April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif jabali kuu ACT-Wazalendo 

Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo

Spread the love

HAIKUWA rahisi hivyo kwa wafuasi wa mwanasiasa gwiji nchini na mtetezi mkuu wa Zanzibar yenye mamlaka kamili, Maalim Seif Shariff Hamad, kuamini kuwa atauvuta umma na kuridhiwa kuongoza Chama cha ACT Wazalendo. Anaripoti Jabir Idrissa, Dar es Salaam … (endelea).

Hata pale alipoonesha kumzidi maarifa ya kiuongozi kwa mbali Shungushela Ngaki waliposhiriki mdahalo wa wawaniaji nafasi za juu za uongozi katika chama hicho juzi tarehe 13 Machi, kwenye ukumbi wa Mlimani City, haikutosha kumhakikishia Maalim Seif ushindi mkubwa wa kura.

Mazingira yapo wazi: ni mpya kwa ACT-Wazalendo baada ya kujiunga mwaka mmoja uliopita akitokea Chama cha Wananchi (CUF); na imekuwa mara yake ya kwanza kutumia jukwaa la chama hicho kuomba ridhaa ya wanachama wa kawaida wanaotoka majimboni Tanzania Bara na Zanzibar.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, wa pili na ambao kwa namna ulivyojionesha umefana kumekijengea chama hicho hadhi ya kuwa kinachokua kwa kasi ya 4G miongoni mwa vyama vya siasa nchini Tanzania, ukiacha waliotoka Unguja na Pemba ambako kwake ndio uwanja wa nyumbani kisiasa, wametoka wilaya za mbali.

Sio Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga na Dar es Salaam tu kule alikozoeleka kama mwanasiasa makini anayejua kuzisarifu siasa za taifa hili la Jamhuri ya Muungano la karibu watu milioni 60, bali mkutano umepata wajumbe kutoka wilaya za mbali kama vile mkoani Ruvuma, Kigoma, Bariadi, Bukoba, Mara, Tabora, Singida na Arusha.

Mara ya mwisho kwa Maalim Seif kufanya hivyo ilikuwa ni mwaka 2014 pale alipopanda kiriri mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF, akiwania nafasi ya katibu mkuu.

https://youtu.be/BIFrNefqOKo

Ndani ya ACT-Wazalendo, hajawahi kuwa maarufu. Lakini pengine hakuwahi kufikiria atajajikuta kulazimika kuomba kura ili ashike nafasi ambayo itamuweka chini kidogo ya mkuu wa chama – Kiongozi wa Chama (KC), Zitto Zuberi Kabwe.

Ni sawa haikuwa rahisi wala kupata kufikiriwa. Ndo imetokea sasa. Usiku wa manane kuamkia leo tarehe 15 Machi 2020, mwanasiasa huyu mzaliwa wa mwaka 1943, kijiji cha Nyali, jimbo la Mtambwe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ameibuka kidedea uchaguzini. Ndiye sasa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo.

Na juu yake, amebakia Zitto, mwanasiasa kijana wa mfano wa kichuguu kwake kisiasa; na isitoshe, hana hata ziraa moja ya kutamba kuweza kumzidi maarifa au ujuzi wa mambo, iwe ya kisiasa, kiuchumi au kidiplomasia.

(Zitto amechaguliwa kwa kura 276, ukiwa ushindi wa asilimia 73.6 wa kura 367 za halali zilizopigwa huku kura nane zikiwa zimeharibika. Ismail Jussa Ladhu, mwenyekiti wa kamati ya mikakati ya chama, amepata kura 91, sawa na asilimia 24.2).

Katika wajumbe 361 waliopiga kura ya kumchagua mwenyekiti, Maalim Seif amepata kura 337 na kujipatia ushindi wa asilimia 93.35 akimshinda kwa mbali Kaheeza Shilungushela Ngaki aliyeshiriki naye mdahalo.

Ngaki, mfugaji wa ng’ombe kutoka mkoani Shinyanga, ambaye alijinasibu wakati wa mdahalo huo kuwa yu mzoefu wa siasa na aliyeazimia kujenga ACT-Wazalendo kuwa chama bora nchini, alipata kura nne (asilimia 1.10).

