Tuesday , 19 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Maalim Seif amtwisha Mbowe mzigo wa ushirikiano, yeye amjibu
Habari za Siasa

Maalim Seif amtwisha Mbowe mzigo wa ushirikiano, yeye amjibu

Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo
Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kukubali kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo Jumanne tarehe 4 Agosti 2020 wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa Chadema unaofanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, mkutano mkuu huo, utamthibitisha Tundu Lissu kuwa mgombea urais wa Tanzania, Salum Mwalimu, mgombea mwenza na Said Issa Mohamed kuwa mgombea urais wa Zanzibar.

Pia, mkutano huo, utapitisha Ilani ya uchaguzi ya Chadema.

Maalim Seif ambaye amezungumza kwa niaba ya vyama vya siasa vilivyohudhuria mkutano huo, ameanza kuzungumza kwa kuwahoji wajumbe wa mkutano huo, “mko tayari kwa kazi” kisha akajibiwa ‘tuko tayari.”

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

“Kwa niaba ya ACT-Wazalendo, nawapongezeni sana kwa kuweza kuandaa mkutano mkubwa kama huu, tena mkutano umefikia viwango vyote,” amesema Maalim Seif.

“Tupo katika kuelekea uchaguzi mkuu. Tunayajua mazingira ya uchaguzi wa Tanzania. Tume zetu tunazijua wenyewe, wanasema ziko huru lakini maelezo yao wanasema yapo kwa mujibu wa sheria.”

“Tanzania kwa sasa hakuna tume huru, kama hakuna tume huru, usitarajia uchaguzi kutendeka kwa haki,” amesema Maalim Seif

Hata hivyo, mara kadhaa, Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli amewahi kunukuliwa akisema, Serikali anayoingoza itahakikisha uchaguzi huo unakuwa amani, huru na haki.

Pia, Rais Magufuli aliionya yeyote atakayethubutu kuvuruga uchaguzi huo, atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Maalim Seif huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo, amesema, “wito wangu kwa Chadema, tusitegemee kama tume itatenda haki, tujipange, tujipange, tujipange kuhakikisha kwamba endapo tutashinda, hakuna wa kuzuia ushindi wetu.”

“Lakini hatutaweza kukubali wafanye watakavyo, tuseme hewala hapana. Ng’ombe atakavyoanguka atachinjwa hivyo hivyo” amesema.

Maalim Seif amesema “ndiyo maana anasema hili ni jukumu letu sote, tusitegemee kuna mjomba atatusaidia, sisi wenyewe tujipange vizuri.”

Kuhusu kushirikiana, Maalim Seif amesema “jana nilimsikia mwenyekiti Freeman Mbowe alisema Chadema wanazungumza na ACT-Wazalendio, nataka kuthibitisha ni kweli.”

“Siyo kwamba vyama vingine tumejipanga, hapana, tulidhani tuweke msingi mathubuti na baada ya hapo vyama vyote makini tunawahakikishieni tutashirikiana,” amesema

“Tungependa, wakati mnafanya mkutano mkuu na sisi kesho tunafanya mkutano mkuu na kabla ya kumaliza, tuwe tumemaliza, tuendelee na mchakato wetu lakini msimamo wa ACT-Wazalendo, hakuna ‘choice’ lazima tushirikiane,” amesema.

Amesema, kilichojitokeza uchaguzi mkuu mwaka 2015 ni ishara kwamba ushirikiano imara, utawezesha kuing’oa CCM madarakani.

“Nina amini, mkutano huu utatoka na mgombea urais na sisi tutatoka na mgombea urais lakini agizo nililopewa na Baraza Kuu la ACT-Wazalendo, tutahakikisha sisi tunaendelea kutafuta umoja hadi dakika za mwisho,” amesema

“Tunaweza kukaa kabisa na kusema huyu ni wetu sote, ombi langu, sote tuwe ‘serious’ sote tuna lengo moja ‘please please please’ tuyaweke maslahi yetu kando. Watanzania wanataka mabadiliko, kama ukizungumza na Watanzania kumi, saba watasema wapinzani unganeni.”

“Hilo ndilo takwa la Watanzania. Niwaombe mwenyekiti mwenzangu (Mbowe), mzigo huu upo juu ya bega langu, bega lako. Sisi wawili tukishakubaliana, viongozi wengine hawawezi kukubali. Tuwaunganishe Watanzania. Mpinzani wetu ni mmoja tu. Mpinzani wetu ni CCM peke yake,” amesema Maalim Seif huku akishangiliwa

Jana, Mbowe akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Chadema, aliwaomba wanachama na viongozi wa chama hicho, kujiandaa kwa ushirikiano baina yao na ACT-Wazalendo.

Mbowe alisema, katika ushirikiano huo, wana Chadema wajiandae kukubali kuachiana majimbo na kata kwa maeneo ambayo wataona ACT-Wazalendo au Chadema wana nguvu ili kusimamia mgombea mmoja.

Leo tena katika mkutano huo, Mbowe amesema, chama hicho kinauwezo wa kusimamia wagombea wote wa udiwani na ubunge lakini “katika kushirikiana, huwezi kupata vyote” hivyo kuna wakati tutaachiana baadhi ya mambo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Zanzibar mbioni kuanza uchimbaji mafuta na gesi baharini

Spread the loveSERIKALI ya Zanzibar, imekamilisha mchakato wa uchimbaji wa mafuta na...

Habari za Siasa

Wizara ya afya yataja mafanikio 10 miaka mitatu Samia madarakani

Spread the loveWIZARA ya Afya imetaja mafanikio 10 iliyoyapata ndani ya miaka...

Habari za Siasa

Mbozi walilia kuwa manispaa, majimbo 3

Spread the loveHALMASHAURI ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe imeeleza dhamira yake...

Habari za Siasa

Wabunge waitaka TPDC kuongeza kasi ya kuunganisha wateja gesi asilia

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini...

error: Content is protected !!