MAALIM Seif Sharif Hamad, Mgombea Urais Zanzibar kupitia ACT- Wazalendo amewakaribisha wale wote ambao wanataka kumwekea pingamizi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufanya hivyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Unguja … (endelea).
Maalim Seif ametoa kauli hiyo jana Jumanne tarehe 8 Septemba 2020 alipozungumza katika Kongamano la Vijana wa ACT-Wazalendo visiwani humo.
Tayari Maalim Seif amekwisha kuchukua fomu za utezi wa kugombea urais ZEC katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020.
Fomu hizo amezirejesha leo Jumatano tarehe 9 Septemba 2020.
Amesema, kuna watu wa vyama vingine wamepanga kumwekea mapingamizi ZEC ili asiteuliwe kugombea.
Maalim Seif ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo anawakaribisha watu wanaotaka kumwekea pingamizi akisema anafahamu namna ya kupangua mapingamizi yao.
“Nasikia kuna watu washapangwa na vyama vingine kuniwekea pingamizi, nawakaribisha sababu kuniwekea pingamizi yeye anakuja kutoa haja zake na ushahidi wake na mimi naujua vilevile.”
“Sioni kama kuna pingamizi yoyote, kama itasimama juu yangu. Mimi nimezaliwa Mtambwe hamjui ninyi? Ndiyo sifa ya kwanza ya mgombea urais awe Mzanzibar wa kuzaliwa sio Mzanzibar mkaribishi,” amesema Maalim Seif.
Leave a comment