

ElimuHabari Mchanganyiko

GGML yawapa mbinu wanafunzi Geita Boys kufikia malengo ya kitaaluma

Spread the loveKampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa mafunzo maalumu...

Habari MchanganyikoKimataifa

Shule zafungwa kutokana na ongezeko la joto

Spread the loveSUDAN Kusini imeamuru kufungwa kwa shule zote kuanzia leo Jumatatu,...

Habari Mchanganyiko

Bunge laja na Marathon kuchangia ujenzi wa sekondari

Spread the loveBUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linatarajia kukusanya fedha...

error: Content is protected !!