Maalim Seif alimtupa Yeremia Maganja aliyemfuata wa pili akiwa amepata kura 20, sawa na asilimia 5.55. Maganja ndiye amekuwa akikaimu nafasi ya uenyekiti tangu mwaka jana.

Ushindi huo ulipokewa kwa shangwe kubwa na wanachama waliokuwa wamechoka kwa vile walisubiri sana kupata matokeo baada ya uchaguzi wenyewe kuanza saa 5 usiku Jumamosi. Kwanza ilipigwa kura ya kumchagua Kiongozi wa Chama.

Shangwe liliibuka kwa sababu nyingi: kwanza ushindi hushangiliwa na waliomtarajia ashinde. Pili chama kilimtaka ashinde kwa kumlinganisha na washindani wake na kibarua kigumu cha kuongoza harakati za kuondoa utawala unaozoea udhalimu wa CCM.

Lakini sababu nyingine ni ukweli kuwa wakati mwingi wajumbe wakisubiri uchaguzi, ndani na kwenye mazingira ya ukumbi, palienea uvumi hasa kwa wale waliotoka Zanzibar, wa kuwepo njama za kutaka kumkwamisha Maalim Seif ili afedheheke.

Uvumi ulioandama wajumbe na wasiokuwa wapigakura katika mkutano mkuu, ulielekeza shutuma kwa “wabaya wa kisiasa” wa kiongozi huyo, kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) hasahasa wale wa Zanzibar. Eti walimpangia njama aangukie pua.

Vyanzo vya taarifa vilithubutu kumtaja kiongozi wa ngazi ya juu katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa aliongoza njama hizo, akitumia staili ya kumlaghai mshindani mmojawapo.

Imeelezwa kuwa sehemu ya kinachoitwa “ushahidi” wa njama hizo, inaweza kujidhihirika siku za hapo usoni kwa mshindani huyo kuhamia CCM.

Akijibu maswali wakati wa mdahalo, Maalim Seif alieleza kuwa anakusudia kukiimarisha chama hicho kiasi cha kufanikiwa kuongeza viti angalau 50 vya bunge upande wa Tanzania Bara baada ya kujihakikishia ushindi mkubwa Zanzibar utakaokiwezesha kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, iliyofanyiwa mabadiliko makubwa mwaka 2010. Ingawa hajatangaza hadharani, Maalim Seif anatarajiwa kuendelea kugombea urais Zanzibar Oktoba 2020.

Kumekuwa na hofu kubwa miongoni mwa viongozi waandamizi wa CCM Zanzibar kuwa kushinda kwake wadhifa huo si tu kutafuta ndoto zao za kumfikisha mwisho wa harakati za kuipatia Zanzibar ukombozi wa kiuchumi, bali pia kutahatarisha maslahi yao na pengine kutarajia “maisha magumu” ya kustaafu chini ya uongozi wa Maalim Seif.

Ni wao walipanga mpango wa kupitisha sheria – kutokana na hoja binafsi iliyokuwa iwasilishwe Baraza la Wawakilishi na Hamza Hassan Juma wa Shaurimoyo – ya kushurutisha kuwa mgombea urais, uwakilishi na udiwani Zanzibar awe ametimiza angalau miaka miwili ya uanachama wa chama kitakachomdhamini.

Hoja hiyo iliyokribia kuzua mgogoro ndani ya chama chao, ingawa iliwasilishwa ofisi ya Spika Zubeir Ali Maulid, haikupangiwa muda wa kuwasilishwa rasmi mbele ya Baraza wakati wa mkutano wake uliomalizika mwezi uliopita.

Ilionekana hoja hiyo ilikuwa imelenga kumkwamisha Maalim Seif na kundi lake la viongozi waliohama CUF katika kile walichokiita “kushusha tanga na kupandisha tanga.”

Maalim Seif, akiwa katibu mkuu, alitangulia kuhama CUF na kufuatwa haraka na kundi la viongozi na wanachama baada ya chama hicho kukamilika kudhoofishwa na mgogoro kwenye uongozi.

Siku zote Maalim Seif na wenzake waliamini kuwa mgogoro huo uliowafikisha kufungua kesi kadhaa mahakamani, ulikuwa ni kazi ya CCM na dola waliopandikiza kwa kuitumia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyomtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti ilhali alishajiuzulu mwaka mzima.

error: Content is protected !!